na Mwandishi wetu
SIKU mbili baada ya Rais Jakaya
Kikwete kutoa kauli ya kuhofia chama chake kuondoka madarakani iwapo rushwa
itashindwa kutokomezwa, Waziri Mkuu mstaafu Frederick Sumaye amemtaka kiongozi
huyo kuchukua hatua.
Akizungumza na Tanzania Daima
Jumapili jana, Sumaye alisema kuwa wala rushwa wanajulikana, lakini wameshindwa
kuchukuliwa hatua.
Sumaye alisema kuwa anashukuru Rais
Kikwete kubaini tatizo hilo na kumshauri kwenda mbali zaidi, ikiwa ni pamoja na
kulifanyia kazi na kuwachukulia hatua watu hao.
“Kama rais naye amegundua hilo, basi
ni vizuri zaidi, ayafanyie kazi hayo. Msimamo wangu unajulikana,
nimeshalalamika sana kuhusu rushwa, najua rushwa inakwamisha maendeleo,
tuchukie rushwa, tutafute nafuu ya maisha kwa Watanzania wote, sio nafuu ya mtu
mmoja mmoja,” alisema.
Alipoulizwa na gazeti hili kama
anawajua wala rushwa na hatua ambazo anamshauri rais achukue, Sumaye alisema
kuwa watu hao wanajulikana na wameshawahi kuandikwa, hivyo hana haja ya
kuwataja.
“Wanajulikana, kama na ninyi
mmeshawaandika basi wanajulikana, sina haja ya kuwataja,” alisema.
Waziri Mkuu huyo mstaafu, mwaka jana
alilalamikia rushwa baada ya kuenguliwa katika kuwania ujumbe wa NEC katika
Wilaya ya Hanang ambako Mary Nagu aliibuka kidedea.
Siku za hivi karibuni, Sumaye
alikaririwa akisema wanaokerwa na karipio lake kuhusu rushwa, wanapaswa
kuachana na vitendo hivyo viovu.
Sumaye, alitoa karipio hilo kwa
viongozi wa dini, hususani ndani ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania
(KKKT), akionya kuhusu kasi ya wanasiasa kutumika katika harambee zake.
Alikaririwa akisema miongoni mwa
wanasiasa hao, wanatumia mwanya huo kama njia ya kuungwa mkono watakapotangaza
kuwania urais katika uchaguzi mkuu ujao.
Ingawa hakuwataja wanasiasa hao kwa
majina, kauli yake ilitafsiriwa kumgusa aliyekuwa mrithi wake, Edward Lowassa,
ambaye baadaye alijiuzulu kufuatia kashfa ya Richmond.
Lowassa, mbunge wa Monduli,
ameshiriki harambee mbalimbali nchini, hali inayoelezwa na baadhi ya wachunguzi
wa mambo ya siasa kuwa na lengo la kujisafishia njia kuelekea katika
kinyang’anyiro cha urais wa 2015.
Lakini Lowassa amekanusha kushiriki
harambee hizo kwa nia ya kutafuta urais, badala yake akasisitiza kwamba ana
karama ya ushawishi inayomfanya afanikishe shughuli hizo kwa kupata fedha
nyingi.
Naye aliyekuwa Waziri wa Nishati na
Madini, Wiliam Ngeleja, alisema anamuunga mkono Rais Kikwete kwa kuwa rushwa
imeumiza taifa, imepoteza rasilimali nyingi, na ufisadi mkubwa umepitia hatua
iliyosababisha maendeleo kurudi nyuma.
“Suala la rushwa linaaibisha taifa
letu, tusilitazame kama suala la Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa,
tulitazame kama suala la Watanzania wote, tuchukie rushwa, rushwa itazamwe kwa
mapana yake, na kila Mtanzania ajue madhara ya rushwa, hapa ndiyo tutasaidia
taifa,” alisema.
Alisema kuwa kama rushwa itaendelea
kushamiri, haki za wananchi zitaminywa, huduma za muhimu hazitapatikana kwa
njia ya haki, hivyo wananchi wataendelea kuteseka na kukosa huduma hali ambayo
inasababisha watu kuichukia CCM na serikali yake.
Ngeleja alisema kuwa anamuunga mkono
Rais Kikwete kwa kauli yake, na kuwataka Watanzania wazidishe mapambano dhidi
ya rushwa, na wenye ushahidi kwa watuhumiwa wa rushwa wajitokeze ili kuisaidia
Takukuru ifanye kazi yake ipasavyo.
Aidha, mhadhiri wa zamani wa Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Azavel Lwaitama alisema Rais Kikwete anaonekana
sasa kuwa na nia nzuri na taifa, hivyo alimuomba Mungu amsamehe makosa ya
zamani, kwa kuwa msimamo wake wa sasa unaitesa CCM.
“Kauli ya Kikwete ya sasa imenifanya
nifikirie uamuzi wa kuendelea kulipia kadi yangu ya CCM, kwani niliacha tangu
2005, baada ya kuona chama kinaendeshwa kwa rushwa. Mimi ninampongeza kwanza
kwa kukiri yale ambayo yalitufanya tuache kulipia kadi, sasa tunamhimiza
afikirie zawadi ya MO Ibrahim, asimamie upatikanaji wa katiba mpya kwa njia ya
haki na kusikiliza maoni ya wapinzani, atusaidie kusimamia uchaguzi wa mwaka
2015 bila rushwa, hayo yataandika historia nzuri ya jina lake na atakumbukwa
kwa msimamo huu,” alisema.
Chanzo: Tanzania daima
No comments:
Post a Comment