• Raia wa kigeni
aliowaita majangili, walibambikwa kesi
na Grace Macha, Arusha
JESHI la Polisi mkoani Arusha,
limeingia kwenye kashfa nzito baada ya kubainika kumdanganya Waziri wa
Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki kwa kuwahusisha raia wawili wa
kigeni na biashara ya ujangili wakati si kweli.
Hatua hiyo inakuja baada ya Waziri
Kagasheki kudai kuwa watumishi wa serikali wanakwamisha juhudi za kukabiliana
na majangili wa tembo, akitolea mfano wa Mkuu wa Upelelezi wa Polisi
mkoani hapa (RCO), Duwan Nyanda, kwamba aliwatorosha raia wawili wa Saudia
ambao walikamatwa wakiwa na meno ya tembo pamoja na silaha nzito.
Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali na
nyaraka kadhaa, Tanzania Daima limebaini kuwa raia hao waliingia nchini
Septemba 12, mwaka huu, kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa
Kilimanjaro (KIA) na kisha kufikia kwenye hoteli ya kitalii ya Mount Meru.
Nyaraka hizo zinaonyesha kuwa wageni
hao waliondoka nchini Oktoba 4, mwaka huu, kupitia uwanja huo huo.
Kwa mujibu wa waraka wa upekuzi wa
polisi (search order) uliosainiwa na Inspekta James, maofisa wa jeshi hilo
walifika kwenye hoteli hiyo Oktoba 3, mwaka huu, na kupekua vyumba vya wageni
hao, lakini hawakukuta kitu chochote kinachohusiana na nyara za taifa za
maliasili kama ilivyodaiwa na Waziri Kagasheki.
Nyaraka hiyo inaonyesha kuwa
walioshuhudia upekuzi huo mbali na waliokuwa watuhumiwa, Ali na Nader, ni
pamoja na Gidion David na Joseph Enock ambao waliisaini.
Tanzania Daima lilifika hotelini hapo
na kuzungumza na meneja mapokezi, Enock Maselle ambaye pia alithibitisha kuwa
Oktoba 3, mwaka huu, walifika polisi kwa ajili ya kukagua vyumba vya wateja
wao, Ali na Nader.
Alisema kuwa waliwaruhusu, lakini
akadai ni vigumu kujua nini kiliendelea.
Raia hao wanadaiwa kujihusisha na
kutafuta watu nchini mwao ambao huwaleta Tanzania kutalii, na kwamba waliingia
nchini na kundi la wageni tisa ambao walifanya safari kwa nyakati mbili
tofauti, wakitembelea hifadhi za taifa za Manyara na Tarangire na Ngorongoro
iliyopo chini ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA).
Mmiliki wa kampuni ya uwakala wa
utalii ya Kalabash, Ally Kalabash aliliambia gazeti hili kwa simu kuwa Ali na
Nader walimletea wageni tisa ambao alifanya nao safari ya siku tatu katika
mbuga za Manyara, Ngorongoro na Tarangire.
“Hawa ni mawakala wapya, na hii ni
mara yangu ya kwanza kufanya nao kazi, ila wageni walioniletea niliwahudumia
mpaka siku wanaondoka, kwani wengine walilala Mount Meru Hotel na wengine Themi
Suite,” alisema.
Naye Salim Islam Salim ambaye ndiye
alikuwa karibu na raia hao wa Saudia, alisema kuwa walipokuwa hapa nchini
walikutana na Richard Kalembe ambaye aliwaambia anamiliki kampuni ya
uwindaji wa kitalii ya RS Kalembe Hunting Routes.
Alisema kuwa Septemba 14, mwaka huu,
Ali na Nader walimlipa Kalembe malipo ya awali kwa ajili ya kwenda kuwinda
kitalii, kiasi cha dola za Marekani 3,000.
Salim alifafanua kuwa Kalembe
aliwapatia wageni hao risiti yenye namba 012 ikionyesha kuwa bado wanadaiwa
dola 7,000 endapo watatumia siku tano na ikiwa watatumia siku tisa wakiwinda,
basi wangelazimika kuongeza dola 9,000.
Kwa mujibu wa Salim, baada ya Kalembe
kupokea malipo hayo, hakufanya mawasiliano tena na wageni hao, hatua
iliyowalazimu kutoa taarifa polisi Oktoba 2, mwaka huu.
Alisema kuwa siku iliyofuata, raia
hao walipigiwa simu na polisi wa upelelezi aliyemtaja kwa jina moja la James,
akiwaambia kuwa mtuhumiwa wao ameshapatikana, hivyo wafike polisi ili
wakakabidhiwe fedha zao.
“Katika hali ya kushangaza,
walipofika polisi waligeuziwa kibao na kuwekwa chini ya ulinzi, wakitakiwa
kwenda kupekuliwa kwenye vyumba vyao katika hoteli waliyofikia ya Mount Meru,
ambako hata hivyo hawakukutwa na kitu.
“Baadaye walirudishwa polisi na
kuelezwa sababu za kupekuliwa, kwamba walitiliwa shaka kuwa wanajihusisha na
ugaidi,” alisema Salim.
Alifafanua kuwa polisi waliwaambia
kuwa kutokana na tukio la kigaidi lililotokea hivi karibuni nchini
Kenya, wamekuwa makini kwa kila mtu wanayemuhisi au kumtilia shaka, na
hivyo humfanyia upekuzi.
Kwa mujibu wa Salim, baada ya maelezo
hayo walielezwa kuwa wanaweza kuwadhamini. Yeye na mtu mwingine aliyemfahamu
kwa jina moja la Ibra, walimdhamini Ali huku Nader akidhaminiwa na
msichana mwingine ambaye hakumfahamu vizuri.
“Oktoba 4, tulifika pale polisi
asubuhi, baada ya panda shuka, watuhumiwa hao waliwaeleza polisi kuwa wanapaswa
kuondoka siku hiyo, hivyo wakaomba wapewe ruhusa wakabadili tiketi zao au
wapelekwe mahakamani ili wajue wanashikiliwa kwa makosa gani.
“Tukiwa pale, akaja polisi mmoja
mwanamke akasema ‘kama hawa mmewapekua mkaona hawana kitu, waachieni waende
zao’. Ilikuwa kama saa tano asubuhi,” alisema.
Salim alisema kuwa wageni hao
walipewa simu na hati zao za kusafiria na hivyo wakaondoka kituoni hapo,
na baadaye jioni walipanda ndege ya Shirika la Ndege la Ethiopia na kurudi
kwao.
Alisema kuwa alishangazwa na taarifa
zilizoandikwa na vyombo mbalimbali vya habari zikiwahusisha Ali na Nader na
uwindaji haramu huku wakidaiwa kukutwa na pembe za ndovu, jambo alilodai ni
uongo na upotoshaji mkubwa.
Salim alisema madai ya kwamba dola
3,000 zilitolewa polisi kama rushwa si ya kweli, kwani kiasi hicho ni fedha
anazodaiwa Kalembe alizochukua kwa raia hao, huku akidai taarifa iko
polisi.
Alipotafutwa Kamanda wa Polisi mkoani
hapa, Liberatus Sabas kuzungumzia sakata hilo, alisema hayuko tayari kwa sababu
linashughulikiwa na mkuu wa jeshi hilo, IGP Said Mwema ambaye ameunda tume ya
uchunguzi.
Naye Waziri Kagasheki alipotafutwa,
simu yake iliita bila kupokelewa.
Salim ageuziwa kibao
Katika hatua nyingine, Salim na
Gerald Kashiro wamelalamikia kitendo cha kukamatwa na askari wa kuzuia ujangili
kwa nyakati tofauti na kupewa mateso makali, huku mfanyabiashara Shafiq Feroz
akidai kuwa alishikiliwa bila kuteswa.
Walisema chanzo cha mateso hayo ni
nyama ya nyati kilo tano ambayo Feroz alimpatia Kashiro baada ya kuwa
amemsindikiza kuwinda kwenye pori la Terati wilayani Simanjiro.
Kashiro alisema kuwa yeye alipopewa
nyama hiyo alimwachia mke wake, Judith Gerald nyumbani akiendelea
kuiandaa, huku yeye akiendelea na shughuli zake.
Alisema kuwa baadaye alipigiwa simu
akiambiwa kuwa mkewe na mama mkwe, wamekamatwa na askari wa Kikosi cha Kuzuia
Ujangili (KDU) wakiwa na wanajeshi.
Akisimulia mkasa mzima, Salim alisema
kuwa Kashiro alimpigia simu akimuomba ampeleke alipo Feroz ili aweze kupeleka
vibali vyake vya uwindaji kwa kambi ya KDU iliyopo Njiro waweze kuwaachia
mkewe na mama mkwe.
Alisema kuwa baada ya kumfikisha kwa
Feroz, aliwaacha wakaelekea Njiro, na yeye akarudi kuendelea na shughuli zake,
lakini wakampigia simu tena wakimuomba akawadhamini kwani wameshikiliwa.
Kwa mujibu wa Salim, juhudi za
kuwadhamini Kashiro na Feroz hazikufanikiwa, hivyo aliamua kuondoka.
Lakini kabla hajafika kwenye lango kuu la kutokea, akaitwa na kuulizwa na
askari nyumbani kwake ni wapi ili wakampekue.
Aliongeza kuwa alipopekuliwa nyumbani
kwake Kimandolu, alikutwa na bunduki tatu aina ya riffle na bastola aina ya
short-gun ambazo zote anazimiki kihalali na kwamba walijiridhisha baada ya
kuwaonyesha nyaraka zote muhimu kisha wakarudi naye hadi KDU Njiro.
“Mimi na Feroz tuliambiwa tujidhamini
wenyewe kwani tunaacha silaha zetu pale. Feroz naye alikuwa amepekuliwa kwenye
hoteli ya Themi Suites alipokuwa amefikia kutoka Dar es Salaam anakokaa.
“Tulitakiwa kurudi siku inayofuata,
yaani Oktoba 8, mwaka huu, lakini tulipofika siku hiyo, tukachukuliwa na
kufungwa pingu, tukapakiwa kwenye gari tukapelekwa Terati. Huko kuna eneo
limefungwa hema, tulipofika sikuamini kama Tanzania kuna watu wanateswa hivyo,”
alidai.
Kwa mujibu wa Salim, aliwekewa vijiti
katikati ya vidole vyake na kuanza kuminywa, lakini akawahakikishia kwamba
hajihusishi na ujangili.
“Wakachukua dumu la maji baridi
la lita 10 na muda huo ni usiku, baridi ni kali, wakanimwagia mwili mzima
nikiwa na nguo, kisha wakaniambia nitambae kwenye mchanga mpaka saa tisa usiku
ndipo nilipewa fursa ya kulala,” alisema Salim.
Alisema kuwa walikuwa watu wengi
wanaopatiwa mateso ya aina mbalimbali, ikiwemo kuchapwa viboko pamoja na
kufanyishwa kwa nguvu mazoezi ya kupiga ‘push-up’. Waliondolewa baada ya siku
tatu wakapelekwa Serengeti kwenye eneo lililotengwa kwa ajili ya kikosi hicho.
Salim alisema kuwa walipofika huko
waliendelea kuteswa, na aliomba kuonana na daktari baada ya hali yake kuzidi
kuwa mbaya kwani anakabiliwa na matatizo ya kisukari pamoja na figo iliyokuwa
ikimuuma sana kutokana na mateke aliyopigwa.
“Daktari alishauri nipatiwe dawa na
nipumzishwe, jambo lililonipa hauweni ya kutoendelea kupata mateso, maana
nilihamishiwa Kituo cha Polisi Bunda nilikokaa kwa siku nne kabla ya kufikishwa
mahakamani.
“Hata hivyo, baada ya kufikishwa
mahakamani sikusomewa shitaka lolote, bali hakimu aliniambia kuwa mahakama
inaniachia huru kwani sina kosa. Nilihoji ni kwanini nikateswa bure siku 14,”
alisema.
Kashiro ambaye naye alilalamikia
kuteswa, alisema kuwa amefunguliwa shitaka la uhujumu uchumi pamoja na Feroz.
Watatakiwa kufika mahakamani Bunda Novemba 7, mwaka huu wakati shauri lao
litakapofika kwa ajili ya kutajwa.
Operesheni Tokomeza Ujangili ilianza
rasmi Oktoba 5, mwaka huu katika hifadhi za taifa, mapori ya akiba na mbuga za
wanyama ikishirikisha Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Polisi, Usalama wa
Taifa, Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA), Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro
(NCAA) na Idara ya Wanyamapori.
Chanzo:
Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment