Thursday, October 31, 2013

Syria yateketeza vifaa vya kemikali



Shirika la kimataifa la kusimamia matumizi ya silaha za kemikali, limesema kuwa Syria imetangaza kwamba vifaa vya kuzalisha, kuchanganyia na kujazia silaha za kemikali vimeharibiwa.

Tangazo hili limetolewa siku moja kabla ya kumalizika kwa tarehe ya mwisho iliyowekwa na Shirika la Kuzuia Silaha za Kemikali duniani, OPCW.
Msemaji wa OPCW amesema silaha hizo zimewekwa lakiri ili kudhibiti matumizi yake.
Wakaguzi wa silaha hizo walitumwa Syria kufuatia tuhuma dhidi ya serikali ya nchi hiyo inayoshutumiwa kutumia silaha za kemikali katika maeneo ya raia.

Kwa upande wake Syria inakanusha shutuma hizo na badala yake imewashutumu wapinzani kuhusika na matumizi ya silaha za kemikali katika vita vinavyoendelea nchini humo kati ya majeshi ya serikali na waasi.
Mashirika ya ujasusi ya nchi za Magharibi, yatakuwa yanafuatilia kwa karibu tangazo la Syria la kuteketeza silaha zake za kemikali.

Ukaguzi huu ni makubaliano yaliyofikiwa kati ya Urusi na Marekani, baada ya Marekani kutishia kutumia nguvu za kijeshi dhidi ya serikali ya Syria, kufuatia tuhuma hizo.
Kwa sasa vifaa hivyo haviwezi kutumika.
Syria imetakiwa kuharibu yenyewe silaha zake za kemikali ifikapo katikati ya mwaka 2014.
Chanzo: BBCSwahili

No comments: