• Adai
alitamani serikali tatu, awashangaa CCM kukwepa
na Josephat Isango na Shehe Semtawa
KADA mkongwe wa Chama Cha Mapinduzi
(CCM) ambaye ni muasisi wa kundi la wabunge waliokuwa wakishinikiza hoja ya
Serikali ya Tanganyika, maarufu kama G55, Njelu Kasaka, ameibuka na kuwashangaa
wabunge wa chama hicho kupinga hoja ya muundo wa serikali tatu wakati ni yao
tangu awali ya kudai mabadiliko ya muundo wa Muungano.
Kasaka aliongeza kuwa hata Baba wa
Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere, aliona umuhimu wa muundo huo wa serikali
tatu, isipokuwa alitoa tahadhari kuwa kwa aina ya uendeshaji wa serikali
uliokuwa unaendekezwa kwa kuogopana na kulindana Muungano usinge dumu.
Mwanasiasa huyo ambaye amewahi kuwa
mbunge wa Lupa, alitoa kauli hiyo jana katika mahojiano maalumu na gazeti hili
jijini Dar es Salaam, huku akiwaasa wabunge hasa wa CCM kuacha mzaha katika
suala la katiba, akisema ni muhimu na lisipoangaliwa kwa umakini linaweza
kuliingiza taifa katika machafuko.
“Wabunge wote watakapokuwa Dodoma
wajue wana dhamana kubwa sana, wasifanye mzaha na suala la katiba, ni suala
muhimu kwani katiba mbaya inaweza kuangamiza. Suala la kubadilishwa katiba
halifanyiki kama wanavyobadili sheria.”
“Wanapitisha leo, rais anasaini
anawarudishia wakafanye mabadiliko, si kitu rahisi. Wakumbuke kuwa wakiamua
vibaya wataangamiza taifa kwa muda mrefu na wakiamua vizuri watalisaidia
taifa,” alisema.
Kasaka alitumia muda mwingi kuelezea
historia ya kundi hilo (G55), akisema lilianzishwa baada ya manung’uniko ya
Wazanzibari kuwa wanaonewa na Serikali ya Muungano.
“Wazanzibari walisema kuwa Serikali
ya Tanganyika imejifanya kuwa ni ya muungano ili kuitawala Zanzibar bila ridhaa
ya Wazanzibari na kwamba ilizuia Serikali ya Zanzibar kufanya mambo yake.
“Serikai tatu ni wazo la CCM, kwani
wakati tunalianzisha vyama vya upinzani vilikuwa vingine havijasajiliwa na
vilivyokuwapo havikuwa na wabunge, vilikuwa makundi ya wanaharakati wakati huo,
waliunga mkono kutaka mabadiliko,” aliasa.
Kasaka aliongeza kuwa hali ya wakati
huo ilimuudhi kwani mtu wa Bara alikuwa akitaka kwenda Zanzibar inabidi awe na
hati ya kusafiria na kuchukuliwa kama mgeni wakati wanazungumzia nchi moja.
“Nilipeleka hoja bungeni, ikaungwa
mkono na Matheo Qares, Arcado Ntagazwa, Mussa Nkhangaa, William Mpiluka
(marehemu), Sebastian Kinyondo (marehemu) na Jenerali Ulimwengu. Kwa ujumla
niliungwa mkono na wabunge 55, ingawa baadaye wabunge karibu wote walituunga
mkono tukaambiwa halimo katika sera za CCM,” alisema.
Kwa mujibu wa mwanasiasa huyo,
serikali tatu au mabadiliko ya muundo wa Muungano kutoka wakati huo hadi sasa
hayaepukiki.
Kwamba, mtazamo wa Wazanzibari
wanasema wapo tayari kutofautiana katika mambo yote kisiasa au kiitikadi lakini
hoja ya Uzanzibari (identity ya nchi) haifi hadi utakapomwondoa Mzanzibari wa
mwisho.
“Kumbuka kuwa aina ya Watanzania wa
sasa si wale wa miaka 30 iliyopita, wakati huo walikuwa wanazaliwa, ila sasa
wao ndio wasomi na wasemaji katika mambo mengi.
“Nawatahadharisha wabunge waangalie
idadi ya Watanzania sasa si ile iliyokuwapo, mwamko wa sasa si ule wa miaka iliyopita.
Mwaka 1993 -1995 watu waliokuwa wanajitambulisha ni wapinzani walikuwa
wanazomewa, sasa wale wanaojitambulisha CCM ndio wanaozomewa, wakubali
mabadiliko, serikali tatu haziepukiki na hii ilikuwa hoja ya wabunge wa CCM,”
alisema.
Kisaka alisema wabunge wakubali
kufanya marekebisho ya sheria iliyorejeshwa na rais, kwani serikali haiwezi
kujitungia katiba, hivyo wabunge wote hasa wa CCM wakubali suala la serikali
tatu, wafanye marekebisho mazuri ili kuondoa uwezekano wa mgogoro mkubwa kati
ya Bara na Zanzibar.
Alimpongeza Rais Jakaya Kikwete kwa
kauli yake aliyoitoa mjini Dodoma hivi karibuni ya kukemea vitendo vya rushwa
ndani ya chama, akisema itawaathiri kwenye Uchaguzi Mkuu ujao ikiwa
hawatajirekebisha.
Alisema anakubaliana na Kikwete kwa
asilimia mia moja kwamba CCM isipoacha rushwa itaanguka, na isipoacha upendeleo
na kulazimisha wagombea wasiokubalika vilevile itakufa.
Kasaka alimtaka Rais Kikwete kuchukua
hatua, asiishie kusema. Kwamba, anaweza kutumia Taasisi ya Kuzuia na Kupambana
na Rushwa (TAKUKURU) kwa masuala ya kisheria na mengine ya kiutendaji yapo
chini ya uwezo wake.
“CCM watu hawachukuliani hatua,
Makamu Mwenyekiti (Bara), Philip Mangula, alilalamikia rushwa aliposhindwa
uenyekiti wa Mkoa wa Iringa, lakini aliishia kusema kuwa uongozi katika chama
unapatikana kama bidhaa gulioni, na alipochaguliwa kuwa makamu mwenyekiti wala
hajawahi kuchukua hatua,” alisema.
Kasaka aliongeza kuwa hadi Rais
Kikwete ameamua kujitoa kuyasemea hayo nje, ni kwa sababu ndani ya CCM watu si
wasikivu, wengine wana dharau.
“Ukiona mke na mume wanatukanana
hadharani ujue ndani wametukanana vya kutosha na imeshindikana, wameonyana
imeshindikana, ndiyo maana wanakuja hadharani kuja kukemeana mbele yetu,”
alisema.
Chanzo:
Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment