Serikali ya Israel imewaachilia
wafungwa 26 wa Palestina kama sehemu ya makubaliano ya kuanza tena mazungumzo
ya amani kati ya pande hizo mbili.
Wafungwa watano, waliachiliwa katika
Ukanda wa Gaza wakati wengine 21 wakipelekwa katika Ukingo wa Magharibi.
Wale walioachiliwa walikuwa
wamehukumiwa kwa kosa la mauaji na walikuwa wameishi jela kwa kati ya miaka 19
na 28 .
Maafisa wa Israel na Palestina
walianza tena mazungumzo mjini Jerusalem mnamo mwezi Agosti, baada ya miaka
mitatu ya kutatizika kwa mazungumzo hayo ya amani.
Kwa mujibu wa mwandishi wa BBC katika
Ukingo wa magharibi,Yolande Knell wale walioachiliwa wanaonekana kama wafungwa
wa kisiasa na mashujaa wa harakati za ukombozi wa wapalestina , lakini uamuzi
wa kuwaachilia wafungwa hao haujawafurahisha wengi nchini Israel.
Wapalestina walioachiliwa mapema
Jumatano, walitolewa kutoka jela la Ofer na kupelekwa katika kivukio cha Erez
kuingia Gaza na katika kivukio kingine cha Beituna kuingia Ukingi wa Magharibi.
Katika Ukanda wa Gaza watu walipiga
baruti huku waliokuwa wafungwa hao wakiingia Palestina kwa msururu wa magari.
Kwenye Ukingo wa Magharibi,
walipelekwa katika eneo la Ramallah ambako Rais wa Palestina alikuwa anahutubia
umati mkubwa wa watu.
Abbas alisema kuwa wafungwa wengine
wataachiliwa katika kipindi cha miezi miwili, na kutoa wito wa kuachiliwa huru
kwa wapalestina wote waliofungwa.
"Hapatakuwa na makubaliano ya
mwisho bila ya kuachiliwa kwa wafungwa wote wa Palestina,’’ alisema Rais Abbas.
Pia alikanusha tetesi kuwa
makubaliano ya kauchiliwa kwa wafungwa yaliafikiwa baada ya Israel kuruhisiwa
kujenga makaazi zaidi ya walowezi katika eneo hilo.
Hatua ya kuachiliwa kwa wafungwa
imesababisha mgawanyiko katika muungano tawala nchini Israel, huku vyama vyenye
msimamo mkali vikitaka kuzuia shughuli hiyo kuendelea.
No comments:
Post a Comment