Zanzibar. Katibu wa Baraza la
Wawakilishi Zanzibar (BLW), Yahya Khamis Hamad amesema Rasimu ya mwisho ya
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lazima izingatie kuwa na utaratibu wa
kupata Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa zamu kati ya Bara na
Zanzibar.
Alisema mfumo huo mpya utasaidia
kuimarisha misingi ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na kutaka Tume ya
Mabadiliko ya Katiba kuzingatia maoni ya wananchi waliopendekeza mfumo huo
wakati wa utoaji wa maoni ya mabaraza ya Katiba.
Aliyaeleza hayo katika mahojiano maalumu
na gazeti hili yaliyofanyika Chukwani Unguja jana na kutaka Wajumbe wa Bunge la
Katiba kuweka kando misimamo ya vyama vyao na kuangalia masilahi ya kila nchi
baina ya pande mbili za Muungano.
Hamad alisema mfumo wa urais wa zamu
utaipa nafasi Zanzibar badala ya mfumo wa sasa unaotumika ambao unaonyesha
Zanzibar itawachukua muda mrefu kutoa nafasi ya urais wa Muungano baada ya Rais
Ali Hassan Mwinyi kuchukua nafasi ya Rais mstaafu Julius Nyerere aliyeondoka
madarakani mwaka 1985. Alisema nafasi hiyo kuendelea kwake kupatikana kwa
ushindani, huku wanasiasa kutoka Zanzibar kuonekana wakikabiliwa na nguvu haba
za kiushawishi wakati siasa za Muungano zikihitaji nguvu na kuwekeza mitaji ya
kisiasa na kiuchumi linaweza kuwanyima haki ya kushika nafasi hiyo.
Hata hivyo, alisema baadhi ya
wanasiasa wa Bara wakianza kutajwa na wengine wakaonekana kufanya maandalizi ya
kampeni hizo, upande wa Zanzibar wamebaki kimya kana kwamba hakuna wenye uwezo
na nia ya kushika nafasi hiyo.
“Sioni sababu ya kuwa na sheria moja ya
vyama vya siasa kama muundo wa Serikali tatu utapita, muhimu jambo hilo
kuliangalia kwa manufaa ya pande mbili za Muungano,” alisema Hamad.
Hata hivyo, alisema iwapo Rasimu mpya
ya Katiba itapitishwa na Bunge la Katiba na kuruhusiwa mgombea binafsi pia Katiba
ya Zanzibar ya mwaka 1984 italazimika kuangaliwa upya ili kulizingatia suala
hilo kwa vile ndiyo njia ya uimarishaji wa msingi ya demokrasia.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment