Wizara
ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, imesema masomo ya dini na mengine,
yataendelea kufundishwa pamoja na kufanyiwa mitihani katika ngazi zote.
Alisema
wizara hiyo haijakubaliana na waraka wa elimu kutoka Tanzania Bara wa kuyafanya
masomo hayo kuwa ya hiari, hivyo yasichangie asilimia yoyote katika ufaulu wa
mtahiniwa.
Naibu
Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Bw. Abdallah Mzee, ameyasema hayo Zanzibar jana
wakati akizungumza na waandishi wa habari ili kukanusha taarifa zilizotolewa na
baadhi ya vyombo vya habari zikidai Wizara hiyo imeondoa mtaala wa masomo ya
dini na Kiarabu kwenye mitihani ya Taifa.
Alisema
watendaji kutoka Wizara ya Elimu Tanzania Bara, walikutana na wenzao wa
Zanzibar ili kujadili waraka wa elimu waliokuja nao uliokuwa unataka kufanyike
mambo mapya.
Bw.
Mzee aliongeza kuwa, katika waraka huo wenzao kutoka Bara walipendekeza masomo
ya dini ya Kiislamu, Kikristo, lugha ya Kiarabu, Kifaransa, Kompyuta, muziki
yawe ya hiari kwa mwanafunzi kuyasoma na yasisaidie ufaulu wowote katika
viwango vya madaraja ya ufaulu.
"Waraka
ulipendekeza masomo hayo yakiwemo dini na Kiarabu yasisaidie chochote katika kupandisha
au kushusha vision ya mtahiniwa," alifafanua Bw. Mzee.
Aliongeza
kuwa, ilipendekezwa utaratibu huo mpya uanzwe kufanyiwa kazi kwa wanafunzi
ambao
wataingia kidato cha kwanza mwaka 2014 na ifikapo 2017, wanafunzi hao wautumie
katika kidato cha nne.
Hata
hivyo, Bw. Mzee alisema watendaji wa Zanzibar waliupinga utaratibu huo kwa kuwa
haukidhi matakwa ya Zanzibar.
"Watendaji
wetu waliupinga waraka huo kwani hautufai na unatofautiana sana na sisi
kulingana na hoja zetu tulizotoa, pia walikubali kuurudisha ili usiweze
kufanyiwa kazi," alisema.
Alisema
Wizara ya Elimu Zanzibar, inatoa Mchepuo wa Masomo ya lugha katika skuli
tofauti ikiwemo Sekondari ya Kiponda hivyo itakuwa vigumu kufuata utaratibu
huo.
Akizungumzia
somo la dini, Bw. Mzee alisema soko hilo kwa Zanzibar ni muhimu sana pia ni
miongoni mwa masomo yenye walimu wazuri wa ngazi za Stashahada hadi
Udaktari-PhD na ufundishwaji wake huanzia darasa la kwanza hadi Chuo Kikuu
hivyo kubadili utaratibu isingewezekana.
Aliongeza
kuwa, katika dunia ya sasa, somo kama kompyuta ni muhimu sana hivyo kulifanya
halina ulazima ni kujirudisha nyuma kimaendeleo.
"Licha
ya uhusiano mzuri uliyopo kati ya Wizara yetu na Bara, sisi hatukushirikishwa
katika uanzishwaji wa waraka husika," alisema.
Katika
hali ya kuliweka sawa jambo hilo, Mawaziri wa Wizara hizo Bw. Ali Juma Shamhuna
na mwenzake wa Bara, Dkt. Shukuru Kawambwa, wanatarajia kukutana kesho
kulijadili jambo hilo.
Chanzo: Majira
No comments:
Post a Comment