na Happiness Mnale
SIKU chache baada ya kutokea kwa kifo
cha mwanajeshi wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Luteni Rajabu Mlima,
aliyekuwa katika operesheni ya kulinda amani Mashariki mwa Kongo (DRC),
serikali imesema haitatetereka wala kurudi nyuma kwa kurudisha majeshi yake
nchini.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana
wakati wa kuaga mwili wa marehemu Mlima katika viwanja vya jeshi Lugalo, Waziri
wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha, alisema serikali
itaendelea kutoa ushirikiano kwa wanajeshi waliobakia nchini humo ikiwa ni
sehemu ya utekelezaji wa kulinda amani ya wananchi wa Kongo.
“Kama serikali tunasikitika kwa kifo
cha mwanajeshi wetu, lakini hili halitufanyi kushindwa kuendelea kulinda raia
wa Kongo na bado tunaendelea kutoa hamasa kubwa kwa wanajeshi waliobaki
waendelee na majukumu yao kama kawaida.
“Kikubwa tutaendelea kutoa
ushirikiano kwa familia ya marehemu kwa kuhakikisha shughuli zote za mazishi
zinaenda sawa pamoja na kuwa nao karibu katika kipindi hiki kigumu cha
majonzi,” alisema Nahodha.
Awali akisoma salamu za rambirambi
kwa niaba ya Mkuu wa Majeshi Nchini (CDF), Davis Mwamunyange, Mnadhimu Mkuu wa
Jeshi la Ulinzi, Luteni Jenerali, Samuel Ndomba, alisema marehemu Mlima
alipigwa risasi Oktoba 27, saa 5:00 asubuhi, akiwa katika milima ya Cavana
iliyoko mashariki mwa Kongo na kufa papo hapo.
Chanzo;
Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment