Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya
Hesabu za Serikali Zitto Kabwe akisisitiza jambo wakati wajumbe wa kamati hiyo
walipofanya kikao na watendaji wa Wizara ya Fedha, jijini Dar es Salaam jana.
Kulia ni Katibu wa kamati hiyo, Michael Kadebe. Picha na Michael Jamson.
Na Beatrice Moses na Fidelis
Butahe, Mwananchi
Dar es Salaam. Wakati Mwenyekiti wa
Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe akisisitiza kuwa hesabu za
Chadema ni miongoni mwa ambazo hazijakaguliwa, chama hicho kimeishutumu kamati
hiyo kwa kuagiza kusitishwa kwa ruzuku kwa vyama vya siasa na kusema hatua hiyo
ni ubabe.
Wakati Chadema wakitoa kauli hiyo,
jana Zitto alisema vyama vya siasa tisa vikiwamo Chadema, CCM na CUF vinatakiwa
kufika mbele ya PAC Oktoba 25 mwaka huu, kwa ajili ya kujieleza na kwamba chama
kitakachokaidi, sheria za Bunge zinaeleza wazi, kwamba wahusika wanaweza
kufungwa jela siku saba.
Chadema kilisema kuwa PAC kabla ya
kuchukua hatua, ilipaswa kuwapa nafasi ya kuwasikiliza viongozi wa vyama
husika, kumhoji Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Msajili
wa vyama vya Siasa ambao wameshindwa kutimiza wajibu wa kukagua hesabu hizo kwa
miaka minne.
Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa
Chadema, Anthony Komu alisema jana kuwa, uamuzi wa PAC utaviathiri vyama kwani
bajeti zake zimezingatia kuwapo kwa ruzuku.
“Kuna vyama ambavyo vinategemea
ruzuku kulipa mishahara ya wafanyakazi wake, Chadema ingawa tuna vyanzo vingine
vya mapato, tunaitegemea kukamilisha bajeti yetu kwa fedha za ruzuku ambazo
zinatusaidia kwa asilimia 45. Ni tabia mbaya kuchukua uamuzi kwa kibabe na
kuhukumu kabla ya kutusikiliza siyo haki hata kidogo,” alisema Komu.
Alitetea chama chake kwamba kimekuwa
na utaratibu wa kuwasilisha hesabu zilizokaguliwa ambapo alitoa ushahidi wa
barua ya Msajili wa Vyama vya Siasa ya April 16, 2012 ikithibitisha kwamba
hesabu zao zipo sawa baada ya kuziwasilisha katika ofisi hiyo.
“Chadema tunataka ukaguzi wa hesabu
usijikite katika fedha za ruzuku pekee bali katika vyanzo vyote vya mapato ya
vyama, tatizo CAG alitueleza kwamba anakabiliwa na upungufu wa rasilimali watu
kwa hiyo PAC walipaswa kuliangalia tatizo hilo na kutafuta ufumbuzi,” alisema
Komu.
Zitto juzi alikaririwa na vyombo vya
habari akieleza kuwa Serikali ilitoa kiasi cha Sh67.7 bilioni kama ruzuku kwa
vyama tisa vya siasa tangu mwaka 2009, lakini vyama hivyo havijawahi
kuwasilisha taarifa za ukaguzi wa hesabu zake kwa msajili kama sheria
inavyoagiza.
Mbunge huyo wa Kigoma Kaskazini
(Chadema), aliamuru Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, kusimamisha
utoaji wa ruzuku hadi hapo vitakapowasilisha ripoti ya ukaguzi na makatibu wake
wakuu kuhojiwa.
Miongoni mwa vyama vilivyotajwa ni
APPT-Maendeleo lakini jana Rais Mtendaji wa Chama hicho, Peter Mziray alisema
chama chake hakijawahi kupewa kiasi cha Sh217 milioni kama inavyodaiwa na PAC.
Mziray alikiri walianza kupata ruzuku
2009 ila inasema ilikuwa kidogo kiasi cha Sh 50,000 kwa mwezi na baadae kupanda
Sh 275,000 kwa mwezi.
Alisema kiasi walichopata kuanzia
mwaka 2009 ni kiasi cha Sh12 milioni tu. “APPT-Maendeleo haina uwakilishi
bungeni kwa hiyo haiwezi kupata kiasi hicho kikubwa cha fedha,” alisema Mziray.
Zitto akaza kamba
Jana Zitto alivitaka Chadema, CUF na
CCM kuacha kupiga kelele katika vyombo vya habari na badala yake viwasilishe
taarifa za ukaguzi wa matumizi yake katika Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa.
“Vyama hivi visilete ujanja ujanja,
hizi ni fedha za umma lazima zikaguliwe. Tatizo la CCM, CUF na Chadema
wanahusisha suala la kuwasilisha taarifa za ukaguzi na nafasi yangu ya Naibu
Katibu Mkuu wa Chadema, sifanyi kazi kwa niaba ya Chadema mimi nafuata sheria
za Bunge na katika hili sitacheka na mtu,” alisema Zitto jana wakati
akizungumza na wanahabari katika ofisi ndogo za bunge, Dar es Salaam.
Zitto alisema Kanuni za Bunge
zinataka ukaguzi wa hesabu ya serikali huku akionya kuwa sio sahihi kwa vyama
hivyo kulichukulia suala hilo kama jambo binafsi. Alisema chama husika
kikishakaguliwa na ofisi ya CAG, na taarifa husika hupigwa muhuri wa ofisi hiyo
ya mkaguzi.
Zitto alisema vyama hivyo vinatakiwa
kuichukua taarifa hiyo na kuipeleka Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ambaye
hutangaza taarifa hiyo katika gazeti la Serikali ili ijulikane wazi mapato ya
vyama husika.
“Hilo ndio halijafanyika, waulizeni
hao CCM, CUF na Chadema lini wamekaguliwa na kama wamekaguliwa mbona taarifa
zao hazipo katika ofisi ya msajili, sisi tunatambua taarifa za ukaguzi wa vyama
ambazo zipo ofisi ya msajili,” alisema Zitto na kuongeza:
“CCM na Chadema ndiyo wana kelele
zaidi, hatuwezi kusimamia Serikali wakati sisi wenyewe ni wachafu, najua kila
mtu alikuwa akiogopa kueleza ukweli kuhusu ukaguzi kwa vyama vya siasa, kuanzia
CAG, Mwenyekiti aliyepita wa PAC hadi Msajili wa vyama.”
Alisema ruzuku za vyama hivyo
ilitakiwa kusimamishwa tangu miaka mitatu iliyopita, kwa maelezo kuwa Sheria ya
Vyama vya Siasa Ibara ya 14(4) inaeleza kuwa Ofisi ya Msajili wa Vyama ina
uwezo wa kufungia ruzuku ya chama fulani, mpaka hapo kitakapowasilisha hesabu
zake.
“Katika hili CAG na Msajili wa Vyama
kila mtu atabeba mzigo wake, inaonekana kulikuwa na kuogopana lakini mimi
nimekuwa Mwenyekiti wa PAC hivi karibuni lazima nisimamie sheria na hiyo ndiyo
kawaida yangu,” alisema Zitto.
Msajili anena
Msajili wa Vyama vya siasa nchini,
Jaji Francis Mutungi alizungumza na gazeti dada la The Citizen juzi na
kufafanua kuwa ofisi yake itayafanyia kazi maoni ya PAC na kuongeza kuwa uamuzi
wowote utakaotolewa utafanyika kwa mujibu wa sheria za ofisi yake.
Alisema kuwa alipitia maoni
yaliyotolewa na Zitto kuhusu vyama kufungiwa kupewa ruzuku na kwamba
atayafanyia kazi licha ya kuwa pia alitoa maoni binafsi kuhusu suala hilo.
Alisema hawezi kuchukua hatua za
haraka kuchukua hatua za kuvifungia vyama hivyo mpaka atakapokutana na Makatibu
Wakuu wa vyama hivyo ambavyo vimetajwa na Zitto kwamba havijawasilisha ukaguzi
wao.
“Nataka kuzungumza nao ili nijue
kwanini wameshindwa kuwasilisha ukaguzi kabla ya kuamua kuchukua hatua za
kisheria” alisema.
No comments:
Post a Comment