Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu
Afrika (CAF), Issa Hayatou amempongeza Jamal Malinzi kwa kuchaguliwa kuwa Rais
wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) katika uchaguzi uliofanyika
Oktoba 27 mwaka huu.
Katika salamu zake kwa niaba ya
Kamati ya Utendaji ya CAF na familia ya mpira wa miguu Afrika, Rais Hayatou
amesema uchaguzi huo unampa Rais Malinzi fursa ya kuupeleka mbele mpira wa
miguu nchini Tanzania.
Amesema CAF ina imani uwezo wake
katika uongozi, uzoefu na ujuzi katika mpira wa miguu havitausaidia mpira wa
miguu Tanzania pekee bali Afrika kwa ujumla, na kuongeza kuwa ataendeleza
ushirikiano uliopo ili kuwanufaisha zaidi vijana wa bara hili.
Rais Hayatou amemtakia Rais Malinzi
kila la kheri katika kipindi chake cha uongozi na kumhakikishia kuwa CAF iko
pamoja naye katika kusukuma mbele gurudumu la kuendeleza mpira wa miguu.
PAMBANO LA YANGA, MGAMBO SHOOTING
LAINGIZA MIL 37/-
Pambano la Ligi Kuu ya Vodacom kati
ya Yanga na Mgambo Shooting lililochezwa jana (Oktoba 29 mwaka huu) Uwanja wa
Taifa, Dar es Salaam limeingiza sh. 37,915,000.
Washabiki waliohudhuria mechi hiyo
namba 46 iliyomalizika kwa Yanga kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 walikuwa 6,515
ambapo viingilio vilikuwa sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000.
Mgawo wa mapato hayo ulikuwa kama
ifuatavyo; Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) sh. 5,783,644.07, gharama za
kuchapa tiketi sh. 3,145,790 wakati kila klabu ilipata sh. 8,550,741.95.
Wamiliki wa uwanja walipata sh.
4,347,834.89, gharama za mchezo sh. 2,608,700.93, Bodi ya Ligi sh.
2,608,700.93, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 1,304,350.47,
Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 1,014,494.81.
SIMBA, KAGERA SUGAR KUUMANA KESHO
Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) inaanza
raundi ya 12 kesho (Oktoba 31 mwaka huu kwa mechi kati ya Simba na Kagera Sugar
itakayofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10 kamili jioni.
Viingilio katika mechi hiyo
itakayooneshwa moja kwa moja na Azam Tv kupitia TBC 1 vitakuwa sh. 5,000, sh.
8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000 kwa VIP A.
Nayo Yanga itashuka uwanjani Novemba
Mosi mwaka huu katika mechi nyingine ya ligi hiyo dhidi ya JKT Ruvu
itakayochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Novemba 2 mwaka huu kutakuwa na mechi
nne; Mgambo Shooting na Coastal Union (Uwanja wa Mkwakwani, Tanga), Tanzania
Prisons na Oljoro JKT (Uwanja wa Sokoine, Mbeya), Azam na Ruvu Shooting (Azam
Complex, Dar es Salaam), na Mtibwa Sugar na Rhino Rangers (Uwanja wa Manungu,
Morogoro).
Raundi hiyo itakamilika Novemba 3
mwaka huu kwa mechi moja ambapo Mbeya City itakuwa mwenyeji wa Ashanti United
kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.
Mechi za kukamilisha mzunguko wa
kwanza wa ligi hiyo zitachezwa Novemba 6 na 7 mwaka huu. Novemba 6 ni JKT Ruvu
vs Coastal Union, Ashani United vs Simba, Kagera Sugar vs Mgambo Shooting,
Rhino Rangers vs Tanzania Prisons na Ruvu Shooting vs Mtibwa Sugar.
Novemba 7 mwaka huu, Azam itacheza na
Mbeya City wakati Yanga itacheza na Oljoro JKT kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam.
Boniface Wambura Mgoyo
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF)
No comments:
Post a Comment