• Mnyika
apinga, ataka posho zifutwe, Lissu awafunda
na Mwandishi wetu
WAKATI watumishi wa umma wakitaabika
na mishahara midogo, huku wakipendekeza marupurupu ya wabunge yapunguzwe,
wabunge wa CCM juzi waliwaweka kitimoto viongozi wa Bunge wakitaka mishahara
yao ipandishwe.
Madai hayo yanakuja zikiwa ni siku
chache tangu Spika wa Bunge, Anne Makinda, naye kunukuliwa na vyombo vya habari
akidai marupurupu ya wabunge ni madogo hatua inayowafanya wengi wao kuishi
maisha magumu baada ya kupoteza ubunge.
Hata hivyo, kikao hicho kilikuwa na
upinzani mkali baada ya wabunge wa CHADEMA, John Mnyika na Tundu Lissu kupinga
hoja za wabunge wa CCM wakiwataka wawe na uchungu na wananchi.
Sakata hilo lilitokea juzi kwenye
kikao cha wabunge na uongozi wa Bunge cha kupeana utaratibu wa ratiba za
shughuli za Bunge (briefing). Baada ya wabunge kupata taarifa fupi ya ratiba
walipata nafasi ya kujadili mambo yanayowahusu, hususani huduma kwa wabunge.
Sintofahamu ilikuja pale wabunge wa
CCM walipotoa hoja ya kuwataka viongozi wa Bunge kuwaambia ni maslahi gani
wanayapata kwa kuwachagua wao hadi sasa.
Chanzo chetu kilidokeza kuwa mbunge
mmoja kutoka mkoani Tabora (jina tunalihifadhi) alihoji hilo na kuwataka
viongozi wao kama wameshindwa kazi basi wajiuzulu kwa hiari huku akisema
wabunge wana maslahi madogo, hivyo kuhitaji kuongezewa mishahara.
“Alitoa hoja ya kuahirisha kujadili
hoja nyingine ili wajadili mishahara yao ambayo alidai ni midogo na kutaka
iongezwe mara moja kwa kuwa wabunge wana hali ngumu sana,” kilisema chanzo
hicho.
Baadaye alifuatia mbunge mwingine
kutoka mkoani Dodoma ambaye alihoji juu ya posho wanazopata na kusema mshahara
ni mdogo, hivyo akapendekeza malipo ya sh milioni 12 ili waweze kufikia viwango
vya nchi nyingine kama Kenya.
“Lakini mbunge mwenzake kutoka mkoani
Mara (anamtaja) alitoa hoja ya viongozi wa Bunge kukaa viti vya mbele ili
wahojiwe na kama hawataki wafukuzwe kazi mara moja na kuchagua makamishina
wengine pamoja na Spika na Naibu Spika,” kiliongeza.
Chanzo hicho kilisema kuwa wabunge
hao walikuwa na umoja na kushikana kupigania posho na mishahara mikubwa zaidi
wakisema hawatosheki.
Kwa mujibu wa chanzo hicho, Mbunge wa
Ubungo, John Mnyika (CHADEMA), nusra atibue mjadala huo baada ya kuwapinga
watoa hoja na kupendekeza posho za vikao zifutwe kama kweli wabunge wanaipenda
nchi yao na wananchi wao.
Inaelezwa kuwa wabunge walipinga hoja
yake kwa kuguna na kunong’ona wakiashiria kutounga mkono, hatua iliyomfanya
mbunge mwenzake wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (CHADEMA) kuingilia kati.
Lissu aliwaambia wabunge waache
umbumbumbu wa kutosoma sheria ya utumishi wa Bunge kwa kuanza kutaka kumtoa
spika na naibu wake madarakani, akisema wao sio sehemu ya uamuzi wa malipo kwa
wabunge na kwamba malipo yao yapo mikononi mwa rais.
Kikao hicho kiliahirishwa kwa
mahitaji kufanyika kwa kikao kingine rasmi kwa ajili ya kujadili maslahi ya
wabunge, huku wabunge wakitaka spika awepo na Waziri Mkuu ili waweze kuwahoji
juu ya malipo yao.
Wadadisi wa masuala ya siasa wanaiona
hali hiyo kama hatua ya wabunge wengi kutokuwa na matumaini ya kurudi bungeni
kwa kipindi kingine.
Kwamba wanashinikiza malipo makubwa
ili fedha hizo ziwasaidie kwa ajili ya maandalizi ya kuhakikisha wanakuwa na
hazina pindi wanapomaliza muda wao mwaka 2015.
Chanzo:
Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment