Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi
na Bodi ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), zitawapa mikopo
wanafunzi 1,107 kutoka katika bajeti zao, baada ya wanafunzi hao kulalamika
kukosa mikopo.
Bodi kuanzia leo, itawaita wanafunzi
hao wanaochukua masomo ya vipaumbele yakiwamo ya Hisabati na Sayansi, ili
kujaza fomu upya.
Hata hivyo kuna wanafunzi wengine
waliokosa mikopo kutokana na kushindwa kujaza fomu za kuomba, lakini masomo yao
si ya kipaumbele na hivyo kuachwa katika uamuzi huo.
Takriban wiki mbili zilizopita, zaidi
ya wanafunzi 100 waliochaguliwa kujiunga katika vyuo vikuu mbalimbali nchini
kwa mwaka huu, waliandamana kwenda Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, kwa
lengo la kukutana na waziri mwenye dhamana na wizara hiyo, Dk Shukuru Kawambwa,
baada ya kukosa mikopo.
Wanafunzi hao walisema wamenyimwa
mikopo bila kupewa maelezo ya msingi licha ya kuilalamikia bodi ya mikopo.
Uamuzi huo wa jana, umekuja baada ya
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Jamii, kuzibana wizara na bodi, ikitaka
kujua kilichosababisha wanafunzi hao kukosa mikopo.
Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya
Ufundi, Philipo Mulugo, alisema jana kuwa baada ya kutafakari suala hilo,
uamuzi umefikiwa kuwa wanafunzi hao waitwe kujaza tena fomu za kuomba mikopo.
" Kilichoamuliwa ni kwamba
wizara na bodi zitatakiwa kutafuta fedha kwenye matumizi mengine, ili kuwapa
mikopo wanafunzi hawa," alisema.
Naibu Waziri huyo alisema, "Bodi
itatakiwa kutafuta fedha hizi kutoka kwenye matumizi mengine (OC), itabidi
wajinyime wasisafiri na kuachana na matumizi yasiyo ya lazima. Pia watumie
fedha za marejesho ya mikopo kugharimia wanafunzi hawa," alisema Mulugo.
Wanafunzi watakaofaidika na idadi yao
kwenye mabano ni wale wanaochukua masomo ya ualimu wa hisabati (20), ualimu
sayansi (164), udaktari tiba (111) na uhandisi umwagiliaji (7).
Wengine ni ualimu (617), sayansi kilimo
(20), uhandisi (70) na sayansi ya jamii (98).
Mulugo alisema jumla ya Sh3.1 bilioni
zinahitajika kuwalipia wanafunzi hao na kwamba bodi itatoa Sh 2 bilioni na
wizara yake itatoa Sh1.1 bilioni.
Alisema kiasi hicho cha fedha
kitakuwa kwa ajili ya chakula na malazi, vitabu viandishi na mafunzo kwa
vitendo na mahitaji maalumu ya vitivo.
Mulugo alisema fedha kwa ajili ya ada
za wanafunzi hao, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa
Sifuni Mchome, atawaandikia wakuu wa vyuo wanakokwenda kuomba kuwa Serikali
itawalipa kwenye bajeti ya mwakani katika bajeti ya 2014/15.
Chanzo: Mjengwablog
No comments:
Post a Comment