Mwenyekiti
wa UVCCM, Sadifa Hamisi Juma
Dodoma na Zanzibar. Baraza Kuu la Umoja wa Vijana wa
Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) linakutana leo jini Dodoma huku hatma ya Mwenyekiti
wa umoja huo, Sadifa Hamisi Juma ikiwa mashakani.
Mkutano huo wa baraza ulitanguliwa na
kikao cha Kamati ya Utekelezaji ya UVCCM kilichokaa jana jioni mjini Dodoma
kwenye Ukumbi wa White House ambako ni makao makuu ya CCM.
Sadifa, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo
la Donge, analalamikiwa kutokana na matatizo mbalimbali ya kiutawala, matumizi
mabaya ya fedha na usimamizi mbovu wa mali za chama hicho.
Alipoulizwa juu ya kuwapo kwa vuguvugu
la kumng’oa, Sadifa alijibu kwa kifupi tu; “Asante Nashukuru.” “Ninaambiwa
nimekuwa mtu wa kutukana watu, nimemtukana nani? Asante Nashukuru.,”aliongeza
Sadifa hata pale mwandishi alipomuuliza kwa zaidi ya mara tatu aliishia kutoa
jibu: “Asante nashukuru.”
Naye Katibu Mkuu wa UVCCM, Sixtus
Mapunda, alipoulizwa na Mwananchi jana, alisema kuwa hana taarifa za kuwapo
mpango wa kumng’oa mwenyekiti wake kama inavyoelezwa.
“Sikiliza, mimi ndiye Mtendaji Mkuu
wa UVCCM, ajenda za mkutano, sisi kama sekretarieti tumeshaziandaa na hakuna
agenda kama hiyo. Umoja huu unaendeshwa kwa kanuni na taratibu,”alisema
Mapunda.
Mapunda aliyechukua mikoba hiyo
Agosti mwaka huu, alipoulizwa kuhusu mkutano huo kugharamiwa na CCM makao makuu
badala ya Jumuiya yenyewe, alikanusha taarifa zilizozagaa akisema: “Mimi ndiye
niliyeitisha mkutano huu, sasa chama kinatoka wapi?”
Mjumbe aanika madudu ya UVCCM
Mwenyekiti wa UVCCM wa Mkoa wa
Ruvuma, Alex Nchimbi alifafanua hakuna njama za kumtoa ila mambo anayotakiwa
kurekebisha ndio yanaweza kumtoa.
Nchimbi alisema kuwa UVCCM
inakabiliwa na tatizo la matumizi mabaya ya fedha na kibaya zaidi hesabu za
chama hicho hazijakaguliwa kwa muda mrefu.
Alisema jumuiiya hiyo hupata kiasi
cha Sh80 milioni kutokana na miradi mbalimbali kama jengo lililoko makao makuu
ya UVCCM, lakini fedha hizo zinafujwa.
“Ila utashangaa kaka yaani zile fedha
zinavyofujwa. Hadi kwa mwezi jumuiya inabakiwa na Sh8 milioni au wakati
mwingine hadi Sh6milioni,” aliongeza Nchimbi.
Nchimbi aliongeza tatizo jingine ni
uteuzi wa viongozi bila kufuata taratibu.
Alisema kuwa Sadifa aliteua
sekretarieti kabla ya uteuzi wa wajumbe wa Kamati ya Utekelezaji ambapo ni
kinyume na utaratibu.
Alitaja viongozi hao kuwa ni Mkuu wa
Idara ya Uchumi na Fedha, Omar Suleimani, Mkuu wa Chipukizi na Uhamasishaji,
Omar Justus na Tumaini Mwakasege, ambaye aliteuliwa kuwa Mkuu wa Oganaizesheni.
“Umoja wetu una pikipiki 10, lakini
kapeleka pikipiki mbili Morogoro na nane kazipeleka Zanzibar kwenye jimbo lake.
Ukichunguza uandikishaji wake utagundua bado zinamilikiwa na UVCCM”, alisema
Nchimbi.
Nchimbi pia alimtuhumu Sadifa kwa
kuanzisha nafasi za makatibu wasaidizi wa mikoa bila ya baraka za Baraza Kuu.
“Hivi nani angewalipa watu hawa.
Lazima tujiulize UVCCM ina fedha gani za kuwalipa makatibu wa mikoa na
wasaidizi?,” alisema Nchimbi
Wanataka UVCCM izaliwe upya
Nchimbi alisema UVCCM wanakabiliwa na
changamoto ya kusafisha uoza ndani ya jumuiya na hasa kwa kuzingatia kuwa
Sadifa anatoka Zanzibar.
“Kwa hali ya kawaida, kama si
kulindwa na wazee kwa hoja za kulinda Muungano na amani katika jumuiya na
kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa basi tusingekuwa naye,” alisema Nchimbi.
Nchimbi, hata hivyo, alionya kuwa
uongozi wa vijana uliopo usiporekebishwa hawawezi kumsaidia balozi wa nyumba 10
kushinda uchaguzi
Jaribio la pili kumtoa Sadifa
Mpango huo wa kumtimua Sadifa ni wa
pili ndani ya siku zisizozidi 60 baada ya awali kuibuka mvutano mkubwa ndani ya
jumuiya hiyo, kutokana na baadhi ya wajumbe wa Baraza Kuu la Umoja huo
kudhamiria kumng’oa madarakani mwenyekiti huyo.
Mgogoro huo ulisababisha kikao cha
Baraza Kuu kilichokuwa kikifanyika Zanzibar, ambacho mgeni rasmi alikuwa Makamu
wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Balozi Seif Ali
Iddi na baadhi ya wajumbe kumtaka Sadifa na Kamati yake ya Utekelezaji kutoka
nje ili wajadiliwe kwa kukiuka kanuni.
Aking’olewa Sadifa, itakuwa mara ya
pili kwa mwanachama wa Jumuiya hiyo kutoka Zanzibar kung’olewa baada ya Masauni
Yussuf Hamad kung’olewa mwaka 2010 kwa tuhuma za kughushi umri.
Chanzo:
Mwananchi
No comments:
Post a Comment