Wednesday, October 23, 2013

Katiba kicheko vyama vyote



Viongozi wa vyama vya siasa,(kushoto)Isaack Cheyo(UDP), Nancy Mrikaria(TLP), Fahmi Nassoro Dovutwa (UPDP), James Mbatia NCCR-Mageuzi, Profesa Ibrahim Lipumba(CUF), Philip Mangula(CCM) na Dk Willibrod Slaa(Chadema)wakiwa wameshikana mikono baada ya kikao cha pamoja jijini Dar es Salaam jana.Picha na Fidelis Felix 
Na Waandishi Wetu, Mwananchi
Dar es Salaam. Serikali inatarajia kuandaa hati ya dharura ili kuwezesha kufanyika kwa maboresho ya Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Mabadiliko ya Katiba ambayo yatajadiliwa upya katika Mkutano wa Bunge unaoanza Oktoba 29 mjini Dodoma.

Tayari vyama vya upinzani na chama tawala vimekubaliana taratibu muhimu za kufuata ili maboresho hayo yaweze kupita ndani ya Bunge. Muswada huo haukuwa umepangwa kujadiliwa katika mkutano ujao wa Bunge ndio maana itabidi iombwe hati hiyo ya dharura. Hatua hiyo ni ushindi kwa vyama vitatu vya upinzani vya Chadema, CUF na NCCR- Mageuzi, ambavyo vilipinga muswada huo wakati wa mkutano uliopita wa Bunge Septemba, mwaka huu.

Muswada wa sheria hiyo uliopitishwa Septemba na Bunge ulisusiwa na wabunge wa vyama hivyo wa upinzani kwa maelezo kuwa una kasoro kwenye baadhi ya vipengele.
Hata hivyo, wabunge wa CCM waliamua kuendelea na mjadala na kupitisha muswada huo kitendo ambacho kilisababisha mvutano mkubwa uliomfanya Rais Jakaya Kikwete kukutana na viongozi wa vyama vya siasa vyenye wabunge kumaliza tofauti zao.

Mbatia asoma tamko la vyama
Akisoma tamko la vyama vya siasa mbele ya waandishi wa habari jana, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia alisema hatua ya Serikali itakuja baada ya vyama vya siasa kufikia mwafaka wa vipengele vinavyotakiwa kufanyiwa marekebisho kwenye muswada huo. Mbatia alisema kuwa tayari kazi hiyo imefanyika na mapendekezo yao yameshapelekwa serikalini ingawa hakutaka kuingia kwa undani walichopendekeza katika marekebisho hayo.

Vyama vilivyokutana ni pamoja na CCM, Chadema, CUF, NCCR -Mageuzi, TLP. Pia vyama vya UDP na UPDP vilishiriki kwa niaba ya vyama visivyo na wabunge.
Mbatia alisema hatua inayofuata ni vyama kuunda kamati yao na Serikali kuunda yake ili kukubaliana kwa pamoja maeneo muhimu ya marekebisho.
Alisema lengo la hatua hiyo ni kuufanya mchakato wa Katiba kuwa shirikishi baada ya kamati hizo kumaliza kazi yake.

“Baada ya hapo, Serikali itaandaa hati ya dharura ili marekebisho yapelekwe haraka katika Mkutano wa Bunge unaoanza Oktoba 29, “ aliongeza Mbatia.
Mbatia alisema wanataka kabla ya Bunge la Katiba halijaanza basi sheria husika ifanyiwe marekebisho. “Tunawaomba Watanzania hasa wabunge waunge mkono juhudi hizi za vyama na Serikali ili kuhakikisha mchakato wa Katiba Mpya unakuwa shirikishi. Wabunge waridhie marekebisho haya na kuyapitisha,” alisema mbunge huyo wa kuteuliwa na Rais.

JK awapa goli wapinzani
CCM, ambayo wabunge wake walipitisha muswada kwa kauli moja, iliweka kando tofauti zake za kiitikadi na kimtizamo na kuungana na Chadema, CUF, NCCR- Mageuzi na vyama vingine vya upinzani.

Kitendo hicho cha CCM kilikuja baada ya Rais Kikwete kukutana na viongozi wa vyama vya siasa vyenye wabunge na vile visivyokuwa na wabunge, wiki iliyopita na kuvitaka vyama hivyo kukaa pamoja na kutoa mapendekezo ili yafanyiwe kazi na Serikali.
Kitendo hicho ni sawa na ushindi wa vyama vya upinzani kwani pamoja na kuwa wabunge wachache tofauti na CCM bado Rais Kikwete aliamua kusikiliza hoja zao.

CCM na Chadema damu damu
Katika hatua ya kuashiria kuwa vyama hivyo viko bega kwa bega, Makamu Mwenyekiti wa CCM, Phillip Mangula na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa walishikana mikono pamoja na viongozi wengine watano wa vyama vya siasa na kutoa tamko la pamoja kuhusu kuboresha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.

Tukio hilo la aina yake lilifanyika jana na kuongozwa na Mbatia, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia Tanzania ambacho kilipewa jukumu na Rais kuratibu ukusanyaji wa maoni ya maboresho ya muswada huo.
Mangula alipoulizwa kama wabunge wa CCM watakuwa tayari kupitisha maboresho ya sheria hiyo itakaporejeshwa tena bungeni alisema kwa kifupi; “Siwezi kuwasemea wabunge wa CCM.”

Alipobanwa zaidi kuhusu ushiriki wa CCM kwenye umoja wa vyama hivyo. Alisema: “CCM haijawahi kuandaa rasimu yake ya Katiba, ila nachojua ni kwamba kila chama kilipewa nafasi na Tume ya Mabadiliko ya Katiba kutoa maoni yake na CCM ni miongoni mwa vyama hivyo. Katiba Mpya ni kitu kizuri kwa taifa letu.”

Serikali yakubali ombi la tume
Serikali imekubali ombi la Tume ya Mabadiliko ya Katiba la kuongezewa muda wa mwezi mmoja kutokana na ugumu wa kazi ya uchambuzi wa maoni yaliyotolewa na wananchi na asasi mbalimbali.

Habari zilizopatikana kutoka vyanzo vya habari ndani ya Serikali na kuthibitishwa na Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe zilisema kuwa awali kabla ya kuomba muda huo, tume hiyo ilikutana na Rais Kikwete ili kuomba kuongezewa muda.

Maana yake ni kuwa Tume hiyo iliyoanza kazi Mei Mosi, mwaka jana ilitakiwa kukamilisha kazi yake Novemba Mosi, mwaka huu hivyo sasa kazi yake itakamilika Desemba. Akizungumza na gazeti hili ofisini kwake jana, Chikawe alisema, “ Kwa nini wakataliwe kama wanaona muda hauwatoshi.” 

Kwa mujibu wa Waziri Chikawe, muda waliomba unakubalika kisheria na kwamba wanaweza kuongezewa hadi miezi miwili.
Alipoulizwa kama haoni muda huo utasababisha kuchelewesha mchakato mzima wa Katiba, Waziri Chikawe alisema, haoni kama kuongezwa kwa muda huo kutaathiri chochote. “Nataka kuwahakikishia Watanzania hakuna haja ya kuwa na wasiwasi mchakato utaendelea kama kawaida kitakachoongezeka ni mwezi mmoja hivyo badala ya rasimu ya pili kukabidhiwa kwa Rais Novemba sasa itaenda mpaka Desemba,”alisema Waziri Chikawe.
Imeandikwa na Tausi Mbowe, Fidelis Butahe na Editha Majura.



No comments: