Rais wa Bunge la Uswisi, Maya Graf
(wa nne kushoto) akizungumza na waandishi wa habari wa magazeti ya Mwananchi na
The Citizen katika mahojiano maalumu, jijini Dar es Salaam. PICHA | EMMANUEL
HERMAN
Na Noor
Shija, Mwananchi
Kampuni ya Mwananchi Communications
Ltd kupitia magazeti yake ya Mwananchi na The Citizen, yalipata fursa pekee ya
kumuhoji Rais Maya Graf, kuhusiana na masuala mbalimbali ikiwamo madhumuni ya
safari yake, mabilioni hayo, uwazi wa mishahara ya viongozi wa juu serikalini
na uhuru wa vyombo vya habari. Mwandishi wetu, Noor Shija alikuwa mmoja wa
walioshiriki kufanya mahojiano na kiongozi huyo wa kitaifa na yafuatayo ni
mahojiano hayo:
Swali: Nini madhumuni ya safari yako
na hii ni mara yako ya kwanza kutembelea Afrika na hasa Tanzania?
Jibu: Hii siyo mara yangu ya kwanza
kutembelea Afrika, mara ya kwanza kuja Afrika ilikuwa mwaka 2011, nilitembelea
nchi ya Senegal. Lakini kwa Tanzania ni mara yangu ya kwanza na kwa wadhifa
wangu wa Rais naruhusiwa kusafiri nje ya nchi.
Na mimi nilichagua Tanzania kwa
sababu ya uhusiano mzuri kati ya Uswisi na Tanzania uliodumu kwa miaka mingi.
Kuna raia wengi wa Uswisi wanaoishi Tanzania, pia tunasaidia miradi mbalimbali
ya maendeleo kama vile hospitali ya Ifakara (Morogoro), ambayo nimeitembelea.
Pia tunashiriki katika uendelezaji wa
miradi mingine mbalimbali kama vile sekta ya kilimo, makazi na masuala mengine
yanayohusiana na Serikali. Nikiwa Rais wa Bunge ni muhimu kwangu kuthibitisha
fedha tunazosaidia Tanzania kama zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.
Swali: Ulikutana na Spika wa Bunge la
Tanzania, Anne Makinda. Mazungumzo yenu yalilenga maeneo gani na nini matokeo
ya mkutano wenu?
Jibu: Kwanza nilifurahi kuonana na Spika,
kwa kuwa sote ni wanawake katika nafasi ya uongozi unaofanana, mazungumzo yetu
yaliegemea sana kuhusu nafasi za wanawake katika uwakilishi wa uongozi wa
kisiasa.
Tulizungumza kuhusu kanuni na
taratibu za mabunge yetu, pia tulizungumza kuhusu changamoto tunazokabiliana
nazo.
Pia tulizungumza kuhusu idadi ya
wanawake ndani ya Bunge na umuhimu wa wanawake kushika nafasi za uongozi katika
sekta ya elimu, sekta ya uchumi na katika ngazi za juu za uongozi. Hayo ndiyo
tuliyozungumza.
Swali: Nchi yako imekuwa na uhusiano
wa muda mrefu na Afrika, na hasa Tanzania katika masuala ya Bunge, diplomasia
na misaada ya maendeleo. Kwa kifupi unaweza kuelezea uhusiano wa masuala ya
Bunge na hasa katika kubadilishana uzoefu?
Jibu: Tuna uhusiano wa muda mrefu hasa
katika ngazi ya kibunge, tumekuwa tukifanya kazi pamoja katika masuala ya umoja
ya kibunge (Inter-Parliamentary Union-IPU), ambapo *fanyika Geneva, Uswisi,
hivi karibuni Anne Makinda alihudhuria, lakini hatukubahatika kuonana.
Masuala mengine ni kama vile misaada
ya kimaendeleo ambayo imeimarisha uhusiano kati ya Tanzania na Uswisi, mfano
miradi iliyopo Dodoma na Ifakara (Morogoro).
Swali: Walipakodi wa Uswisi wamekuwa
wakichangia juhudi za maendeleo ya Tanzania katika kupambana na umaskini
kupitia nyanja za maendeleo ya kiuchumi, utawala bora, afya, maji na masuala ya
jenda. Uwazi na rushwa ni mijadala iliyotawala Bunge letu, ni uzoefu upi
unaoweza kutolewa kati ya nchi hizi mbili kuhakikisha utawala bora na vita
dhidi ya rushwa?
Jibu: Kwanza napenda kuweka sawa kuwa
suala hili nitalizungumzia hasa kwa upande wa Uswisi, na sitaweza kutoa maoni
yoyote kwa upande wa Tanzania.
Kutokana na taratibu na kanuni za
Bunge la Uswisi, nina wajibu kwa Serikali yangu, pia nina wajibu kwa Bunge.
Tumekuwa tukitoa taarifa za uwajibikaji wa Serikali wa ngazi zote na wananchi
wana haki ya kupata taarifa wanazozitaka kuhusiana na utendaji wa Serikali yao
kwa ngazi zote.
[Balozi wa Uswisi nchini, Olivier
Chave, aliingilia kati na kufafanua kuwa; kila mwananchi anayetaka taarifa
kuhusu Serikali yake, ana haki kwa mujibu wa Katiba kupata taarifa hizo.
Hata hivyo, Rais Graf aliendelea
kutoa maelezo kuwa ni muhimu kuwapa taarifa wananchi ambazo kwa kiasi kikubwa
zinahamasisha kuwapo kwa uhuru wa kutoa maoni, akisema: “Jana (Jumanne)
tulitembelea TMF (Tanzania Media Fund) ambao tunawasaidia. TMF tunawafadhili na
hasa katika kuboresha uandishi wa habari.”
Ni muhimu pia kuwa na taasisi zisizo
za kiserikali na taasisi za kijamii zenye nguvu zinazoweza kuaminika na
kusimamia uwajibikaji.
Swali: Uswisi inaridhishwa na namna
Tanzania inavyotumia misaada yake?
Jibu: Napenda kusema kuwa Uswisi imekuwa
ikisaidia nchi nyingi na msaada wake kwa Tanzania uko kwenye miradi mbalimbali ambayo
fedha hupitia kwenye bajeti ya serikali. Ni vizuri kuwa na udhibiti mzuri
katika kuendeleza miradi hiyo. Na hii ni moja ya sababu za mimi kuwapo Tanzania
kwa ajili ya kuangalia miradi ambayo tunasaidia.
Hapo likaulizwa swali la nyongeza
lililotaka kufahamu maoni ya Uswisi kuhusu uamuzi wa Serikali ya Tanzania
kufungia magazeti mawili, Mwananchi na Mtanzania.
Jibu: Kwa hili nitazungumzia kwa upande wa
nchi yangu ambako ndiko nawajibika. Nakumbuka tukio la kufungia gazeti
lilitokea wakati wa Vita vya Pili vya Dunia (vilivyopiganwa mwaka 1939 hadi
1945), tangu wakati huo hakuna utaratibu wala sheria ya kufungia vyombo vya
habari.
Hapo tena Balozi Chave alifafanua
zaidi kwamba; nimeulizwa sana suala hili, ninachoweza kusema ni kwamba Uswisi
hatuna sheria ya kufungia magazeti au vyombo vya habari. Kama kuna mtu au
Serikali wataona hawakutendewa haki na chombo cha habari, kwa kuchafuliwa au
namna yoyote, mlalamikaji anatakiwa kwenda mahakamani ambako ndiko haki
inapatikana. Serikali ikikosewa na chombo cha habari itaenda mahakamani kama
mlalamikaji.
Itaendelea wiki ijayo.
Chanzo: mwananchi
No comments:
Post a Comment