Marais wa Sudan na Sudan Kusini
wamekubaliana kubuni mikakati ya kusuluhisha maswala yote yanayotatiza uhusiano
wa pande hizo mbili.
Viongozi hao walikutana leo wakati wa
mkutano wa faragha katika mji mkuu wa Sudan Kusini, Juba.
Aidha vingozi wa kamati sita
wakiwemo, mawaziri kutoka nchi hizo mbili pia walikutana wakati wa mkutano hio
na kujadili maswala kuhusu nchi hizo mbili.
Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir
Mayardit alielezea furaha yake kwa kufikia makubaliano ya pande hizo mbili
akisema kuwa serikali yake itajitolea kuhakikisha kuwa makubaliano hayo
yatatekelezwa.
Kwa upande wake Rais Umar al-Bashir
alisema kuwa mkutano ulifanikiwa na kuongeza kuwa serikali yake itajitolea
kuhakikisha kuwa makubaliano waliyoafikia yanatekelezwa.
Marais hao walifanya mkutano wa
faragha muda mfupi baada ya Bashir kuwasili na wajumbe wake wa Sudan katika
Ikulu ya Rais mjini Juba.
Kwa mujibu wa shirika la habari la
SUNA, baadhi ya maswala yaliyojadiliwa kwenye mkutano huo ni mambo tete kuhusu
Abyei,usalama pamoja na kutekelezwa kwa makubaliano ya ushirikiano kati ya nchi
hizo mbili.
Mnamo siku ya Jumatatu, waziri wa
mambo ya nje wa Sudan Kusini Barnaba Marial Benjamin, aliambia kituo cha redio
cha Sudan CRN kuwa marais hao wawili watazungumzia mgogoro wa Abyei katika
kutaka kuboresha uhusiano kati ya nchi hizo mbili.
Kuhusu swala la kura ya maoni kuhusu
Abyei , waziri alisema kuwa Muungano wa Afrika hauruhusu uamuzi wa pande moja
kuhusu kura ya maoni.
Aliongeza kuwa Kura ya maoni lazima
iruhusiwe na nchi hizo mbili na kuidhinishwa na baraza la usalama la Umoja wa
Mataifa.
Aidha alisema kuwa sudan Kusini
inashurutishwa na makubaliano ya ushirikiano kati ya nchi hizo mbili na kwa
hivyo haiwezi kuunga mkono kura ya maoni inayoshinikizwa na upande mmoja.
Hata hivyo alisema anaelewa kwa nini
jamii ya Abyei iliamua kupiga kura ya maoni kujitenga na ni kwa sababu ya
masaibu waliyoyapitia.
Alisisitiza kuwa Muungano wa Afrika
na Sudan lazima ziisikilize jamii ya Abyei na kukubaliana kuhusu tarehe ya
kufanyika kwa kura ya maoni kuhusu kutaka kujitawala wenyewe.
Chanzo: BBC Swahili
No comments:
Post a Comment