Wednesday, October 30, 2013

WAHARIRI: USALAMA WA WANAHABARI HATARINI

Mwenyekiti wa chama cha waandishi wa habari mkoa wa Iringa Frank Leonard kulia. Picha hii ni ya
                                                                   Maktaba


Jukwaa la Wahariri nchini (TEF), limesema usalama wa wanahabari hauwezi kutenganishwa na mfumo wa sheria unaosimamia tasnia hiyo.
Kutokana na ukweli huo, TEF imeazimia kupigania uwepo wa sheria mahususi ambayo itawalinda wanahabari kutokana na asili ya kazi zao na mazingira hatarishi wanayofanyia ambayo huhatarisha usalama wao tofauti na taaluma nyingine.

Tamko hilo limetolewa Dar es Salaam jana na Katibu Mkuu wa TEF, Bw. Neville Meena wakati akisoma maazimio ya mkutano wao wa tatu wa kitaaluma uliofanyika mkoani Iringa, Oktoba 24 hadi 27 mwaka huu, uliojadili masuala ya kitaaluma, uendeshaji wa vyombo vya habari nchini.

Mkutano huo uliongozwa na mada isemayo; "Usalama wa Waandishi wa habari nchini Tanzania", kutokana na matukio makuu mawili yaliyotokea yakiwahusisha waandishi.
Alisema matukio hayo yamethibitisha kutetereka kwa usalama wa waandishi wa habari nchini hivi karibuni ambayo ni kuteswa hadi kusababishiwa ulemavu wa kudumu Mwenyekiti wa TEF, Bw. Absalom Kibanda na kuuawa kwa aliyekuwa Mwandishi wa Kituo cha Channel Ten mkoani Iringa, Daudi Mwangosi.

Aliongeza kuwa, mkutano huo pia ulijadili kwa kina matumizi ya Sheria ya Magazeti ya 1976 ambayo inatumiwa na Serikali kufungia magazeti kama ilivyotokea kwenye magazeti ya Mwananchi ambalo lilifungiwa wiki mbili na Mtanzania linaloendelea kutumikia adhabu ya kifungo cha siku tisini.

"Kimsingi tulikubaliana kwamba, tasnia hii imezingirwa na lengo la kuizingira ni kupoka uhuru wake, kuinyong'onyeza, kuisambaratisha, kuivunja uti wa mgongo ili isisimame wima kuutumikia umma kama ilivyo dhima yake bali iwatumikie wachache na kulinda masilahi yao ikiwa imejawa hofu.

"Usalama wa waandishi wa habari ni suala nyeti hivyo kwa kuzingatia yaliyowapata wanahabari wenzetu, tumeazimia tutafanya kila linalowezekana kuhakikisha tukio la kuuawa Mwangosi, kupigwa na kuteswa kwa Kibanda, yanakuwa matukio ya mwisho," alisema Bw. Meena.

Alisema wajumbe wa jukwaa hilo walisoma na kuijadili kwa kina ripoti ya kamati iliyochunguza tukio la Kibanda na kuazimia kuwa, ripoti hiyo siyo mwisho bali wataendelea na uchunguzi ambao wanaamini siku moja utatusaidia kupatikana ukweli.
Bw. Meena alisema TEF inasikitishwa na ukimya ambao umeendelea kuwapo juu ya suala hilo serikalini, ndani ya Jeshi la Polisi kwani hadi sasa hakuna mtu aliyekamatwa na kufikishwa mahakamani.

"Hali hii inaweza kuwa kichocheo cha wanaotekeleza matendo haya kuendelea kuwadhuru waandishi wa habari, tunaendelea kusubiri uchunguzi wa polisi na tungependa kuona wahusika wanakamatwa na kufikishwa mahakamani," alisema.
Aliongeza kuwa, mkutano huo pia ulitupia jicho vyumba vya habari jinsi vinavyofanya kazi zake kila siku na kukubaliana kuwa, vyombo vya habari vinaendeshwa na binadamu hivyo wahusika hawapaswi kuwa juu ya sheria, wanapofanya makosa tuwe tayari kusahihishwa.

Alisema walikubaliana kuwa si busara kwa Serikali kuyafungia magazeti kwa kutumia sheria ambayo tayari imetajwa kuwa ni kandamizi, inakinzana na haki ya kupata habari.
"Pia tulikubaliana maadili na weledi ndiyo ngao ya kwanza ya mwanahabari, tuepuke tabia na utendaji unaoweza kutuletea matatizo yasiyo ya lazima tukiwa watumishi wa kweli wa umma, itakuwa rahisi hata kuulilia umma pale tutakapoonewa na kunyanyaswa.
"Wahariri walikumbushana kutimiza wajibu wao kitaaluma kwa kuzingatia miongozo maalumu ya uandishi wa habari ambayo ni pamoja na; Nia Njema, Ukweli na Usahihi," alisema.

Bw. Meena alisema, TEF itaendelea kushirikiana na vyombo vingine vya kihabari kama Taasisi ya Habari Kusini mwa Afrika (Misa Tan), Baraza la Habari nchini (MCT), Chama cha Wanahabari Wanawake nchini (TAMWA) na vinginevyo kuhakikisha kwamba tasnia inatekeleza majukumu yake kwa kuzingatia weledi na miongozo ya kihabari
Chanzo: Majira

No comments: