HAMD Yahya Juma wa Mtibwa Sugar ndiye
Mwenyekiti wa kwanza wa Bodi ya Ligi Tanzania (Tanzania Professional League-
TPL Board) baada ya kushinda katika uchaguzi uliofanyika leo mchana (Oktoba 25
mwaka huu) kwenye ukumbi wa mikutano uliopo Golden Jubilee Tower, Dar es
Salaam. (HM)
Juma ambaye hakuwa na mpinzani
alipata kura zote kumi za ndiyo zilizopigwa na klabu za Ligi Kuu zilizohudhuria
mkutano huo. Klabu ambazo hazikuhudhuria uchaguzi huo ni JKT Ruvu, Mgambo
Shooting, Coastal Union na Rhino Rangers.
Naye Sheikh Said Muhammad Said Abeid
ambaye pia hakuwa na mpinzani amechaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti kwa kupata
kura zote za ndiyo.
Kwa upande wa wajumbe wawili wa
Kamati ya Uendeshaji, wote Kazimoto Miraji Muzo wa Pamba na Khatib Omari
Mwindadi wa Mwadui wameshinda kwa kura zilizopigwa na klabu za Ligi Daraja la
Kwanza (FDL).
Muzo alipata kura 15 za ndiyo wakati
mbili zikimkataa, huku Mwindadi akipata kura 16 na moja ilimkataa. Klabu za FDL
ambazo hazikuhudhuria uchaguzi huo ni Transit Camp, Burkina Faso, Polisi Mara,
Stand United, Toto Africans, Polisi Tabora na Kanembwa JKT. wakati huo huo,
Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) anayemaliza muda wake, Leodegar Tenga
amesema amefurahishwa na jinsi kampeni za uchaguzi zinazokwenda kutoka na
ukweli kuwa wagombea wamekuwa wakielezea kile wanachotaka kuufanyia mpira wa
miguu.
Akizungumza na Waandishi wa habari
kwenye ofisi za TFF leo mchana, Rais Tenga ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya
Utendaji ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) amesema Watanzania wanataka kusikia
ajenda za wagombea.
"Ombi langu ni kwamba kampeni
zimeanza vizuri, watu wanazungumza hoja zaidi. Ni jukumu la wajumbe kupima na kufanya
uamuzi. Kwangu mimi nimejitayarisha kumkabidhi Katiba, Rais mpya wa TFF,"
amesema.
Tenga ambaye pia ni Mwenyekiti wa
Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) amesema kazi kubwa
iliyofanywa na uongozi wake ni kujenga taasisi (TFF) pamoja na kuweka mifumo
(structure) inayoainisha majukumu ya kila mmoja.
"Ajenda yetu wakati tunaingia
madarakani mwaka 2005 ilikuwa ni kujenga taasisi. Tayari taasisi ipo, sasa
mtazamo uwe kuushughulia mpira wa miguu wenyewe," amesema.
Mkutano Mkuu wa TFF unafanyika kesho
kwenye ukumbi wa mikutano wa NSSF Waterfront, na tayari wajumbe wa mkutano huo
ambao pia utakuwa na ajenda ya uchaguzi siku inayofuata wameshawasili jijini
Dar es Salaam.
Wawakilishi kutoka Shirikisho la
Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), Ashford Mamelodi ambaye ni Ofisa Maendeleo
wa kanda hii, Magdi Shams El Din ambaye ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya CAF
na Rais wa Chama cha Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFA) ni miongoni mwa wageni
watakaohudhuria mkutano huo.
Chanzo: Boniface Wambura
No comments:
Post a Comment