Mfalme Abdullah akiwa na Rais Obama
Saudi
Arabia imetahadharisha kwamba uhusiano kati yake na Marekani unaweza ukaingia
dosari kutokana na jinsi Marekani inavyoendesha sera zake katika kushughulikia
mzozo wa Syria na mpango wa nyuklia wa Iran.
Taarifa hiyo imetolewa na mkuu wa
ujasusi wa Saudi Arabia, Mwanamfalme Bandar bin Sultan, ambaye ameahidi kuwa
nchi yake itabadilisha mtazamo wake na kufanya mageuzi makubwa katika uhusiano
na Marekani ikiwa ni katika kupinga jinsi Marekani inavyoshughulikia vita vya
wenyewe kwa wenyewe vya Syria na Iran.
Duru za karibu na sera za Saudi
Arabia, zimeeleza kuwa Bandar amewaambia wanadiplomasia wa Ulaya kwamba
Marekani imeshindwa kuchukua hatua madhubuti dhidi ya Rais Bashar al-Assad wa
Syria na mpango wa nyuklia wa Iran.
Marekani yashindwa kuiunga mkono
Saudi Arabia
Amesema Marekani pia ilishindwa
kuiunga mkono Saudi Arabia ilipokuwa upande wa Bahrain wakati ilipopambana na
raia wanaoipinga serikali katika vuguvugu la mwaka 2011.
Amesema mageuzi hayo kwa Marekani
yatakuwa makubwa na kwamba Saudi Arabia haitaki kujikuta katika hali ya kuwa
tegemezi.
Mwanamfalme Turki Al Faisal
Hata hivyo, haikufahamika wazi iwapo
matamshi hayo ya Mwanamfalme Bandar, aliyekuwa balozi wa Saudi Arabia nchini
Marekani kwa miaka 22, yanaungwa mkono na Mfalme Abdullah.
Mvutano huo kati ya nchi hizo mbili
pia umegonga vichwa vya habari vya Marekani, ambako mwanamfalme mwingine
mwandamizi wa Saudi Arabia, amekosoa sera za Rais Barack Obama za Mashariki ya
Kati, akimtuhumu kwa kukwamisha amani ya Syria na Israel na Palestina.
Mwanamfalme Turki al-Faisal, amesema
sera za Obama kuhusu Syria zinasikitisha na ameukejeli mpango wa Urusi wa
kutokomeza silaha za sumu za Assad.
Dalili zilianza mapema
Saudi Arabia ilianza kuonyesha dalili
za kutoridhishwa na sera za Obama wiki iliyopita, baada ya kukataa kuchukua
wadhifa wa kuwa mwanachama mpya asiyekuwa na kiti cha kudumu kwenye Baraza la
Usalama la Umoja wa Mataifa, katika kile ilichoeleza ni kukasirishwa baada ya
jumuiya ya kimataifa kushindwa kumaliza vita vya Syria na kushughulikia masuala
mengine ya Mashariki ya Kati.
John Kerry na Saud al-Faisal
Katika mkutano wa jana Jumanne wa
marafiki wa Syria uliofanyika London, Uingereza, Waziri wa Mambo ya Nje wa
Marekani, John Kerry amesema atayazungumzia matamshi hayo ya Saudi Arabia
atakapokutana na waziri mwenzake wa Saudi Arabia, Saud al-Faisal mjini Paris,
Ufaransa Jumatatu ijayo.
Marekani na Saudi Arabia zimekuwa
washirika tangu taifa hilo la Kifalme lilipotangazwa mwaka 1932, huku Saudi
Arabia ikipewa usimamizi wa nguvu za kijeshi na Marekani ikihakikishiwaa
usambazaji wa mafuta. Ukosoaji huo wa Saudi Arabia umetokea siku chache baada
ya kuadhimisha miaka 40 ya vikwazo vya mafuta vya nchi za kiarabu Oktoba mwaka
1973, vilivyowekwa kuziadhibu nchi za Magharibi kwa kuiunga mkono Israel katika
vita vya Yom Kippur.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/RTRE
Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman
Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman
No comments:
Post a Comment