Wednesday, October 30, 2013

Tishio la ugaidi, ulinzi waimarishwa bungeni



 “Hata maeneo ya umma sasa wanaimarisha usalama si hapa bungeni tu,” PICHA|MAKTABA  

Na Sharon Sauwa, Mwananchi
Dodoma. Huku kukiwa na tishio la ugaidi katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, Bunge limeimarisha ulinzi na kuongeza vifaa vya ukaguzi katika maeneo mbalimbali.
Gazeti hili lilishuhudia kuongezwa kwa mashine za usalama katika maeneo kadhaa ya jengo hilo ikiwamo lango la kuingilia utawala na wa kuingia waandishi wa habari, wageni na maofisa wa Serikali ndani ya Kumbi za Bunge.

Pia maaskari wa Bunge, wameonekana kuwa makini zaidi tofauti na nyakati za nyuma ambapo sasa watu wasiokuwa na vitambulisho wamekuwa wakikumbana na maswali mengi. Aidha, watu wanaobeba maji ya kunywa na kuingia katika viwanja na jengo la utawala wamekuwa wakilazimika kuyanywa kwanza. kabla ya maofisa usalama kuwaruhusu kuingia nayo ndani.

Akizungumzia hali hiyo jana, Mkurugenzi wa Idara ya Habari na Ushirikiano wa Kimataifa wa Bunge, Jossey Mwakasyuka, alisema ni shughuli ya kawaida inayolenga kuiboresha ofisi hiyo Bunge. “Suala la kuimarisha usalama hatujaanza leo, tunafanya hatua kwa hatua, ni suala muhimu kufanyika huwezi kujua mahali ambapo(magaidi),wanaweza kuingia:

“Hata maeneo ya umma sasa wanaimarisha usalama si hapa bungeni tu,” alisema Mwakasyuka.
Septemba mwaka huu, Bunge liliandaa semina kwa ajili ya maaskari wote wanaolinda usalama katika chombo hicho.

No comments: