Dar es Salaam. Wakati Serikali ikiendelea kuikalia
ripoti ya Tume ya Kuchunguza Matokeo ya Kidato cha Nne iliyoundwa na Waziri
Mkuu, Mizengo Pinda mapema mwaka huu, baadhi ya wajumbe wake wameanika madudu
mengi yaliyobainika katika uchunguzi huo.
Mmoja wa wajumbe waliounda Tume hiyo
ameliambia gazeti hili hivi karibuni kuwa waligundua mambo mengi
yanayodhihirisha udhaifu mkubwa katika uendeshaji wa sekta ya elimu nchini,
ikiwa ni pamoja na kubaini kuwa idadi kubwa ya wakuu wa shule hawana elimu ya
shahada.
Alieleza kuwa kiutaratibu mkuu wa shule
anatakiwa kuwa na elimu isiyopungua shahada pamoja na mafunzo ya uongozi na
usimamizi. “Kumbukumbu zilionyesha kuwa elimu ya sekondari ya kawaida ina jumla
ya shule 4,528. Wakuu wa shule 1,498 wana shahada ya kwanza au zaidi, 1,703
wana stashahada, 33 wana sifa nyingine” alisema.
Sehemu kubwa ya matokeo ya uchunguzi
huo inasemekana yamejikita zaidi katika kuzitupia lawama taasisi za Baraza la
Mitihani la Taifa (Necta) na Taasisi ya Elimu Tanzania (TIE).
Udhaifu wa kiutendaji kati ya taasisi
hizo mbili unadaiwa umechangia kwa wanafunzi wengi kufanya vibaya kwenye
mitihani ya kidato cha nne mwaka jana, kiasi cha kuilazimisha Serikali kuunda
tume kuchunguza tatizo kutokana na kilio kikubwa cha wadau wa elimu na
wananchi.
Matokeo hayo ya mtihani wa kidato cha
nne uliofanyika mwaka jana yanaonyesha kuwa watahiniwa 240,903 sawa na asilimia
60.6 walipata sifuri, huku wanafunzi 23,520 tu ambao ni sawa na asilimia 5.16
ndiyo waliofaulu na wengine 103,327 sawa na asilimia 26.02 wakiwa wamepata
daraja la nne.
Katika mtihani huo, watahiniwa
397,136 walikuwa wa shuleni na 68,806 wa kujitegemea.
Kutokana na hali hiyo, Waziri Mkuu
Pinda aliamua kuunda Tume iliyoanza kufanya kazi kuanzia Machi hadi Juni mwaka
huu. Tume hiyo iliyokuwa inaongozwa na Profesa Sifuni Mchome ilimkabidhi Waziri
Mkuu ripoti Juni 15, mwaka huu.
Hata hivyo, ripoti hiyo haijawahi
kutolewa hadharani baada ya Tume kumaliza kazi yake, huku Profesa Mchome ambaye
alikuwa Katibu Mtendaji wa Taasisi ya Vyuo Vikuu Tanzania akipandishwa cheo na
kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi.
Kauli ya Profesa Mchome
Profesa Mchome alipotafutwa jana
kuzungumzia kuhusu upatikanaji wa wakuu wa shule alisema, “Mimi hivi sasa ni
katibu mkuu wa wizara siwezi kuzungumzia hilo, kwanza sijaiona hiyo ripoti. Ukitaka
ufafanuzi mzuri mtafute Kamishna wa Elimu.”
Gazeti hili lilimtafuta kamishna huyo
pamoja na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa, Naibu
Waziri wa Wizara hiyo, Philipo Mulugo bila mafanikio kwani simu zao zilikuwa
zikiita bila majibu.
Akifafanua zaidi kuhusu viwango vya
elimu, uzoefu na uwezo wa wakuu wa shule za sekondari mjumbe huyo alisema,
“Mkuu wa shule anatakiwa achaguliwe kwa vigezo maalumu na apewe muda wa miaka
mitano katika nafasi hiyo na kila baada ya miaka mitano apimwe utendaji wake
kabla ya kumuongezea kipindi kingine.”
Alisema kuwa bado malengo ya sera ya
kuwa na wakuu wa shule wenye kiwango cha shahada ya kwanza au zaidi
haujafanikiwa.
“Hivi sasa kuna shule za sekondari
4,528 wakati rekodi zinaonyesha jumla ya wakuu wa shule ni 3,238 hivyo kuwa na
tofauti ya shule 1,294. Wakuu wa shule wengi hawajaandaliwa katika fani ya
utawala na hawapati mafunzo yenye tija ya kujenga umahiri wakiwa kazini”
alisema na kuongeza;
“Baadhi yao kubaki wakiogelea na
kufanikiwa kwa juhudi zao wenyewe. Kukosekana kwa utaratibu wa upimaji kwa
wakuu wa shule za umma kumewafanya walimu hao kukosa motisha na hivyo
kutojitahidi katika kuifanya shule yake kuwa ya kwanza au ya mfano katika
elimu.”
Alisema kuwa utaratibu wa kuteua na
kutokuwapima wakuu wa shule umekuwepo kwa muda mrefu tangu wakati idadi ya
shule, wanafunzi na walimu ilipokuwa ndogo.
“Kwa hali ya sasa, kuna ongezeko la
idadi ya shule, walimu na wanafunzi hivyo mkuu wa shule hawezi kuchaguliwa na
kuachwa bila kujengewa umahiri na akategemewa kufaulu katika kazi yake”
alisema.
Alisema kuwa vigezo vya kumchagua
mkuu wa shule vitumike, wapimwe weledi wao kila mara na wapate motisha pale
wanapofanya vizuri na kuleta maendeleo katika shule zao.
Alisema kuwa utaratibu wa kupata
wakuu wa shule katika shule za binafsi na tofauti na shule za umma, kusisitiza
kuwa sasa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) inatakiwa kuandaa na
kutekeleza utaratibu wa kupima utendaji wa wakuu wa shule na taarifa za
utendaji wao zijadiliwe katika vikao husika vya Halmashauri.
“Shule za Serikali za sekondari
zinapata wakuu wa shule kutokana na mfumo wa uteuzi. Shule nyingi za binafsi
hasa zile zinazofanya vizuri katika masomo na mitihani zina mifumo endelevu ya
kumpata mwalimu mkuu,” alisema na kuongeza:
“Baadhi ya shule za binafsi pia bado
hazina uwezo wa kupata Wakuu wa Shule kwa mfumo wa aina hii kwa sababu ya uwezo
mdogo wa kulipa mishahara kwa Wakuu wa Shule wenye sifa za juu na wanaoleta
matokeo yanayotarajiwa na mwajiri.”
Alisema kwa kiasi kikubwa sekta
binafsi imekuwa ikiitegemea sekta ya umma katika kupata Wakuu wa Shule walio
mahiri.
Alifafanua kwamba hali hiyo inatokana
na shule binafsi kulipa mishahara mikubwa kuliko ya Serikali na hivyo walimu wa
Serikali kuhamia huko kwa sababu ya tofauti katika masilahi.
Alisema kutokana na mazingira
kubadilika, ualimu mkuu sasa ni fani na siyo cheo tu, kwamba hauna kipindi
maalumu na hivyo mtu anaweza kuwa mwalimu mkuu kwa muda wake wote wa ajira.
“Mfumo wa aina hii hautoi fursa ya
ubunifu katika maendeleo ya shule. Shule nyingi za binafsi zinaendeshwa kwa
misingi ya mkataba wakati za serikali zina mfumo wa ajira ya umma wa kudumu.
Mifumo hii ni tofauti na inahitaji mifumo ya uwajibikaji tofauti” alisema
Alisema walimu katika sekta ya umma
ni wengi na hivyo huhitaji umahiri mkubwa katika kuwasimamia, kuwaendeleza na
kushughulikia masilahi yao kuliko kwenye sekta binafsi.
Chanzo:
mwananchi
No comments:
Post a Comment