Picha hii ni ya Maktaba
Chama cha Wananchi (CUF) kimelaani
vitendo vya wananchi kupigwa, kuteswa na wengine kupoteza mali zao wakati wa
utekelezaji wa operesheni kuondoa majangili na wahamiaji haramu katika maeneo
mbalimbali ya nchi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa
vyombo vya habari Dar es Salaam jana na kusainiwa Naibu Mkurugenzi wa Habari na
Haki za Binadamu na sheria wa CUF, Abdul Kambaya, operesheni hiyo imesababisha
mtu mmoja kupoteza maisha na wengine kupoteza mali zao.
Alisema katika maeneo inapofanyika
operesheni hiyo kama vile Katavi na Kilindi kumeripotiwa kutokea madhara
makubwa ya wananchi kupigwa na mmoja kuuawa katika Kata ya Majimoto mkoani
Katavi.
Pia alisema Diwani wa Kata Majimoto
mkoani katavi aliyetambulika kwa jina moja la, Serengeti alipigwa na vikosi
vinavyohusika kwenye operesheni hiyo pale alipo hoji iweke operesheni hiyo
ifanyika kwenye Kata anayoiongoza bila ya kujulishwa ili aweze kutoa
ushirikiano.
"Mkazi mmoja alipigwa risasi na
Vikosi hivyo vinavyotekeleza Operesheni hiyo na Mchungaji wa Kanisa la
Anglikana, Geofrey amekimbia kipigo na kuacha nyumba yake kukiwa na sh. 800,000
na Biblia ambazo zimechukuliwa," alidai Kambaya.
"CUF kinamuomba Rais Kikwete
kulitazama jambo hili kwa undani na kuweza kuwasaidia wa nanchi kuondokana na
adha kubwa wanayopata, " alisema Kambaya.
Aliongezea kuwa vikosi vinavyoendesha
operesheni hiyo vijue kuwa si kila mwananchi ni mhamiaji haramu au jangili,
hivyo kazi hiyo ifanyika kwa mujibu.
Alisema utaratibu unaotumika utashusha
heshima ya vikosi vyetu vya Ulinzi ndani ya Taifa letu, lakini utaratibu huo
utafanikiwa kujenga hofu na uadui baina ya wananchi na vikosi vyetu vya Ulinzi.
Alitoa wito kwa Taasisi za Haki za
Binadamu na Mambo ya Sheria kuweza kufika Mkoa wa Katavi Kata ya Majimoto
kwenda kujionea hali ilivyo .
Pia Taasisi zinazojishughulisha na
kutoa Misaada ya Kibinadamu kama Msalaba Mwekundu na nyingine kwenda mkoani
Katavi kutoa misaada kwa familia zilizoathirika na Operesheni hiyo.
No comments:
Post a Comment