Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, ametoa rai kwa viongozi wa dini kukemea
watu wanaogeuza nyumba za ibada kama njia ya kutaka kufanikisha malengo yao ya
kisiasa kwa kutoa michango ya fedha wanazozipata kwa njia ya ufisadi.
Kwa mujibu wa Ofisa Habari Mwandamizi
wa chama hicho, Tumaini Makene, Mbowe alitoa wito huo mwishoni mwa wiki wakati
akiongoza harambee ya kuchangia ujenzi wa jengo la Kanisa la Kiinjili la
Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Sono uliopo katika kijiji cha
Masama-Sono, wilayani Hai.
Aliwataka viongozi wa dini zote
nchini kukemea suala hilo na wawe makini na watu wa namna hiyo, badala ya
kuangalia kiwango cha ukubwa wa fedha wanazotoa bali uhalali na usafi wa kile
wanachochangia.
Mbowe aliwapongeza waumini wa
usharika huo kwa kuamua kujenga kanisa hilo wao wenyewe, tangu mwaka 1994.
"Kwanza napenda kuwapongeza
Watanzania wenzangu na waumini wa usharika huu wa Sono, kwa kuifanya kazi ya
Mungu, mlipoamua kujenga jengo hili zuri kwa nguvu zenu wenyewe, polepole tangu
mwaka 1994 na sasa bado mnaendelea, mkiwa mmemaliza sehemu kubwa ya kazi hii
muhimu.
"Katika hatua hii ningependa pia
kutoa rai yangu kwa viongozi wetu wa dini nchini. Nitajengea hoja zangu
kutokana na mahubiri ya Baba Askofu Erasto Kweka. Kwa siku za hivi karibuni
kumeibuka tabia ya watu kugeuza nyumba za ibada kuwa ni soko au mapango ya
walanguzi.
"Watu wengine wanajulikana
wamepata fedha kwa dhuluma, wizi, rushwa na ufisadi mwingi, fedha ambazo
zingeweza kutumika kununulia dawa za watoto wetu hospitalini, dawa za akina
mama hospitalini, kuboresha elimu yetu inayoporomoka na huduma zingine muhimu.
"Wanapita kwenye nyumba za ibada
wakitumia kama sehemu za kujisafisha na kujitakasa kwa kutoa kiasi kikubwa cha
fedha. Sisemi muwalaani na kuwafukuzilia mbali, bali muwaombee sana ili wawe
wasafi, wakija kwenye nyumba za ibada, waje wakiwa safi ili hata wanachotoa
kiwe na baraka, kwa sababu wakiendelea kutoa fedha zao chafu wanakosa hizo
baraka," alisema.
Alisema anawasihi viongozi hao
wasiingie kwenye mtego wa kuangalia ukubwa wa michango inayotolewa na watu
kwenye nyumba za ibada, bali waangalie usafi wa hicho kinachotolewa, wasikubali
mahali pa ibada kutumika kusafisha fedha chafu. Endeleeni kuwaombea wapate
utakaso na kukiri dhambi zao.
Aliongeza kuwa yeye na wenzake
hawapambani na serikali kwa sababu hawana adabu, bali wameamua kuwa sauti ya
watu wengi wanyonge wasiokuwa na sauti katika kupata haki na matumaini katika
nchi yao.
"Na ni vyema waumini wenzangu
tukaelewana vyema, ninaposema vyama vya upinzani wajibu wake ni kuikosoa
serikali na chama kilichopo madarakani kwa wakati huo, hatumaanishi tunapambana
na serikali kwa sababu hatuna adabu, bali tumeamua kuwa sauti ya wanyonge wengi
katika nchi hii.
Naye Askofu Mkuu mstaafu wa KKKT,
Erasto Kweka, alimshukuru mbunge huyo kuwa pamoja na kutingwa na majukumu
mengi, kuitikia wito wa kujumuika na waumini wa usharika huo na kuwatia nguvu
katika ujenzi wa kanisa lao, akimtaka aendelee na moyo huo.
"Tunajua kutokana na majukumu
yako, umejibidisha sana kufika hapa. Mungu aendelee kukutia nguvu na kukujengea
moyo wa namna hiyo si kwa ajili ya kanisa tu, bali kwa ajili ya jamii nzima ya
Watanzania inayohitaji utumishi wa watu wanaojitoa.
Takriban Sh. milioni 16 zilichangwa
kwa fedha taslim na ahadi, katika harambee hiyo, ambapo waumini usharika huo
walichangia jumla ya Sh. 7,956,800 huku mbunge huyo akichangia Shilingi milioni
nane.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment