Makamu
wa Rais Dk. Mohammed Gharib Bilal akikagua ujenzi wa nyumba 851 kwa ajili ya
kuuzia wafanyakazi wa serikali baada a kuweka jiwe la msingi jana katika
eneo la Mabwe Pande Jijini la Dar es Salaam. . Kulia ni Waziri wa Ujenzi, Dk.
John Magufuli. Picha na Salim Shao.
Na Aidan Mhando, Mwananchi
Dar es Salaam. Waziri wa Ujenzi, Dk
John Magufuli ametoa mwezi mmoja kwa watumishi wa Serikali ambao wanadaiwa
mikopo ya nyumba kulipa madeni yao mara moja na kuonya kwamba ikiwa watashindwa
kulipa, watanyang’anywa nyumba hizo na watakopeshwa watu wengine.
Dk Magufuli ameibuka na hoja hiyo
mpya, zikiwa ni siku chache tangu alipopigwa ‘stop’ na Waziri Mkuu, Mizengo
Pinda kutekeleza sheria ya kuondoa msamaha wa asilimia tano kwa mizigo
inayozidi kwenye malori, hali ambayo ilizusha mvutano mkubwa baina ya Serikali
na wasafirishaji wa mizigo nchini.
Akizungumza wakati wa kuweka jiwe la
msingi kuzindua ujenzi wa nyumba 851 za watumishi wa Serikali eneo la
Mabwepande jijini Dar es Salaam, Dk Magufuli alisema watumishi 2500 hawajalipa
mikopo ya nyumba walizonunua.
Dk Magufuli alionya kuwa atafuatilia
suala hilo na kuhakikisha madeni hayo yanalipwa mara moja, huku akimwomba
Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal kumuunga mkono kwenye jambo hilo,
ambalo ni utekelezaji wa sheria za nchi.
“Naomba ifahamike kwamba tunapojenga
nyumba kwa ajili ya kuwakopesha watumishi wa umma tunataka kuboresha makazi
yao. Pia fedha tunazokusanya zinasaidia kujenga nyumba zaidi,” alisema Dk
Magufuli. Hata hivyo alisema hadi sasa watumishi wa Serikali 4,900 ambao
walikopa nyumba hizo tayari wamelipa madeni.
“Mimi nafanya kazi kwa kufuata sheria
na kila mtumishi wa Serikali anafahamu jambo hilo, hivyo watu ambao wanajua
tunawadai wakae kwa tahadhari, kwani ndani ya mwezi mmoja kama hawatalipa
tutawachukulia hatua bila kupuuzia,” alionya Magufuli.
Hii siyo mara ya kwanza kwa Dk
Magufuli kutangaza kunyang’anya nyumba hizo, kwani alifanya hivyo mwishoni mwa
Machi mwaka jana pale alipouagiza uongozi wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA),
kuwapa siku saba watu wote walionunua nyumba hizo kulipa madeni yao.
Dk Magufuli aliwataka TBA kutoa ilani
ya maandishi inayowataka wahusika walipe fedha hizo ndani ya wiki moja
vinginevyo wangenyang’anywa kwa maelezo kwamba wanachelewesha malengo ya TBA
kujenga nyumba zaidi. Hata hivyo, hakuna taarifa zozote zilizowahi kutolewa
kuhusu kutekelezwa kwa amri hiyo iliyotolewa zaidi ya miezi 18 iliyopita.
Jana, Makamu wa Rais, Dk Bilal
alimuunga mkono Magufuli akisema: “Naunga mkono tamko la Waziri wa Ujenzi
kwamba ni lazima watumishi wa Serikali ambao wanakopeshwa nyumba walipe haraka
ili fedha hizo zisaidie kujenga nyumba nyingine.”
Dk Bilal alikuwa mgeni rasmi katika
shughuli ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa nyumba 851, kwenye eneo la Bunju
‘B’ Kinondoni, Dar es Salaam. Ofisa Mtendaji Mkuu wa TBA, Elius Mwakalinga,
alisema ujenzi huo unafanyika kwa awamu mbili ambapo awamu ya kwanza iligharimu
Sh2 bilioni na awamu ya pili Sh1 bilioni.
“Nyumba 851 zinazojengwa Bunju B ni
sehemu ya ujenzi wa nyumba 4,400 katika Mkoa wa Dar es Salaam na nyumba 10,000
kwa nchi nzima,” alisema Mwakalinga.
Hafla hiyo ilisimama takriban kwa
dakika 10 wakati Dk Bilal akitaka kuhutubia baada ya jenereta kushindwa kufanya
kazi, hivyo kumlazimu kurudi kuketi kwenye kiti hadi umeme uliporejea. Mkuu wa
Wilaya ya Kinondoni, Jordan Rugimbana alilazimika kwenda kufuatilia suala hilo
na mafundi waliokuwapo walifanikiwa kuunganisha mashine za kipaza sauti na
umeme wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), hivyo Makamu wa Rais aliendelea
kuhutubia.
Uuzaji wa nyumba
Nyumba nyingi za Serikali zilijengwa
kipindi cha utawala wa ukoloni wa Wajerumani uliodumu kati ya 1885 na 1919 na
ule wa Waingereza ulioanza 1919 hadi 1961.
Taarifa zilizopo zinaonyesha kuwa
nyumba za Serikali zilizouzwa nchi nzima tangu mwaka 2002 wakati wa uongozi wa
awamu ya tatu chini ya Rais Benjamin Mkapa ni zaidi ya 6,000. Malengo ya kuuza
nyumba ni kwamba, fedha zilizopatikana zingetumika kujenga nyumba nyingine kwa
ajili ya watumishi wa Serikali katika maeneo mbalimbali nchini yakiwamo Dar es
Salaam, Arusha, Dodoma na Mwanza.
Hata hivyo, uuzaji huo ulikuwa na
utata hali iliyosababisha kupingwa vikali na watu wa kada mbalimbali wakiwamo
wanasiasa na wanaharakati, kwa maelezo kwamba uliwanufaisha vigogo.
Malalamiko pia yalijengwa kwenye hoja
kwamba nyumba hizo ziliuzwa kwa bei ndogo ambayo haikuzingatia thamani ya ardhi
husika, huku wengine wakisema hakukuwa na umakini kwani viongozi wengi walikosa
makazi na hasa wale walioteuliwa baada ya Rais Jakaya Kikwete kuingia
madarakani.
Miongoni mwa walionunua nyumba hizo
ni mawaziri wengi, kama si wote, wakati wa Serikali ya Awamu ya Tatu, hasa
katika mikoa ya Dar es Salaam na Dodoma, kwa kuwa walikuwa wakiishi katika
nyumba hizo.
Hali hiyo ilisababisha viongozi
mbalimbali wakiwamo mawaziri, majaji, wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya,
wakurugenzi wa ngazi mbalimbali na viongozi wengine kukaa hotelini na
kuisababishia Serikali gharama kubwa.
Tatizo lingine lililoibuka ni kuwa
baadhi ya nyumba zilizouzwa zilikuwa ndani ya maeneo ya jeshi na hasa Polisi,
hivyo kuilazimisha Serikali ya awamu ya nne ilipoingia madarakani kulazimisha
kurejesha baadhi ya nyumba hizo.
Hata hivyo, kulikuwa na ugumu katika
urejeshaji kwani baadhi ya waliouziwa tayari walikuwa wamezibomoa na kuanza
upya ujenzi wake na wengine walikuwa tayari wamezipangisha kwa mabalozi,
kampuni binafsi, mashirika yasiyokuwa ya kiserikali (NGOs) na nyingine
kujengewa maduka ya biashara.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment