Mkuu wa ujasusi nchini Marekani,
James Clapper amesema kuwa nia ya baadhi ya viongozi wa kimataifa ndio moja ya
sababu kuu ya Marekani kufanya upelelezi.
Mkurugenzi wa shirika la kitaifa la
upelelezi, James Clapper, katika kutetea sababu yao ya kuwapeleleza viongozi wa
kimataifa , alisema kuwa juhudi kama hizo ni muhimu sana katika sera ya
upelelezi ya Marekani.
Lakini aliambia kamati ya waakilishi
wa bunge kuhusu upelelezi, kuwa Marekani haipelelezi mataifa ya kigeni kwa
undani na kiholela.
Bwana Clapper alikuwa anajibu tuhuma
dhidi ya Marekani kufuatia ripoti za udukuzi dhidi ya viongozi wa kimataifa na
ambao ni washirika wakuu wa taifa hilo.
"Nia ya viongozi ndio moja ya
sababu kuu ya kwa nini tunafanya upelelezi na kuutathmini,'' alisema Clapper
akiongeza kuwa washirika wa kimataifa a Marekani pia huchunguza maafisa wa
Marekani na mashirika mengine kama sehemu ya mipangilio ya serikali.
Alisema kuvuja kwa taarifa kuhusu
shughuli za upelelezi wa Marekani dhidi ya mataifa mengine imeharibia nchi hiyo
sifa yake na kuwa alitarajia taarifa zaidi kutolewa.
Rais Obama anasema kuwa anataka
kubadili namna nchi hiyo inavyokusanya ujasusi wake.
Lakini alisema hakuna nchi nyengine
iliyo na uwezo wa kukusanya upelelezi kama Marekani na kuwa kulikuwa na makosa
yaliofanyika ambayo ni ya kibinadamu au yaliyotokana na hitilafu za kimitambo.
Mwandishi wa BBC Jonny Dymond mjini
Washington alisema kuwa ikiwa mtu yeyote alikuwa anatarajia kuombwa radhi na
Marekani basi ajue kuwa hilo haliwezi kufanyika.
Chanzo: BBCSwahili
No comments:
Post a Comment