Serikali ya Tanzania imesema
inatafakari ushiriki wake ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na inaweza
kujitoa ndani ya Jumuiya hiyo iwapo itaendelea kutengwa katika baadhi ya vikao.
Aidha imesema Tanzania haitambui
vikao vinavyofanywa na nchi tatu zilizopo ndani ya Jumuiya hiyo ambazo zimekuwa
zikizitenga Tanzania na Burundi.
Waziri anayehusika na masuala ya
Afrika Mashariki wa Tanzania Samwel Sitta ameliambia Bunge la Tanzania kuwa
makubaliano ya vikao hivyo vinavyofanywa na nchi za Kenya, Rwanda na Uganda
yatatekelezwa na nchi hizo zinazofanya vikao hivyo kwa sababu vinafanyika nje
ya utaratibu wa mkataba wa jumuiya hiyo.
Katika mikutano iliyofanyika hivi
karibuni Tanzania na Burundi hazikualikwa kwenye vikao hivyo.
Kwa mujibu wa Waziri Sitta mikutano
ya wakuu wa nchi za Rwanda, Kenya na Uganda ambayo ilianza kwa kuitenga
Tanzania ilifanyika Entebbe nchini Uganda mwezi Juni mwaka huu na kufuatiwa na
mkutano wa pili uliofanyika Agosti mwaka huu huko Mombasa nchini Kenya ambapo
nchi hizo tatu bila kuishirikisha Tanzania walizungumzia uanzishaji wa himaya
moja ya forodha.
Mambo mengine waliyozungumza wakuu
hao ilikuwa uanzishaji wa visa moja ya utalii kwa nchi zao na matumizi ya
vitambulisho vya uraia ambavyo vitatumika kama hati za kusafiria miongoni mwa
nchi hizo.
Aidha Waziri Sitta amesema ndani ya
mikutano hiyo pia walizungumzia kuanzisha mchakato wa kuanzisha shirikisho la
nchi hizo.
Tayari Tanzania imeanza mazungumzo na
nchi za Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo kuangalia ni kwa namna gani
zitaanzisha ushirikiano nje ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kama zinavyofanya
nchi za Rwanda, Uganda na Kenya.
Tanzania imesema itatoa msimamo wake
wiki hii kuhusu mkutano wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki
(EAC) ngazi ya marais, uliotarajiwa kufanyika jana kujadili masuala yanayohusu
maslahi ya nchi zilizoko katika ukanda huo bila kushirikishwa.
Waziri wa Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Samuel Sitta, aliliambia NIPASHE mjini hapa jana kuwa mkutano huo
ulitarajiwa kufanyika nchini Rwanda jana na kwamba ungehusisha marais wa nchi
za Rwanda, Paul Kagame; Rais wa Uganda, Yoweri Museveni; Rais wa Kenya, Uhuru
Kenyatta na Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza.
Alisema hayo alipokuwa akijibu swali
la NIPASHE lililotaka kauli ya serikali kuhusu uamuzi wa nchi hizo kuendeleza
tabia yao ya kuitenga Tanzania katika mikutano yao.
"Mkutano wa Rwanda unafanyika
leo ngazi ya marais. Tunasubiri kupata maazimio. Tanzania itatoa msimamo wiki
hii," alisema Waziri Sitta bila kutaka kuingia kwa undani kuhusiana na
suala hilo.
Mkutano huo ni wa tatu kufanyika bila
kuishirikisha Tanzania. Mara mbili mfululizo, marais wa nchi hizo walikutana na
kujadili mchakato wa kuanzisha miradi mbalimbali ya maendeleo, huku wakiitenga
Tanzania.
Marais Kenyata, Museveni na Kagame
alikutana mara zote hizo bila kumualika Rais Jakaya Kikwete.Kwenye vikao viwili
vilivyofanyika nchini Uganda na Kenya, viongozi hao walikubaliana kutekeleza
kwa haraka miradi ya ujenzi wa reli itakayounganisha nchi hizo na bomba la
mafuta litakalojengwa kuanzia Sudan Kusini hadi Mombasa na lingine kutoka Kenya
hadi Rwanda.
Pia nchi hizo zilitangaza kuanzia
Januari Mosi, raia wao watembeleane bila kuwa na hati za kusafiria, pia kuwa na
viza moja kwa watalii.
Mkutano wa Kenya ulioambatana na
ufunguzi wa gati katika bandari ya Mombasa, nchi za Burundi na Sudani Kusini
zilialikwa na kuwakilishwa na mawaziri wao waandamizi, lakini Tanzania
haikualikwa.
Vile vile, vyombo vya habari
viliwakariri baadhi ya mawaziri wa nchi hizo waliopewa jukumu la kusimamia
makubaliano hayo, wakiyaeleza kuwa ni ya jumuiya nzima na endapo Tanzania
ikipenda kuingia itakaribishwa. Kutokana na hali hiyo, Serikali ya Tanzania
ilionyesha wasiwasi wake juu ya mwenendo wa nchi hizo.
Ilipinga dalili zinazoonekana kwa
nchi za Kenya, Uganda na Rwanda kutumia jina la EAC kuomba fedha au kugharimia
miradi inayopaswa kuwa ya jumuiya.
Kauli hiyo ilitolewa na Naibu Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Abdullah Juma Saadalla.
Kauli hiyo ilitolewa na Naibu Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Abdullah Juma Saadalla.
Alisema malalamiko hayo
yalishawasilishwa pia katika kikao cha Baraza la Mawaziri wa EAC,
kilichofanyika jijini Arusha.
Dk. Saadalla alisema serikali
imemtaka Katibu Mkuu wa EAC, Dk. Richard Sezibera, kutoa maelezo juu ya gharama
ya miradi kadhaa inayoaminika kuwa sehemu ya jumuiya hiyo. Pia alisema hatua
zilizochukuliwa na nchi hizo kwa kukubali kuanzisha utaratibu wa matumizi ya
viza moja na vitambulisho vya pamoja, ni mfano wa ubabe usiokidhi matakwa ya
kidemokrasia.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Kimataifa, Bernard Membe, alisema hivi karibuni kuwa Tanzania ikibaini
kuwapo haja ya kujitoa EAC itafuata utaratibu kwa kulifikisha suala hilo
bungeni ili wabunge waliamue.
Chanzo: BBCSwahili/Nipashe
No comments:
Post a Comment