Thursday, October 24, 2013

Mazito yafichuka operesheni ya kimbunga nchini


Naibu Kamishna wa Polisi nchini na msimamizi wa operesheni kimbunga, Kamanda Simon Sirro akieleza jambo hivi karibuni. Picha ya maktaba.
Na Julieth Kulangwa, Mwananchi
Hivi karibuni Serikali ilianzisha operesheni maalumu iliyopewa jina la ‘Operesheni Kimbunga’ kwa lengo la kuwaondoa nchini watu wote ambao hawana uraia au haki ya kisheria kuishi nchini.

Baadhi ya mambo mazito yaliyoibuliwa na operesheni hiyo ni kubainika kwa wahamiaji haramu ambao huja nchini kwa lengo la kufanya ujangili. Aidha wengine huja maalumu kwa lengo la kufanya ujambazi.

Kama hiyo haitoshi imebainika kwamba wapo ambao wanakuja nchini kwa ajili ya kuuza silaha mbalimbali zikiwemo bastola na bunduki za aina mbalimbali zikiwamo Smg kutoka Burundi nan chi zingine. Wapo pia ambao huingia nchini kwa lengo la kulisha mifugo yao, na uthibitisho wa hili ni kwamba wapo ng’ombe kadhaa na mifugo mingine ambayo imekamatwan nchini ikiletwa kwa ajili ya kulishwa.

Operesheni hii ilikuwa na awamu mbili; ya kwanza ilianzisha Septemba sita hadi 20 mwaka huu na nyingine ya pili ni iliyoendelea ambayo ilianza Septemba 21, mwaka huu.
Kwa mujibu wa taarifa za Wizara ya Mambo ya Ndani hivi karibuni, wahamiaji haramu 425 wamekamatwa wakiwamo wanaowahifadhi.

Ingawa baadhi ya watu wanailalamikia operesheni hii wakisema baadhi ya maofisa wanatumia mwanya huo kuwanyanyasa kwa kuwaondoa nchini watu wenye chuki nao, Serikali inasema haina ushahidi juu ya hilo na kwamba kama yuko mwenye kufanya hivyo atachukuliwa hatua kali.

Kiongozi wa Timu ya Habari na Mawasiliano ya Operesheni Kimbunga, Zamaradi Kawawa amesema opereshani hiyo haijaundwa kwa lengo la kumuonea yeyote wala kuwaondoa watu wa taifa fulani, bali kujua nani anaishi kwa haki na nani haishi kwa kufuata haki.

Anasema mpaka kufikia Septemba 20, 2013, wamefanikiwa kuwakamata watuhumiwa 9,283 toka nchi za Rwanda, Burundi, Uganda, Somalia, DRC Congo, Yemen na India, kwa madai ya kuishi nchini isivyo halali.

Kwanini kuna operesheni hii?
Zamaradi anasema kilichomsukuma Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete kuanzisha operesheni hiyo ni kukithiri kwa matukio ya uhalifu hasa katika mikoa iliyopo pembezoni mwa nchi.

“Operesheni Kimbunga ilianzishwa kwa lengo la kukabiliana na vitendo vya uhalifu vilivyokithiri vikiwemo ujambazi wa kutumia silaha,ujangili, utekaji wa magari na mauaji ya kikatili pamoja na migogoro ya ardhi inayotokana na wafuagaji kutoka nchi jirani kuingiza mifugo yao kwa ajili ya malisho,” anasema Zamaradi.

Aidha amesema idadi kubwa ya wahamiaji haramu waliokamatwa ni kutoka Burundi (5,355) wakiafuatiwa na Rwanda (2,379), Uganda (939), DRC Congo (564), Somalia (44), Yemen (1) na India (1).
Aliongeza kuwa, takwimu zinaonyesha kuwa Mkoa wa Kigoma unaongoza kwa idadi kubwa ya wahamiaji haramu walioondoshwa nchini kwani 4,365 kati ya 9,283 walitoka mkoani humo.

“Karibu nusu ya wahamiaji haramu tuliowakamata walitokea mkoani Kigoma ukifuatiwa na Mkoa wa Geita ambao ulikuwa na wahamiaji haramu 583,” anabainisha Zamaradi.
Kati ya hao waliokamatwa, 3,238 waliondoshwa nchini kwa amri ya mahakama baada ya kupewa hati ya kufukuzwa nchini.

Aidha wananchi wengine 1,108 waliokuwa wanachunguzwa uraia wao waliachiwa baada ya watendaji kuthibitisha kuwa ni raia. Hata hivyo watu wengine 1,303 bado wanaendelea kuchunguzwa baada ya kuhisiwa kuwa wanaweza kuwa sio raia wa Tanzania.

Operesheni na madai ya rushwa
Anafafanua kuwa Operesheni Kimbunga inahusisha watendaji kutoka vyombo mbali mbali nchini vikiwamo; Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Idara ya Uhamiaji, Jeshi la Polisi, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na rushwa (TAKUKURU), Idara ya Usalama wa Taifa, Idara ya wanyamapori na taasisi nyingine za serikali.

“Mazingira ya kazi ya kuwakamata wahamiaji haramu na kuwahoji ili kuthibitisha uraia wao ni ya wazi hayawezi kuruhusu watendaji kupokea rushwa,” anasema na kuongeza.
Akashauri kuwa wananchi wanapaswa kufahamu kuwa iwapo kuna mtendaji wa operesheni hii ameomba na kupokea rushwa anakiuka sheria, ni vyema kama kuna mtu mwenye ushahidi wowote atoe taarifa kwenye ofisi za TAKUKURU zilizopo mikoani na Wilaya zote nchini.

Kuhusu kuhusishwa na ukikukwaji wa haki za binadamu Zamaradi amesema zoezi la hilo halilengi kuwanyanyasa wazee, watoto na wanawake wasio raia wa Tanzania.
“ Wakimbizi 36,000 kutoka nchi ya Rwanda waliingia nchini miaka ya 1959 hadi 1961 na walikuwa wakiishi katika Mkoa wa Kagera ambao walipewa uraia wa Tanzania kwa tajinisi mwaka 1983 isipokuwa watoto wao kwa kuwa wazazi wao hawakuwaombea uraia huo,” anafafanua.

Kuzaliwa Tanzania pekee hakumpi mtu haki ya kuwa raia moja kwa moja mpaka taratibu nyingine zifuatwe. Kuna watoto walizaliwa Tanzania na raia wa nchi za nje waliokuwa wanaishi nchini kabla ya kupatiwa uraia. Hao hawawezi kuwa raia moja kwa moja mpaka taratibu za kisheria zifuatwe.

Opereresheni yafichua kisiwa cha maficho ya uhamiaji haramu
Kamati ya ulinzi na usalama wilayani Mkinga imebaini kuwepo kwa kisiwa maalumu cha maficho ya wahamiaji haramu kutoka Somalia na Ethiopia ambao wametengeneza kiwanja maalumu ndani ya kisiwa hicho kwa ajili ya kufanya mazoezi.

Kisiwa hicho kinachojulikana kwa jina la Kirui chenye ukubwa wa hekta 600 kilichopo katika bahari ya Hindi kimeanza kuleta hofu kwa Kamati hiyo, askari waliokuwa na silaha mbali mbali walilazimika kuvamia kisiwa hicho kwa muda wa siku mbili na kufanikiwa kukamata wahamiaji haramu kutoka Ethiopia na Somalia wapatao 22 huku wengine wakidaiwa kutoroka ndani ya kichaka cha msitu huo wa miti aina ya mikoko.
Mahakama ya Wilaya ya Biharamulo imetoa hukumu ya kutaifisha Ng’ombe 103 mali ya Kalemela George kwa kosa la kuingiza mifugo hiyo katika hifadhi ya taifa ya Biharamulo.
Naibu Kamishna wa Polisi nchini, Kamanda Simon Sirro amewaambia waandishi wa Habari akiwa mjini Bukoba kuwa adhabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa kifungu namba 111 cha sheria ya wanayama pori na uhifadhi ya mwaka 2009.

Ng’ombe hao walikamatwa wakati Operesheni Kimbunga awamu ya Pili inaendelea katika mikoa ya Kagera, Kigoma na Geita ambapo jumla ya Ng’ombe 2,220 walikamatwa kwenye hifadhi ya Taifa kwa kipindi cha siku 10 tangu kuanza kwa awamu hii ya operesheni Septemba 21, 2013.

Kwa mujibu wa Kamanda Sirro, jumla ya watuhumiwa 88 wa unyang’anyi wa kutumia silaha pamoja na silaha 23 zikiwemo bomu la kurushwa kwa mkono moja, bunduki aina ya SMG 3, Pisto 2, magobole18 na risasi 484 miongoni mwake zipo risasi za SMG/SAR 471 na risasi za bastola 13, magazine za SMG 2 na sare za Jeshi la Burundi zimekamatwa katika kipindi cha siku 10 za operesheni Kimbunga Awamu ya Pili.

Akifafanua, Kamanda Sirro amesema watuhumiwa wawili wa ujambazi wa kutumia silaha wamekiri kufanya uchuuzi wa kununua silaha nchini Burundi hususan silaha za Kivita za SMG na kuziuza nchini kwa majambazi wa kutumia silaha.

Kamanda Sirro amesema mtu huyo bila kumtaja jina ameiambia polisi kuwa awali alikuwa mfanyabiashara ya mbuzi kutokea Tanzania kwenda Burundi ndipo alipogundua biashara yake hiyo hailipi na kuamua kujiingiza kwenye biashara ya kununua bBunduki aina ya SMG kwa Sh500,000 kutoka Burundi na kuja kuziuza Tanzania kwa zaidi ya Sh1milioni.

“Mtu huyu amekiri kuuza silaha nyingi nchini ambazo amekuwa akiziingiza kutoka nchini Burundi. Serikali itazungumza na Serikaliya Burundi kuona namna ya kudhibiti tatizo hilo nchini Burundi ambapo silaha za SMG zisizotakiwa kumilikiwa na raia isipokuwa Jeshi pekee zinapatikana kirahisi,” anasema Kamanda Sirro.
Chanzo: Mwananchi



No comments: