Tuesday, October 29, 2013

Vurugu Chadema: Mwigamba apinga kusimamishwa,Mnyika apigilia msumari hukumu hiyo



Hizi tuhuma kuwa natumiwa na Zitto nimekuwa nikizisikia, lakini huo ni upofu, mimi si mtu wa kutumika nina elimu yangu nzuri ya shahada ya kwanza ya utawala wa biashara, najua ninachokifanya ni kwa masilahi ya chama. Samson Mwigamba

Na Mussa Juma, Mwananchi

Arusha. Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba, amepinga uamuzi wa kusimamishwa  kwa maelezo kuwa kikao kilichochukua uamuzi huo hakitambuliki kikatiba huku akikanusha tuhuma za kutumiwa na Naibu Katibu Mkuu,  Zitto Kabwe, kukisambaratisha chama hicho.

Akizungumza jana na gazeti hili, Mwigamba alisema kikao ambacho kina mamlaka ya kumwajibisha ni Kamati Kuu baada ya kupokea tuhuma na kumsikiliza.
“Baraza la uongozi la Kanda halina mamlaka ya kunisimamisha uenyekiti, lakini kwa kuwa mimi bado ni mwanachama hai wa Chadema na sitahama Chadema, nitakaa pembeni ili chama kifanye uchunguzi wa tuhuma zangu nikiwa nje ya ofisi,” alisema Mwigamba.

Hata hivyo, alisema anakusudia kufafanua chanzo cha mgogoro wake na baadhi ya viongozi leo, baada ya kukabidhiwa kompyuta mpakato (laptop) na viongozi wa chama hicho ambao waliichukua ili kuifanyia uchunguzi.

Akana kutumiwa na Zitto
Akizungumzia tuhuma za muda mrefu kuwa, amekuwa akitumiwa na  Zitto hasa kuelekea uchaguzi ndani ya chama hicho, alisema  wanaofikiri hivyo ni vipofu wa kisiasa.
“Hizi tuhuma kuwa natumiwa na Zitto nimekuwa nikizisikia, lakini huo ni upofu, mimi si mtu wa kutumika nina elimu yangu nzuri ya shahada ya kwanza ya utawala wa biashara, najua ninachokifanya ni kwa masilahi ya chama,” alisema Mwigamba.

Alisema kama angekuwa mtu wa kutumiwa sasa, angetumiwa na mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe ambaye ana uwezo wa kifedha kuliko Zitto au Katibu Mkuu, Dk Willibrod Slaa ambaye atakuwa mgombea wa urais wa chama hicho na ana uwezekano wa kushinda.

Alisema kabla ya tuhuma za sasa kwamba anatumiwa na Zitto, aliwahi kutuhumiwa pia na Zitto kuwa anatuhumiwa na Mbowe hasa kutokana na misimamo yake na kauli zake katika vikao na maeneo mbalimbali, lakini baadaye ilithibitika kuwa alikuwa na hoja za msingi.

“Mimi ni mwanachama hai wa Chadema na nimekuwa nikitoa maoni yangu si kama Mwenyekiti wa Chadema Mkoa. Nina uhuru wa kutoa maoni katika kuhakikisha chama changu kinashika dola,” alisema Mwigamba.
Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Mchungaji Israel Natse alitangaza juzi kusimamishwa Mwigamba hasa kutokana na tuhuma za kukichafua chama hicho kwenye mitandao ya kijamii.

Kabla ya hatua hiyo, Mwigamba alipata kipigo kutoka kwa vijana wa Chadema  baada ya kutuhumiwa kurusha kwenye mtandao wa Jamii Forum   tuhuma za matumizi mabaya ya fedha ndani ya chama hicho akiwa ndani ya kikao cha Baraza la viongozi Kanda ya Kaskazini.

Hata hivyo, wachunguzi wa mambo wanaamini kuna uwezekano kuwa mgogoro katika chama hicho unatokana na vuguvugu la uchaguzi uliosogezwa mbele hadi mwakani.
Kuna wasiwasi huenda yakajirudia ya mwaka 2009 wakati Zitto alipojaribu kuwania nafasi ya Mwenyekiti dhidi ya Mbowe na kuzua mvutano mkubwa ndani ya chama hicho.

Hata hivyo, Zitto aliweka bayana kuwa hawezi kuzungumzia mambo hayo kwani hafahamu hata huo uchaguzi  wa ndani utafanyika lini.
Akizungumzia suala hilo, Katibu Mwenezi wa Chadema, John Mnyika alifafanua kuwa kikao kilichomsimamisha Mwigamba kilikuwa halali.
Mnyika alisema, hata hivyo, ikiwa Mwigamba hajaridhishwa  na hatua hiyo anapaswa kukata rufaa na siyo kulalamika kwenye magazeti.

Alisema kuwa Mwigamba anapaswa kusoma katiba ya chama hicho na kuelewa mambo ya chama yanamalizwa na kikao husika na siyo kwenye vyombo vya habari.
“Kikao kile kinaweza kumsimamisha ila kama hajaridhishwa na uamuzi ule basi aende kwenye ngazi inayofuata,” alisema Mnyika.

Mnyika, hata hivyo, alisema kwa ngazi ya taifa wanasubiri taarifa ya kikao kilichomsimamisha kwani walikuwa hawajapokea na  wala kutumiwa malalamiko yoyote na Mwigamba.
Chanzo: Mwananchi

No comments: