Thursday, October 31, 2013

Mahakama iliyoibuliwa na Mwananchi kuwa ni chakavu kuvunjwa



Hali ilivyo katika sehemu ya kuhifadhia mafaili ya kesi katika Mahakama ya Wilaya ya Bagamoyo. Picha na Editha Majura

Na Editha Majura, Mwananchi
Bagamoyo.Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Ahmed Kiponzi amesema jengo la Mahakama ya wilaya ya Bagamoyo ambalo liliripotiwa na gazeti hili miezi kadhaa iliyopita kuwa linatishia uhai wa watu wanaofanya shughuli humo kutokana na uchakavu litavunjwa ili kujengwa nyingine mpya.

Anasema kuwa jengo hilo ni chakavu kwa sababu ni la muda mrefu na kwamba wameshaunda kamati ya kulishughulikia.
Akizungumza na Mwananchi ofisini kwake Bagamoyo, Kiponzi anasema kasi ya utendaji wa kamati hiyo katika kushughulikia upatikanaji wa jengo mbadala la mahakama ya Wilaya ilipungua, baada ya aliyekuwa hakimu wa wilaya hiyo, Said Ali Mkasiwa kwenda masomoni nje ya nchi.

Tayari kimetengwa Kiwanja kitakachotumika kwa ujenzi wa jengo jipya, litakalokuwa mbadala wa jengo linalotumiwa sasa kwa shughuli za mahakama ya wilaya.
Hata hivyo hakutaja eneo kilipo kiwanja hicho kwa maelezo kuwa hiyo ni moja ya taarifa zitakazotolewa na kamati ya kushughulikia upatikanaji wa jengo jipya la mahakama hiyo, itakayokutana punde.

Anasema tayari mchoro wa ramani ya jengo litakalokuwa la mahakama ya Wilaya ya Bagamoyo umekamilishwa na kwamba kilichobaki ni kamati kujadili na kutekeleza hatua zilizosalia katika kukamilisha ujenzi huo.

“Usifikiri ni maneno tu, (akitoa kabrasha la michoro ya ramani ya jengo la mahakama na kumkabidhi mwandishi wa makala hii) unaweza kushuhudia mwenyewe mchoro wa ramani ya jengo litakalojengwa kwa ajili ya mahakama ya wilaya; tupe muda kidogo bila shaka utakapofuatilia tena utakuta mabadiliko na tutakupa taarifa nzuri zaidi ya hizi,”anaeleza Kiponzi.

Kwa mujibu wa Kiponzi, kamati hiyo inafanya kazi chini ya uongozi wake kama mwenyekiti huku hakimu mfawidhi wa wilaya hiyo akiwa Katibu na kwamba kutokana na nafasi iliyoachwa na Mkasiwa kuzibwa na hakimu mfawidhi, Liad Chamshama; utendaji wa kamati hiyo utarejea kwenye kasi inayotakiwa.

Shughuli za Mahakama ya Wilaya ya Bagamoyo zinaendeshwa ndani ya jengo la enzi za utawala wa kikoloni. Limechakaa na kuchoka kiasi ambacho kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana mahakamani hapo zinasema mhandisi wa wilaya hiyo, ameishaeleza tena kwa maandishi kuwa halistahili kutumika.

Mkazi wa kijiji cha Miono ambaye ni miongoni mwa watumiaji wa mahakama hiyo, Kilo Khamis Mdete (42) anasema jengo hilo kufanywa ofisi ya wataalamu, wanaotoa haki na adhabu kwa mujibu wa sheria, ni sawa na udhalilishaji.
Anashauri Serikali kutumia rasilimali zake kuwezesha upatikanaji wa haraka wa jengo jipya.
Chanzo: Mwananchi

No comments: