Wanaume sita wa kisomali wamepatikana
na hatia ya kosa la uharamia nchini Uhispania baada ya jaribio lao la kuteka
manowari ya kijeshi ya Uhispania katika ufuo Somalia Januari mwaka 2012.
Mmoja wa wanaume hao, alihukumiwa
miaka 12 na nusu jela wakati wengine watano wakipokea kifungo cha miaka minane
jela kila mmoja.
Wakati kesi hiyo ikiendelea
kusikilizwa mjini Madrid, wanaume hao sita walikanusha kuwa maharamia wakisema
kuwa walikuwa wavuvi waliokuwa wanataka usaidizi kutoka katika meli hiyo.
Wanaume hao hatimaye walisalimu amri.
Manowari ya kijeshi ya Uhispania,
Patino, ilikuwa inashiriki katika harakati za Muungano wa Ulaya dhidi ya
uharamia katika bahari hindi wakati wa jaribuo la watu hao kuiteka.
Kwa mujibu wa viongozi wa mashitaka
wanaume hao walijaribu kuingia kwenye boti hiyo kwa lazima kabla ya saa tisa
mchana saa za Uhispania.
Wasomali hao waliokuwa wamejihami kwa
bunduki aina AK-47 na maguruneti walijaribu kuivamia meli hiyo lakini
walifuatwa kwa kasi na manowari hiyo huku ufyatulianaji risasi ukizuka na
kudumu kwa dakika mbili . Alisema mwendesha mashitaka.
Walianza kutoroka lakini walifuatwa
na wanajeshi wa Uhispania na hatimaye wakasalimu amri.
Wanaume hao sita - Mohamed Abdullah
Hassan, Mohamed Aden Mohamed, Issa Abdullah Issa, Abdillahi Mohamed Gouled,
Mohamed Said Ahmed na Hamoud Elfaf Mahou – walihukumiwa kwa kosa la uharamia
pamoja na kumiliki silaha .
Mmoja wa wanaume hao alipatikana na
kosa la kuwa mwanachama wa genge la wahalifu na kupewa kifungo kirefu kuliko
washukiwa wengine watano.
Wiki jana Umoja wa Mataifa ulisema
kuwa visa vya uhaaramia vimepungua sana katika bahari hindi ikilinganishwa na
hali ilivyokuwa mwaka 2006 kutokana na kuimarishwa kwa usalama.
Chanzo: BBCSwahili
No comments:
Post a Comment