Sunday, October 27, 2013

Dokta feki, vipimo feki, dawa feki: Majanga Sekta ya Afya – 2



Wagonjwa wakiwa wamepumzika katika mazingira duni sana ndani ya moja ya zahanati za umma zilizoko maeneo ya vijijini. Wengi wako katika hatari kubwa kwani uchunguzi wa Mwananchi unaonyesha mfumo mzima wa kitabibu Tanzania umeoza, huku wagonjwa wakitumbukia katika makucha ya madaktari na wafamasia feki, wanaotoa vipimo visivyofaa, na dawa zisizokidhi viwango.

Wiki iliyopita tuliona ushuhuda wa daktari feki aliyejitambulisha kwa jina la Ramla Maganga (siyo jina lake halisi), akieleza namna alivyokuwa akihudumia wagonjwa kwenye zahanati binafasi wilayani Temeke, Dar es Salaam. Inaendelea...

Madhara yatokanayo na madaktari feki
Daktari bingwa wa upasuaji, Hospitali ya Aga Khan, Dk Aidan Njau anasema madaktari feki wanasababisha madhara makubwa kwa wagonjwa kwa kuwa wanatumia uzoefu badala ya taaluma ya matibabu.

"Hawa watu wanatoa dawa kwa mazoea, baadhi yao wamefanyakazi wodini kama manesi kwa miaka 10 hadi 20 wakiwaona madaktari wanavyotoa dawa. Wengine wamefikia hata hatua ya kuwa na vibanda vya dawa mitaani," alisema.
Anasema kwamba baadhi ya madaktari hao huwapa wagonjwa dawa chini ya kipimo kinachotakiwa, hivyo kuwafanya washindwe kupona, huku wengine wakizidisha dozi na kusababisha madhara kwenye maini na figo.

"Wanatoa dawa bila kufanya vipimo. Mgonjwa anapewa dawa ya maumivu anameza, baada ya mwezi anagundulika kuwa ana saratani. Mtu mwingine anasema anasikia maumivu tumboni anapewa dawa ya maumivu, kumbe ni Appendisitis (shambulizi la kidole tumbo) baadaye kinapasuka. Mbaya zaidi baadhi yao wanauza dawa zilizokwisha muda wake," anasema.

Maduka ya dawa yanauza dawa tofauti
Baadhi ya wauzaji wa dawa za binadamu kwenye maduka wanawauzia wateja wao dawa tofauti na zile walizoandikiwa kwenye vyeti na madaktari kwa maelezo kuwa walizonazo ni bora zaidi au ni za aina moja ila zimetengenezwa na viwanda tofauti.
Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi kwenye maduka kadhaa ya dawa muhimu, umebaini kuwa baadhi ya wauzaji kwenye maduka hayo huwalazimisha wateja wao kununua dawa tofauti ambazo hazina uwezo wa kutibu ugonjwa husika.

Mwandishi wetu alitumia cheti cha mgonjwa aliyeandikiwa dawa aina ya Clarithromycin kuzunguka kwenye maduka mbalimbali ya dawa, lakini kila alipokwenda aliuziwa dawa zenye majina tofauti huku akiambiwa kuwa zote zinatibu ugonjwa ya aina moja.
Katika duka la kwanza lililopo Mbagala Kuu, wilayani Temeke, muuzaji ambaye hakufahamika jina lake, alipoulizwa kama ana dawa ya Clarithromycin alijibu kuwa anayo. Hata hivyo, alileta dawa aina ya Erythtromycin na kumkabidhi mwandishi bila maelezo yoyote.

Alipoulizwa mbona dawa hiyo ni tofauti na ile aliyoandika daktari, muuzaji huyo alisisitiza kuwa zote zina nguvu sawa ila zimetengenezwa na kampuni tofauti.
"Dawa ya Erythtromycin ni sawa kabisa na Clarithromycin, sijui kwa nini daktari wako amesema lazima uipate hiyo hiyo," alisema muuzaji.

Mwandishi akiwa bado yupo dukani, alimpigia simu daktari aliyetaka dawa hiyo inunuliwe na kumuuliza ikiwa dawa aliyokuwa anataka kuuziwa ni sahihi kuinunua, ndipo alipoambiwa kuwa dawa hiyo ni tofauti na kwamba haifai kutibu ugonjwa uliokusudiwa.
Akifafanua daktari huyo wa Hospitali ya Aga Khan, ambaye hakutaka kutajwa gazetini kwa kuwa si msemaji wa hospitali, alisema ingawa dawa zote mbili ni aina ya antibiotics, zina nguvu tofauti katika kupambana na magonjwa na kwamba mgonjwa anatakiwa kupewa dawa kulingana na hatua ambayo ugonjwa wake umefikia.

"Hapana, usinunue dawa aina tofauti. Kama dawa niliyokuandikia haipo urudi hospitali nikuandikie dawa nyingine," alisema daktari.
Katika duka jingine lililopo nje ya hospitali ya Wilaya ya Temeke, muuzaji alipoulizwa kama ana dawa iliyokuwa ikitafutwa, alijibu kuwa anayo, lakini kama ilivyokuwa kwa muuzaji katika duka la awali alitoa dawa tofauti, mara hii Gentamycin.

Rais wa Chama Cha Wafamasia Tanzania (PST), Dk Elizabeth Shekalaghe akizungumzia suala hilo alisema watu wengi wamepata madhara kutokana na kupewa dawa zisizostahili na watu waliojiingiza kwenye tasnia ya udaktari bila ya kuwa na sifa.
"Taaluma imeingiliwa, tumeua watu wengi kwa kuwapa dawa zisizostahili. Haturuhusiwi kubadilisha jina la dawa," alisema.

Wauzaji dawa wasio na taaluma
Pia, uchunguzi wetu umebaini kuwepo kwa wauzaji wa dawa kwenye maduka hayo wasio na taaluma ya madawa. Mwandishi wetu alifika katika duka moja la kuuza dawa baridi lililopo katikati ya Jiji la Dar es Salaam, ambapo baada ya kuulizia dawa aliyokuwa anaitafuta, muuzaji alisema kuwa haipo, lakini anafahamu sehemu inakoweza kupatikana.
Aliwasiliana kwa njia ya simu na mmiliki wa duka moja la dawa baridi lililopo Mtaa wa Uhuru, Kariakoo ambapo aliambiwa asubiri kwa dakika chache ili mtu huyo aangalie kama dawa hiyo ipo. Wakati wakisubiri simu, muuzaji alitoa angalizo kuhusu wahudumu wa duka la dawa la lililotajwa.

"Naamini Clarithromycin unaweza kuipata kwa huyu jamaa pale Kariakoo, nenda kama utaipata nipigie nikuelekeze dozi sahihi inayofaa maana wale (wauzaji) nawajua pale hakuna mtaalamu wa dawa, wanaweza kukuandikia vitu vya ajabu," alisema.

Baadaye mwandishi aliambiwa aende katika duka hilo lililopo mtaa wenye maduka mengi ya dawa baridi, ambapo alifanikiwa kuipata Clarithromycin. Katika hali isiyokuwa ya kawaida; muuzaji alionekana kubabaika namna ya kuandika dozi baada ya kukosea na kufuta mara tatu, ingawa dozi sahihi ilikuwa imeandikwa kwenye cheti cha mgonjwa.
"Ahh! Samahani sikujua kama ni syrup, hii dawa ni kwa ajili ya mtoto, si ndiyo?" alimuuliza mwandishi.

Msajili wa Baraza la Wafamasia Tanzania, Mildred Kinyawa alisema kuwa baadhi ya wamiliki wa maduka ya dawa wamekuwa wakikiuka taratibu za uendeshaji wa biashara hiyo ikiwa ni pamoja na kuwa na watumishi wasiokuwa na taaluma ya dawa.
"Tatizo hilo ni kubwa, hairuhusiwi kufungua duka la dawa baridi kama huna mtaalamu," alisema na kuongeza kuwa baadhi ya wafanyabiashara wamefungua maduka ya dawa muhimu katikati ya miji huku wakijua kufanya hivyo ni kinyume cha sheria," alisema.
Muda wa matumizi ya dawa wabadilishwa

Uchunguzi wetu ulifanikiwa kubaini mbinu zinazotumiwa na baadhi ya wamiliki wa maduka ya dawa, kubadilisha muda wa matumizi uliokwisha baada ya kuona baadhi ya makopo ya kuhifadhia dawa hizo yakiwa yamefutwa muda uliokwisha na kuandikwa tarehe mpya.

Muuzaji wa duka la dawa, Leah Atukufigwewe ambaye ni muuguzi mstaafu, alisema kuwa kuna baadhi ya wauza dawa wasiowaaminifu huzifungua dawa za vidonge na kuzihifadhi kwenye makopo ambayo hayaonyeshi muda wa matumizi ijapokuwa wanajua kufanya hivyo ni kosa.

"Dawa za vidonge kama Panadol ambazo zinahifadhiwa kwenye makopo ni hatari zaidi kwa sababu hazionyeshi muda wa mwisho wa matumizi," alisema.
Akizungumzia mbinu hiyo ya kubadilisha muda wa matumizi kwenye dawa, Ofisa Uhusiano wa Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA), Gaudensia Simwanza, alisema operesheni ya kukagua dawa inayofanywa na mamlaka hiyo imewezesha kukamatwa dawa zilizobadilishwa muda wa matumizi.

Mwanzoni mwa Oktoba, serikali ikishirikiana na wadau wengine wa dawa likiwepo jeshi la polisi nchini, walifanya operesheni iliyopewa jina la Gibodia ya kukamata watu wanaojihusisha na biashara ya dawa bandia, zisizosajiliwa, zisizo na ubora na zilizoisha muda wa matumizi.
Operesheni hiyo iliyofanyika katika mikoa tisa, ilifanikisha kukamatwa kwa dawa bandia 273 zenye thamani zaidi ya Sh 49 milioni.

Watumiaji kadi za bima waongezewa dawa
Pia uchunguzi wetu umebaini kuwa kuna baadhi ya madaktari ambao humwongezea dawa mgonjwa anayetumia kadi za Bima ya Afya kwa lengo la kujipatia fedha zaidi.
Muhidini Mkamba, mkazi wa Magomeni jijini Dar es Salaam, anasema watu wanaotumia Bima za Afya wanapaswa kuwa makini, kwa kuwa baadhi ya madaktari kwenye hospitali wanawaandikia magonjwa yenye gharama kubwa kwa masilahi yao.

Anasema alimpeleka binti yake wa miezi 11 kwenye zahanati moja iliyopo karibu na nyumbani kwake, baada ya kuambiwa kuwa sehemu hiyo wanapokea Bima ya Afya.
"Manesi walimpa mtoto dawa ya homa ya tumbo, lakini baada ya muda mfupi hali yake ilianza kuwa mbaya tukaamua kumpeleka hospitali nyingine ambako walisema alikuwa na tatizo tofauti," alisema.

Tofauti za vipimo vya malaria kwenye zahanati
Pia uchunguzi wetu ulifanikiwa kubaini kuwapo kwa tofauti kubwa za vipimo vya malaria vinavyotolewa kwenye zahanati na maabara binafsi nchini.
Mwandishi wetu alipima malaria kwenye vituo vitatu tofauti jijini Dar es Salaam siku moja na kupewa majibu yaliyotofautiana. Katika zahanati ya kwanza iliyopo Mbagala Rangi Tatu wilayani Temeke, aliambiwa kuwa ana malaria moja na kuandikiwa dawa ya Malafin pamoja na dawa za kutuliza maumivu aina ya Panadol.

Pia alikwenda kupima katika zahanati moja iliyopo Tandale kwa Mtogole wilayani Kinondoni, ambako aliambiwa kuwa hana malaria badala yake alishauriwa apime Typhoid.
Chanzo:Mwananchi

No comments: