Thursday, October 31, 2013

Mageuzi sekta ya elimu



•  Madaraja ya ufaulu yapanguliwa, sifuri lafutwa

na Lucy Ngowi
WIZARA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, imefanya marekebisho katika upangaji wa viwango vya alama za matokeo ya wanafunzi wa kidato cha nne kwa kufutwa daraja sifuri na kuwekwa daraja la tano, ambalo litakuwa la mwisho katika ufaulu.
Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Profesa Sifuni Mchome, alitangaza mageuzi hayo jana alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu upangaji wa viwango vya alama, matumizi ya alama endelevu ya mwanafunzi na ufaulu.

Alisema kwa muundo mpya, daraja la kwanza litabakia kuanzia pointi 7 hadi 17 kama ulivyokuwa muundo wa zamani, ambalo ni kundi la ufaulu uliojipambanua na bora sana, daraja la pili litaanzia pointi 18 hadi 24, badala ya pointi 18 hadi 21 kama zamani na likiwa ni kundi la ufaulu mzuri sana.

Pia daraja la tatu pointi zake zitaanzia 25 hadi 31, badala ya zile za zamani za 22 hadi 25 na kundi hili litakuwa la ufaulu mzuri wa wastani.
Kwa mujibu wa Prof. Mchome, daraja la nne litaanzia pointi 32 hadi 47, badala ya zile za zamani za kuanzia pointi 26 hadi 33, na kundi hilo litajulikana kama la ufaulu hafifu.
Daraja jipya lililoongezwa ni lile la tano, litakaloanzia pointi 48 hadi 49, litakalofuta daraja sifuri la zamani, lililokuwa na pointi 34 hadi 35, na sasa litajulikana kama kundi la ufaulu usioridhisha.

Prof. Mchome alifafanua kuwa mabadiliko hayo yamefanyika ili kuendelea kuimarisha mfumo wa elimu na kuweka wazi taratibu mbalimbali kwa ajili ya mitihani na masuala mengine.

Pia alisema wataalamu wa mifumo ya mitihani wataufanyia kazi zaidi muundo huo wa madaraja ili uweze kutumika kwa ufanisi katika kipindi hiki cha mpito.
“Yapo mambo mengi mengine ambayo hayana budi kuendelea kuimarishwa, ukiwamo mfumo wa mitaala, walimu, mazingira ya kujifunzia na kufundishia pamoja na vitabu na vifaa vingine muhimu katika elimu,” alisema.

Awali alisema kuwa wizara imekusanya maoni ya wadau wa elimu kuhusu upangaji wa viwango vya alama katika mitihani ya kuhitimu kidato cha nne na cha sita pamoja na matumizi ya alama za tathmini endelevu ya mwanafunzi.
Alisema maoni hayo ya wadau yamekusanywa kwa sababu kwa muda mrefu sasa upangaji wa viwango vya alama vinavyotumika na utaratibu wake katika mitihani hiyo yote ni vya elimu ya sekondari.

“Sera ya elimu na mafunzo ya 1995 imeelekeza kwamba katika kuamua kiwango cha ufaulu wa mwanafunzi wa elimu ya sekondari, alama za tathmini endelevu ya mwanafunzi zitachangia asilimia 50 na mtihani wa mwisho asilimia 50.
“Kwa upande wa Zanzibar alama hizo zimekuwa zikiandaliwa kwa mfumo wa asilimia 40 na mtihani wa mwisho asilimia 60. Pamoja na kwamba baraza halijawahi kuitumia mifumo hii tokea ilipowekwa, kumekuwa na mitazamo, maoni na mapendekezo tofauti katika muundo na matumizi ya alama hizo,” alisema.

Vilevile alisema kuwa wadau wengi walishauri muundo uliopo sasa wa madaraja uimarishwe ili kuanza kutumia muundo wa wastani wa alama katika ufaulu (GPA), kwa kuwa ni rahisi kueleweka na kuuandaa kuliko muundo wa madaraja.
Pia kwa kutumia muundo huo wa GPA inakuwa rahisi katika kukadiria uwezo wa mwanafunzi kielimu na kufanya uamuzi mbalimbali ikiwamo kuendelea na masomo katika ngazi mbalimbali za elimu.

Wakati huo huo, Prof. Mchome alisema kuwa mtihani wa kidato cha nne na mtihani wa maarifa mwaka huu unatarajiwa kufanyika nchini kote kwa siku 18 kuanzia Novemba 4 hadi 21.
Alisema jumla ya watahiniwa walioandikishwa kufanya mtihani huo ni 427,906, ambapo kati yao 367,399 ni watahiniwa wa shule na 60,507 ni wa kujitegemea.

Kwa mujibu wa katibu mkuu huyo, hadi sasa maandalizi na usafirishaji wa mitihani hiyo hadi ngazi ya mkoa yamekamilika.
Alitoa wito kwa kamati za mitihani za mikoa yote kuhakikisha kuwa taratibu zote za utunzaji, uhifadhi na usafirishaji wa mitihani hiyo zinazingatiwa.
Chanzo: Tanzania Daima

No comments: