na Grace Macha, Arusha
WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Balozi
Khamis Kagasheki, amesema kuwa suala la Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Arusha
(RCO), Duwan Nyanda, anayetuhumiwa kutorosha watuhumiwa wa ujangili
linashughulikiwa na Inspekta Jenerali wa Jeshi la Polisi (IGP), Saidi Mwema.
Mwishoni mwa wiki iliyopita,
Kagasheki alimtuhumu RCO huyo kuhujumu operesheni ‘Tokomeza Majangili’, baada
ya kudaiwa kuwatorosha majangili wawili raia wa kigeni.
Akizungumza na waandishi wa habari
jana jijini Arusha, Kagasheki alisema kuwa vita dhidi ya ujangili wa meno ya
tembo inayotishia kutoweka kwa wanyama hao haitakoma mpaka majangili hao
waache.
Aliongeza kuwa watumishi wa serikali
wanaowasaidia majangili hao wanasukumwa na ubinafsi kwa kuamua kujinufaisha
binafsi na rasilimali hizo za umma.
Alisema operesheni hiyo ya ‘Tokomeza
Ujangili’ iliyoanza hivi karibuni inahusisha majeshi yote ya ulinzi na usalama.
RCO Nyanda anadaiwa kusaidia
kuwatorosha watu wawili wenye uraia wa Saudi Arabia ambao walikuwa
wakishikiliwa baada ya kukutwa wakiwa na silaha na baadhi ya vithibitisho
vinavyoonesha walikuwa majangili.
“Inasikitisha sana na inaturudisha
nyuma ikiwa kama kiongozi wa jeshi anayevaa sare ya Watanzania, kwa makusudi
anawaachia watuhumiwa wa ujangili na kusaidia kuondoka nchini,” alisema
Kagasheki wakati akizungumza na waandishi mwishoni mwa wiki.
Alisema katika tukio hilo, polisi
walifanikiwa kuwakamata watu hao wakiwa na vithibitisho vyote vya kujihusisha
na ujangili na kuwapeleka kituo cha polisi Arusha kwa ajili ya mahojiano.
Alifafanua kuwa kabla ya kuwekwa
rumande, watu hao walinyang’anywa hati zao za kusafiria ili kuwazuia
wasitoroke. Lakini katika hali ya kushangaza RCO Nyanda alihakikisha anawatoa
nje kwa dhamana na kisha aliwakabidhi hati hizo kitu kilichosababisha watoroke
nchini.
Mapema akifungua mkutano wa mwaka wa
Chama cha Mashirika ya Utangazaji ya Kusini mwa Afrika (Saba) jijini hapa jana,
Makamu wa Rais, Dk. Mohammed Gharib Bilal, alivitaka vyombo vya habari vya nchi
hizo kujikita katika kutangaza vivutio vilivyopo.
Alisema lengo ni kuongeza idadi ya
watalii watakaovutiwa kuvitembelea ili kukuza uchumi wa nchi zao.
Pia vimetakiwa kuandaa vipindi vya
maendeleo ikiwamo kutangaza vivutio vya kiutamaduni ambapo mbali na kuyaingizia
mapato mataifa yao kutawezesha kuongeza fursa za ajira kwa wananchi wa maeneo
husika.
Alisema kuwa vyombo vya habari ni
muhimu katika kuelimisha na kuburudisha lakini vikitumiwa vizuri vinaweza
kuchangia kuleta maendeleo ikiwamo sekta ya utalii.
Dk. Bilal alisema suala la kutangaza
vivutio vya Afrika lisiachiwe vyombo vya habari vya nje ya bara pekee ambavyo
huwashawishi watalii kwenda maeneo wanayoyataka wao, bali vitangaze maeneo yote
kwa kueleza uzuri wake.
Alivitaka vyombo hivyo kutoa elimu
kwa umma juu ya umuhimu wa uhifadhi na ulinzi wa vivutio vya maliasili badala
ya kusubiri ziharibike ndipo vianze kutoa taarifa za madhara.
Dk. Bilal alivitaka vyombo vya habari
nchini kuungana na serikali katika kukabiliana na ujangili ili kuhakikisha
unamalizika kabisa.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Hifadhi za
Taifa nchini (Tanapa), Allan Kijazi, alisema tayari wamekamilisha taratibu za
Mamlaka ya Udhibiti na Usimamizi wa Mawasiliano nchini (TCRA) ili waruhusiwe
kuandaa filamu za wanyamapori.
Alisema kuwa kwa sasa ni watu kutoka
mataifa ya Ulaya ndio hufika kwa ajili ya kuandaa filamu hizo, hivyo kukamilika
kwa taratibu ni fursa kwa shirika hilo kuanza kuandaa filamu hizo zikionesha na
kuzungumzia vivutio vyote vya utalii vilivyoko nchini.
Kijazi alisema kwa sasa ni vivutio
vichache tu ndivyo vinavyotambuliwa huku vingi vikiwa vimeachwa, jambo
alilotaka kuwepo na mwamko miongoni mwa wanahabari kuvitangaza kwa kufuatilia
ni kitu gani kipya kinaendelea kwenye sekta ya utalii na kuvitangaza kwa
usahihi.
Mkutano huo wa siku nne unahudhuriwa
na washiriki kutoka nchi 14 za SADCC, ambapo pia ulihudhuriwa na Waziri wa
Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Prof. Makame Mbarawa.
Chanzo: Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment