Wananchi wa Madagascar wanapiga kura
hii leo katika uchaguzi wa kwanza kufanyika nchini humo tangu yalipofanyika
mapinduzi yaliyoungwa mkono na jeshi miaka minne iliyopita.
Wagombea 33 wanawania urais wa nchi
hiyo katika uchaguzi huo, ambao umeahirishwa mara tatu mwaka huu.
Wagombea wawili wanaopewa nafasi ya
kushinda, wanaahidi kujenga upya uchumi wa Madagascar baada ya miaka ya mgogoro
wa kisiasa na kiuchumi.
Kwa mujibu wa Benki ya Dunia, zaidi
ya asilimia 92% ya wananchi milioni 21 wa Madagascar wanaishi chini ya dola
mbili kwa siku.
Rais Andry Rajoelina alimng'oa
madarakani Marc Ravalomanana mwaka 2009, na kulitumbukiza taifa hilo katika
mgogoro mkubwa wa kisiasa na kusababisha nchi hiyo kutengwa na jumuiya ya
kimataifa na kunyimwa misaada kutoka nje.
Mvutano wa Kisiasa
Baada ya kupora madaraka, Bwana
Rajoelina alitangaza kuwa kungekuwa na katiba mpya na uchaguzi kufanyika ndani
ya miezi 24.
Mwezi Mei mwaka 2009 ilikubalika kuwa
marais wote wa zamani wangeruhusiwa kugombea katika uchaguzi. Hata hivyo hilo
halikufanyika mwaka 2009 au 2010.
Wagombea Urais waliondolewa kwenye kinyang'anyiro
Mwezi Januari mwaka huu Bwana
Rajoelina na Bwana Ravalomanana wote walikubali kutogombea katika uchaguzi huu,
ikiwa ni makubaliano na Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika,
SADC, chombo cha kikanda ambacho Madagascar ni moja ya nchi wanachama wake.
Awamu ya kwanza ya uchaguzi huu,
ulipangwa kufanyika Julai 2013 lakini ukasogezwa mbele hadi mwezi Agosti kwa
sababu mke wa Bwana Ravalomanana, Lalao - na baadaye Bwana Rajoelina mwenyewe
kuamua kugombea, hali iliyosababisha nchi wahisani kusitisha fedha kwa ajili ya
uchaguzi huo.
Bwana Rajoelina na Lalao Ravalomanana
walizuiwa kugombea na mahakama ya uchaguzi pia ilimwondoa katika orodha ya
wagombea, rais wa zamani Didier Ratsiraka baada ya wote watatu kukataa
kujiondoa.
Chanzo: BBCSwahili
No comments:
Post a Comment