PICHA HII NI YA MAKTABA YA Blog
Dar es Salaam. Utafiti mpya umebaini
kuwa, Watanzania wanaongoza katika Afrika kwa kuwa na hofu ya kutendewa matukio
ya kihalifu katika nyumba zao kutokana na kupungua kwa usalama hapa nchini.
Hayo yalibainika kwenye majibu ya
utafiti uliotolewa jijini Dar es Salaam jana na Taasisi ya Utafiti kuhusu
Kuondoa Umaskini (Repoa), ambao unaonyesha kuwa asilimia 40 ya wananchi 2,400
waliohojiwa wana hofu ya kufanyiwa uhalifu na kuifanya Tanzania kuwa kinara
kati ya nchi 34 zilizofanyiwa utafiti huo.
Nchi nyingine zilizopo katika tano
bora ni; Afrika Kusini asilimia 38, Cameroon (37), Liberia (35) na Swaziland
asilimia 34.
Ripoti hiyo iliyoandaliwa kati ya Mei
hadi Juni, 2012, kwa kushirikiana na asasi ya Afrobarometer ililenga kuchunguza
hali ya uhalifu nchini na utayari wa wananchi kutoa taarifa za kihalifu kwa
polisi.
Akiwasilisha ripoti hiyo, Mtafiti
Msaidizi wa Repoa, Rose Aiko alisema kuwa vitendo vya watu kujeruhiwa kutokana
na uhalifu vimeongezeka nchini na idadi ya watu walzojeruhiwa imeongezeka
kutoka asilimia 10 mwaka 2003 hadi asilimia 44 mwaka 2012.
“Utafiti unaonyesha kuwa matukio ya
mtu mmoja mmoja kupigwa na kujeruhiwa yameongezeka, huku wizi katika nyumba nao
umeongezeka kutoka asilimia 22 mwaka 2005 hadi asilimia 36 mwaka 2012,” alisema
Aiko.
Akifafanua namna ambavyo watu wana
hofu ya kuibiwa kwenye nyumba zao, Aiko alisema kuwa vitendo vya kihalifu
viliongezeka kuanzia mwaka 2008 na mwaka 2003 kulikuwa na matukio mengi kwa
asilimia 48, lakini mwaka 2005 yalipungua hadi kufikia asilimia 34.
Hata hivyo, vitendo hivyo
viliongezeka tena na kufikia asilimia 43 mwaka 2012.
Pia utafiti huo umebainisha kuwa
ikilinganishwa na nchi nyingine za Afrika Mashariki, Tanzania ina asilimia 32
ya watu waliowahi kuibiwa nyumbani, huku ikiwa na asilimia 26 ya watu hao
katika Afrika.
Imebainika kuwa, asilimia 42 ya watu
waliofanyiwa vitendo vya kihalifu kati ya mwaka 2011 na 2012, ndiyo waliotoa
taarifa polisi huku ikielezwa kwamba wanaume ndiyo wanaoongoza kwa kutoa
taarifa hizo polisi.
“Utafiti unaonyesha kuwa wanawake ni
waoga zaidi wa matukio ya kihalifu ingawa imebainika kuwa sio wengi wanaokumbwa
na matukio hayo. Hata hivyo, imebainika kuwa wengi wapo tayari kuripoti polisi
taarifa za kuibiwa kuliko kupigwa,” ilisema sehemu ya ripoti hiyo.
Mtafiti Mwandamizi wa Repoa, Dk Abel
Kinyondo alisema kuwa asilimia 18 ya waliohojiwa walisema hawakupeleka taarifa
za uhalifu polisi kwasababu vituo vipo mbali, asilimia 15 walisema polisi wana
tabia ya kutokusilikiza shida zao, asilimia 14 walisema polisi wangetaka rushwa
huku asilimia 12 walisema walitoa taarifa kwa viongozi wengine walio karibu
yao.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment