Picha hii ni ya Maktaba
na Abdallah Khamis
WAKATI Rais Jakaya Kikwete na Waziri
wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo, wakiwabeza Watanzania kuwa hawana
uwezo wa kifedha kuwekeza katika utafiti wa gesi na mafuta, mwanasheria maarufu
nchini, Mabere Marando, ametoboa siri za vyanzo vya fedha za wawekezaji wa nje
wanaopigiwa debe na serikali.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara
uliofanyika katika viwanja vya stendi ya Kibiti wilayani Rufiji juzi, Marando
alisema wawekezaji wengi kutoka nje hawaji na fedha mifukoni, badala yake
wanatumia mabenki ya hapa nchini kujipatia mitaji hiyo, jambo alilodai kuwa
linaweza kufanywa na wawekezaji wazawa.
Marando ambaye pia ni mjumbe wa
Halmashauri Kuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na Makamu
Mwenyekiti wa chama Kanda ya Pwani, alisema serikali imeshindwa kuwasaidia
wazawa kwa kuwachukulia dhamana ya kukopa mitaji mikubwa kama inavyofanywa na
nchi nyingine.
Kwamba badala ya kuwawezesha imegeuka
kuwasimanga na kuwabeza kuwa hawana uwezo wa kifedha wa kampuni zao kushiriki
katika michakato hiyo ya kupewa vitalu vya utafiti wa gesi na mafuta. Alisema
hali hiyo ni makusudi ya serikali ya CCM kuwazuia Watanzania kutumia fursa
zilizopo na badala yake inakimbiza fursa hiyo kwa wageni.
“Niliposikia rais akitoa kuli hiyo
niliumia sana lakini nikaja kutambua kuwa huyu mtu hakuwahi kupigika katika
maisha ya tabu na wala hajawahi kufanya biashara kwa maana hao wageni aliokuwa
nao juzi wengi wao wakiwa wanataka vitalu, mimi nimewaandalia nyaraka za kukopa
katika mabenki yetu nchini,” alisema.
Marando aliongeza kuwa mmoja wa
waombaji hao wa uwekezaji katika vitalu vya gesi, ameweka leseni ya kampuni
yake kama dhamana katika moja ya benki hapa nchini ili aweze kupata mkopo,
jambo aliloeleza kuwa linaweza kufanywa na Watanzania wengi wenye dhamana za
kutosha.
Aliongeza kuwa sera ya CHADEMA ni
kuwapa kipaumbele wazawa badala ya wageni katika kumiliki vyanzo vya rasilimali
hali aliyoeleza kuwa ni tofauti na serikali ya CCM.
Marando alisisitiza kuwa makubaliano
ya uwekezaji wa eneo lolote nchini unapaswa uanzie kwa mwekezaji kukubaliana na
mmiliki wa eneo analotaka kuwekeza tofauti na ilivyo sasa kwa serikali kuamua
bila kuwashirikisha wananchi.
Alitolea mifano uamuzi wa serikali
kushindwa kuwashirikisha wananchi katika hatua za awali ni matokea ya migongano
ya mara kwa mara baina ya wawekezaji na wananchi wa maeneo husika.
Chanzo:
Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment