Hizi tuhuma kuwa natumiwa na Zitto nimekuwa nikizisikia,
lakini huo ni upofu, mimi si mtu wa kutumika nina elimu yangu nzuri ya shahada
ya kwanza ya utawala wa biashara, najua ninachokifanya ni kwa masilahi ya
chama. Samson Mwigamba
Na Mussa
Juma, Mwananchi
Arusha. Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa
Arusha, Samson Mwigamba, amepinga uamuzi wa kusimamishwa kwa maelezo kuwa
kikao kilichochukua uamuzi huo hakitambuliki kikatiba huku akikanusha tuhuma za
kutumiwa na Naibu Katibu Mkuu, Zitto Kabwe, kukisambaratisha chama hicho.
Akizungumza jana na gazeti hili,
Mwigamba alisema kikao ambacho kina mamlaka ya kumwajibisha ni Kamati Kuu baada
ya kupokea tuhuma na kumsikiliza.
“Baraza la uongozi la Kanda halina
mamlaka ya kunisimamisha uenyekiti, lakini kwa kuwa mimi bado ni mwanachama hai
wa Chadema na sitahama Chadema, nitakaa pembeni ili chama kifanye uchunguzi wa
tuhuma zangu nikiwa nje ya ofisi,” alisema Mwigamba.
Hata hivyo, alisema anakusudia
kufafanua chanzo cha mgogoro wake na baadhi ya viongozi leo, baada ya
kukabidhiwa kompyuta mpakato (laptop) na viongozi wa chama hicho ambao
waliichukua ili kuifanyia uchunguzi.
Akana kutumiwa na Zitto
Akizungumzia tuhuma za muda mrefu
kuwa, amekuwa akitumiwa na Zitto hasa kuelekea uchaguzi ndani ya chama
hicho, alisema wanaofikiri hivyo ni vipofu wa kisiasa.
“Hizi tuhuma kuwa natumiwa na Zitto
nimekuwa nikizisikia, lakini huo ni upofu, mimi si mtu wa kutumika nina elimu
yangu nzuri ya shahada ya kwanza ya utawala wa biashara, najua ninachokifanya
ni kwa masilahi ya chama,” alisema Mwigamba.
Alisema kama angekuwa mtu wa kutumiwa
sasa, angetumiwa na mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe ambaye ana uwezo
wa kifedha kuliko Zitto au Katibu Mkuu, Dk Willibrod Slaa ambaye atakuwa
mgombea wa urais wa chama hicho na ana uwezekano wa kushinda.
Alisema kabla ya tuhuma za sasa
kwamba anatumiwa na Zitto, aliwahi kutuhumiwa pia na Zitto kuwa anatuhumiwa na
Mbowe hasa kutokana na misimamo yake na kauli zake katika vikao na maeneo
mbalimbali, lakini baadaye ilithibitika kuwa alikuwa na hoja za msingi.
“Mimi ni mwanachama hai wa Chadema na
nimekuwa nikitoa maoni yangu si kama Mwenyekiti wa Chadema Mkoa. Nina uhuru wa
kutoa maoni katika kuhakikisha chama changu kinashika dola,” alisema Mwigamba.
Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya
Kaskazini, Mchungaji Israel Natse alitangaza juzi kusimamishwa Mwigamba hasa
kutokana na tuhuma za kukichafua chama hicho kwenye mitandao ya kijamii.
Kabla ya hatua hiyo, Mwigamba alipata
kipigo kutoka kwa vijana wa Chadema baada ya kutuhumiwa kurusha kwenye
mtandao wa Jamii Forum tuhuma za matumizi mabaya ya fedha ndani ya
chama hicho akiwa ndani ya kikao cha Baraza la viongozi Kanda ya Kaskazini.
Hata hivyo, wachunguzi wa mambo
wanaamini kuna uwezekano kuwa mgogoro katika chama hicho unatokana na vuguvugu
la uchaguzi uliosogezwa mbele hadi mwakani.
Kuna wasiwasi huenda yakajirudia ya
mwaka 2009 wakati Zitto alipojaribu kuwania nafasi ya Mwenyekiti dhidi ya Mbowe
na kuzua mvutano mkubwa ndani ya chama hicho.
Hata hivyo, Zitto aliweka bayana kuwa
hawezi kuzungumzia mambo hayo kwani hafahamu hata huo uchaguzi wa ndani
utafanyika lini.
Akizungumzia suala hilo, Katibu
Mwenezi wa Chadema, John Mnyika alifafanua kuwa kikao kilichomsimamisha
Mwigamba kilikuwa halali.
Mnyika alisema, hata hivyo, ikiwa
Mwigamba hajaridhishwa na hatua hiyo anapaswa kukata rufaa na siyo
kulalamika kwenye magazeti.
Alisema kuwa Mwigamba anapaswa kusoma
katiba ya chama hicho na kuelewa mambo ya chama yanamalizwa na kikao husika na
siyo kwenye vyombo vya habari.
“Kikao kile kinaweza kumsimamisha ila
kama hajaridhishwa na uamuzi ule basi aende kwenye ngazi inayofuata,” alisema
Mnyika.
Mnyika, hata hivyo, alisema kwa ngazi
ya taifa wanasubiri taarifa ya kikao kilichomsimamisha kwani walikuwa
hawajapokea na wala kutumiwa malalamiko yoyote na Mwigamba.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment