Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo
ya Ufundi Profesa Sifuni Mchome akifafanua kwa waandishi wa habari
(hawapo pichani) juu ya upangaji wa viwango vya alama, matumizi ya alama
endelevu ya mwanafunzi na ufaulu leo jijini Dar es Salaam, kulia ni
Kamishna wa Elimu Profesa Eustella Bhalasesa.
Picha zote na Eliphace Marwa
(MAELEZO)
UPANGAJI WA VIWANGO VYA ALAMA,
MATUMIZI YA ALAMA ENDELEVU YA MWANAFUNZI NA UFAULU
UTANGULIZI
Wizara imekusanya maoni ya Wadau wa Elimu
kuhusu Upangaji wa Viwango vya Alama (Grade Ranges) katika Mitihani ya Kuhitimu
Kidato cha Nne na cha Sita pamoja na Matumizi ya Alama za Tathmini Endelevu ya
Mwanafunzi (Continuous Assessment ama CA) kwa ajili ya kuamua kiwango cha
ufaulu wa mwanafunzi. Maoni ya wadau yamekusanywa kwa sababu kwa muda mrefu
sasa upangaji wa viwango vya alama vinavyotumika na utaratibu wake katika
mitihani ya kuhitimu Kidato cha Nne na Kidato cha Sita umekuwa haufanani pamoja
na kwamba mitihani hiyo yote ni ya elimu ya sekondari.
Pia mfumo masuala
mbalimbali ya mitihani katika elimu ya sekondari umekuwa na miundo tofauti
ikiwemo ule unaotumika shuleni na ule wa Baraza la Mitihani la Taifa. Kwa sasa
kuna miundo mikuu miwili katika mfumo huo.
Muundo wa Kwanza ni upangaji wa
viwango katika ngazi ya Shule ambapo Alama Mgando (Fixed Grade Ranges)
zifuatazo hutumika kupanga madaraja: A = 81 – 100; B = 61 – 80; C = 41 – 60; D
= 21 – 40 na F = 0 – 20. Muundo huu umetumika kwa muda mrefu na umezoeleka kwa
walimu na wanafunzi wa elimu ya sekondari kwa ujumla.
Muundo wa Pili ni wa viwango
vinavyotumiwa na Baraza la Mitihani la Taifa ambapo ambapo kabla ya mwaka 2012
muundo wa viwango nyumbufu (flexible grade ranges) ulitumika. Katika muundo huu
uwigo wa alama ulibadilika badilika kulingana na hali ya matokeo ilivyokuwa kwa
mwaka husika.
Lakini kuanzia mwaka 2012, Serikali iliamua kutumia mfumo wa
Upangaji wa Alama Mgando (Fixed Grade Range) kwa Kidato cha Nne na Kidato cha
Sita. Katika mtihani wa Kidato cha Nne mwaka 2012 Baraza lilitumia mfumo huu wa
alama mgando ambapo: A = 80 – 100, B = 65 – 79, C = 50 – 64, D = 35 – 49, F = 0
– 34. Kwa upande wa Kidato cha Sita Baraza lilitumia mfumo wa A = 80 – 100; B =
75 - 79; C = 65 – 74; D = 55 – 64; E = 45 – 54; S = 40 – 44 na F = 0 – 39. Mifumo
hii ya Baraza haikuwa inafahamika kwa wadau na hivyo kuwa sehemu ya malalamiko
katika sekta ya elimu na mafunzo.
Vilevile, Sera ya Elimu na Mafunzo ya
mwaka 1995 imeelekeza kwamba katika kuamua kiwango cha ufaulu wa mwanafunzi wa
elimu ya sekondari, Alama za CA zitachangia asilimia hamsini (50%) na Mtihani
wa mwisho utachangia asilimia hamsini (50%). Kwa upande wa Zanzibar, CA
zimekuwa zikiandaliwa kwa mfumo wa asilimia arobaini (40%) na mtihani wa mwisho
asilimia sitini (60%). Pamoja na kwamba Baraza halijawahi kuutumia mifumo hii
tangu ilipowekwa, kumekuwa na mitazamo, maoni na
mapendekezo tofauti katika
muundo na matumizi ya alama za CA. Kuna mawazo pia kwamba mfumo wa CA kuchangia
matokeo ya mwisho ya mwanafunzi pia utumike kwa watahiniwa wa kujitegemea
(private candidates). Kwa sasa matokeo ya mitihani ya watahiniwa hawa yamekuwa
yakitumia alama za mtihani wa mwisho tu na hivyo kutafsiriwa kama utaratibu
ambao unamwonea mwanafunzi ambaye anahamu ya kujiendeleza kielimu lakini
anakwama kwa sababu mfumo unaotumika siyo rafiki kwa mtahiniwa.
Kwa mantiki hii, Wizara imedhamiria
kufanya harmonization ya masuala ya alama katika mitihani ya Kidato cha Nne na
Kidato cha Sita ili kupata muundo mmoja na ulio wazi kwa wadau wote wa elimu ya
sekondari. Lakini pia serikali imedhamiria kuhakikisha tathmini za wanafunzi
katika ngazi mbalimbali zinakwenda sambamba na matarajio ya mitaala inayotumika
na ambayo inahuishwa mara kwa mara ili iendane na wakati na mahitaji ya elimu
katika ngazi mbalimbali.
VIWANGO NA UTARATIBU KUANZIA MWAKA
2013 KWA KIDATO CHA NNE NA
MWAKA 2014 KIDATO CHA SITA
Baada ya kufanya tathmini ya maoni
mbalimbali ya wadau, misingi ifuatayo ilizingatiwa katika maamuzi kuhusu
makundi ya alama na muachano wake:
a) Alama zitakazotumika zitakuwa A,
B, C, D, E na F. Muachano wa alama kati ya kundi moja hadi jingine utafanana,
isipokuwa tu pale ambapo itaonekana kuna sababu na hakuna athari za kuwa na
muachano tofauti na ule ambao umetumika katika makundi mengine.
b) Makundi ya alama hayatakuwa na
clusters isipokuwa pale ambapo itaonekana kufanya hivyo kunaleta tija katika
kupata picha ya wahitimu kwa ajili ya matumizi mbalimbali. Kwa mantiki hii
(i) makundi ya alama A, C, D, E na F
yabaki na cluster moja moja bali kundi la alama B litakuwa na clusters mbili.
Kundi la kwanza litakuwa la wale ambao wamepata alama kati ya 50 mpaka 59 na
litaitwa B na lingine litakuwa la wale ambao wamevuka uwigo wa 50 hadi 59 na
kuelekea uwigo wa 60 hadi 74 na hili litaitwa B+ (angalia jedwali hapo chini).
(ii) Pamoja na kuwa na muachano wa
alama 26 kama jedwali linavyoonesha hapo chini, alama A kwa miaka mingi imekuwa
ikianzia alama 75 hadi 100 na kwamba pamoja na uwigo huo bado wanaofaulu kwa
kiwango hicho ni wachache sana. Kwa mantiki hii, hakuna haja ya kubadilisha
uwigo ila juhudi ziendelee katika ufundishaji na ujifunzaji ili kiwango cha
ufaulu kiongezeke na kupata wanafunzi wengi zaidi wanaofaulu katika kundi hili.
(iii) Pia, pamoja na kuwa na muachano
wa alama 20 kama jedwali linavyoonesha hapo chini kwa miaka mingi, huko shuleni
mwanafunzi aliyepata alama 21 na hadi 30 alihesabiwa kuwa na ufaulu wa chini
kabisa au hafifu kwa kiwango cha alama D na ingawa ilikubalika ufaulu wa aina
hiyo kwa mazingira ya nchi yetu unaridhisha.
Alama F ilikuwa ni kwa wale
waliopata chini ya hapo. Hivyo, alama F itaendelea kuwepo na itaanzia alama 0
hadi 19 na E itaanzia alama 20 hadi 29 na D – 30 -39. Lengo la muundo huu ni
kuwa alama mbalimbali, isipokuwa kwa makundi machache, zianzie kwenye 0 yaani
0, 10, 20, 30, 40 na kuendelea badala ya kuanzia kwenye moja yaani 1, 11, 21,
31, 41 na kuendelea. Hii ni kwa ajili ya kuleta mtizamo unaofanana katika ngazi
mbalimbali za elimu ambapo kwa sasa ngazi ambazo siyo za elimu msingi na
sekondari zinatumia muundo wa kuanzia kwenye 0 badala ya 1.
c) Uwigo wa jumla wa alama kwa Kidato
cha Nne na Kidato cha Sita utaendelea kuwa wa alama 0 hadi 100 na kila kundi
katika uwigo huu limepewa tafsiri kwa ajili ya kuamua mambo mbalimbali
yanayohusu maendeleo ya mwanafunzi kulingana na malengo ya mtihani husika. Kimsingi,
tafsiri zifuatazo zitakatumika
(i) Alama A itakuwa na maana ya
ufaulu uliojipambanua (distincion or outstanding performance),
(ii) Alama B+ itakuwa na maana ya
ufaulu bora sana (excellent performance),
(iii) Alama B itakuwa na maana ya
ufaulu mzuri sana ( very good perfomance),
(iv) Alama C itakuwa na maana ya
ufaulu mzuri (good performance);
(v) Alama D itakuwa na maana ya
ufaulu wa wastani (low performance),
(vi) Alama E itakuwa na maana ya
ufaulu hafifu (very low performance), na
(vii) Alama F itakuwa na maana ya
ufaulu usioridhisha (unsatisfactory performance).
Wataalamu katika maeneo mbalimbali ya
elimu na ulimwengu wa kazi, kwa kushirikiana na Wizara, watatoa maana ya
tafsiri hizi kiutendaji katika maeneo yao kulingana pia na mahitaji yao.
d) Alama C iwe ndiyo alama ya ufaulu
mzuri ambao hauhitaji urekebu wa lazima, wakati alama D na E ni alama za ufaulu
unaohitaji urekebu kadri mwanafunzi atakavyokuwa anaendelea na masomo ili
kuthibitisha kama mlengwa anaweza na kulingana na mahitaji ya eneo husika
(targeted remediation). Alama F iwe alama ya eneo linalohitaji urekebu wa hali
ya juu (intesive remediation) ili mwanafunzi huyo aweze kumudu masomo kadri
anavyoendelea kukua kielimu ama atakapoingia katika ulimwengu wa kazi.
e) Makundi ya alama yatajumuisha CA
kwa kiwango cha asilimia isiyozidi 40 na mtihani wa mwisho kwa asilimia
isiyozidi 60 kwa makundi yote ya watahiniwa ikiwemo wale wa kujitegemea
(private candidates). Hii ni kwa kuzingatia kwamba CA siyo vizuri izidi uwigo
wa alama ya ufaulu mzuri unapoanzia ambayo ni C au 40.
f) CA kwa upande wa Kidato cha Nne
zitokane na mtihani wa Kidato cha Pili (alama 15), matokeo ya Kidato cha Tatu
(alama 5 kwa kila muhula, na hivyo jumla ya alama 10), mtihani wa Mock (alama
10) na kazi mradi au Projects (alama 5). Kwa upande wa Kidato cha Sita, CA
iendelee kutokana na muundo unaotumika sasa.
g) CA zitumike pia kwa watahiniwa wa
kujitegemea. Kwa upande wa watahiniwa wa kujitegmea ambao wanarudia Mitihani,
CA zao zitumike zile zilizotumika kutoa matokeo yake ya mitihani ya awali. Kwa
watahiniwa wa kujitegemea waliopitia mfumo wa Qualifying Test (QT), matokeo ya
QT yatumike kama CA na mtihani wa mwisho uchangie alama 60.
h) Kwa vile alama endelevu kwa mwaka
2013 kwa wanafunzi wa Kidato cha Nne tayari zimeshawasilishwa Baraza la
Mitihani Tanzania, alama hizo zichangie asilimia 40 katika mtihani wa Kidato
cha Nne mwaka 2013.
i) Muundo wa wastani wa alama katika
ufaulu (Grade Points Average ama GPA) utaandaliwa na kuanza kutumika pale
utakapokuwa tayari na wadau wataelimishwa kuhusu muundo huo ili wapate
kuufahamu na manufaa yake katika elimu ya sekondari.
j) Muundo huu mpya wa alama utatumika
kwa mzunguko wa miaka minne kabla haujahuishwa tena ili kuupa muda wa kutosha
kuona aina ya changamoto zinazojitokeza na jinsi ya kuzishughulikia. Aina hii
ya muda itaruhusu vidato vinne vya elimu ya
sekondari ya kawaida na nane ya
elimu ya sekondari ya juu kupimwa.
Hata hivyo, uhusihaji wa masuala ya mitihani
unaweza ukafanyika iwapo matokeo ya uhuishaji wa mitaala kwa ujumla utahitaji
pia eneo la mitihani liguswe na kuhuishwa pia.
Kwa mantiki hii, viwango vya alama na
ufaulu ni kama inavyooneshwa kwenye jedwali la 1 hapa chini:
Jedwali Na 1
MUUNDO WA ALAMA NA UFAULU
Kwa aina hii ya muundo wa alama, na
kwa kuwa muundo wa GPA utaanza kuandaliwa na wadau kuelimishwa kabla haujaanza
kutumika, katika kipindi hiki mpaka wakati huo, muundo wa madaraja utakuwa kama
inavyooneshwa kwenye jedwali la 2 hapa chini.
Jedwali Na 2
MUUNDO WA MADARAJA
Wataalamu wa mifumo ya mitihani
watalifanyia kazi zaidi jedwali hili la madaraja ili liweze kutumika kwa
ufanisi katika kipindi hiki cha mpito.
Kwa mantiki hii, Daraja Sifuri linafutwa
na kuwekwa daraja litakalojulikana kama Daraja la Tano na ambalo litakuwa ndilo
la mwisho kabisa katika ufaulu.
HITIMISHO
Mabadiliko haya yamefanyika ili
kuendelea kuimarisha mfumo wetu wa elimu na kuweka wazi taratibu mbalimbali kwa
ajili ya mitihani na masuala mengine. Yako mambo mengi mengine ambayo hayana
budi kuendelea kuimarishwa ikiwemo mfumo wa mitaala, walimu, mazingira ya
kujifunzia na kufundishia pamoja na vitabu na vifaa vingine muhimu katika
elimu. Masuala haya yanaendelea kuangaliwa kupitia mikakati mbalimbali ikiwemo
mpango wa Matokeo Makubwa Sasa ama Big Results Now (BRN).
Ushirikiano wa wadau
wote ili kuleta tija kwenye elimu ni muhimu sana na hivyo wizara itaendelea
kuwashirikisha wadau wote kwa kadri itakavyohitajika na wadau pia wanaombwa
wasiache kuishirikisha wizara pale watakapokuwa na jambo lolote ambalo
linahitaji ushirikiano ili kwa pamoja tuweze kupata mafanikio katika sekta ya
elimu.
Imetolewa,
KATIBU MKUU
WIZARA YA ELIMU NA MAFUNZO YA UFUNDI
No comments:
Post a Comment