Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete akiwahutubia
wanachama wa chama hicho kwenye moja ya mikutano, Kilosa mjini mkoani Morogoro.
Picha ya Maktaba
Na Sharon
Sauwa na Habel Chidawali, Mwananchi
Dodoma. Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais
Jakaya Kikwete amesema kama rushwa haitakomeshwa ndani ya chama hicho, katika
uchaguzi mkuu utakaofanyika mwaka 2015 kitaanguka vibaya na iwapo kitanusurika
hakitapita kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.
Katika hatua nyingine, Rais Kikwete
amempa jukumu la kushughulikia viongozi wa CCM wanaokula rushwa, Makamu
Mwenyekiti wa CCM, Philipo Mangula.
Rais Kikwete, alitoa onyo hilo juzi
usiku, alipokuwa akifunga mafunzo maalumu ya siku nne kwa makatibu wa mikoa,
makatibu na wenyeviti wa wilaya wa chama hicho nchini.
“Kama hatutabadilika katika suala la
rushwa mwaka 2015 tutakuwa na wakati mgumu sana na kama mwaka huo tutafanikiwa
kuishika Serikali, basi mwaka 2020 hatutarudi tena madarakani.
“Najua rushwa ipo na mnaendelea
kupokea shilingi laki mbili za airtime (muda wa mawasiliano), ndugu zangu
hatutafika ama wengine watavuka na wengine kukwama,” alisema Mwenyekiti wa CCM,
Rais Kikwete.
Hii ni kauli ya kwanza nzito ya Rais
Kikwete ya hivi karibuni ya kukionya chama hicho kuhusu uimara wake wa
kuendelea kushika dola.
Aliendelea kusema kuwa tatizo la
rushwa kwa viongozi wa chama hicho linazidi kuwa kubwa kila siku, hali ambayo
inawapotezea imani wananchi ambao ndio wapiga kura wao.
“Viongozi wa chama ndio mmekuwa
mawakala wa kusambaza rushwa bila hata aibu. Nawaombeni tubadilike, kama
tutaendelea hivi hali yetu itakuwa ngumu sana katika chaguzi mbalimbali,
nawaambieni,” alisema Rais Kikwete ambaye alitumia muda wa saa mbili kufunga
mafunzo hayo.
Aliwaambia kuwa siku hizi watu wana
mbadala wa vyama vingine na siyo CCM peke yao.
Aidha, Rais Kikwete alisema viongozi
ambao wanajihusisha na vitendo vya rushwa waondolewe mara moja katika nafasi
zao, ili kuwaweka watu watakaokisaidia chama kupata mafanikio.
“Tuna vijana wengi kutoka katika vyuo
mbalimbali ambao wanaweza kufanya kazi kwa uadilifu wa hali ya juu, hivyo
hatuna budi kuachana na hawa wala rushwa ambao watatupotezea sifa yetu kwa
wananchi.
“Tukipoteza urais ndiyo tumekwisha na
chama kinaweza kufa.”
Aidha, aliwaonya viongozi ambao
wanajihusisha na uuzaji wa mali za chama kama vile viwanja na baadhi yao
kuingia mikataba yenye utata.
“Kuna watu wanapoingia mikataba sijui
wanakuwa wamelewa...kwanza unashindwa hata kuelewa...kwa mfano utakuta mtu
alipangishwa jengo la CCM kwa miaka 264 sasa unawaza huu mkataba wa aina gani
kwa sisi tuliopo hapa, miaka 50 ijayo hakuna atakayekuwapo duniani, sasa
mmiliki wa lile jengo atakuwa nani?” alisema.
Hata hivyo, aliwataka makatibu hao na
wenyeviti wa wilaya na mikoa kuhakikisha wanawatembelea wanachama wao na
kutafuta wanachama wapya kwa ajili ya kujiimarisha kwa chaguzi mbalimbali
zijazo.
“Viongozi wengi hatuna tabia ya
kuwatembelea wanachama wetu na kuwatatulia kero zao, hali ambayo inatugharimu
wakati wa uchaguzi kupata kura kidogo tofauti na idadi ya wanachama tulionao,”
alisema na kuongeza:
“Wenzenu wakiendelea kutembelea
wanachama na kuitisha mikutano, nyie mnabakia kuimba wembe ni uleule ushindi,
shauri yenu mtakatwa,” alisema.
Alisema wapinzani wana rekodi ya
kufanya vizuri kwa kufanya mikutano kuliko viongozi wa CCM.
Aidha, alisema iwapo hawatafanya kazi
vizuri chama hakitaweza kufanikiwa na kuwataka kutumia maarifa waliyopata
katika mafunzo hayo kuhakikisha chama kinakuwa imara na chenye uwezo wa
kuongoza. “Lazima muendelee kuongeza wanachama siyo kupanda majukwaani na
kuimba iyena iyena...Utendaji mpya wa kuongeza wanachama ni kuwatambua na kuwapa
majukumu,” alisema.
Alisema chama hicho kina udhaifu wa
kuwashawishi watu kujiandikisha katika daftari la kudumu na kwenda kupiga kura.
“Kama ni udhaifu katika chama chetu
ni huu kwani tuna wanachama, lakini wakati wa kwenda kupiga kura hatuwafuatilii
ni vyema suala hili nyie viongozi muanze nalo sasa.”
Peter Kisumu
Hivi karibuni mwanasiasa na kada
mkongwe wa CCM, Peter Kisumo naye alionya kuwa chama hicho kinaweza kuondolewa
madarakani kutokana na kunyamazia vitendo vya ufisadi na matumizi mabaya ya
rasilimali za umma vinavyotokea nchini.
Mzee Kisumo alitoa onyo hilo wiki iliyopita katika
mazungumzo maalumu aliyofanya na gazeti hili nyumbani kwake Dar es Salaam
kuhusu kumbukumbu ya Miaka 14 ya Kifo cha Mwalimu Julius Nyerere.
Alisema tatizo kubwa la chama hicho ni kwamba kimeendelea
kuwa chama dola kikikaa mbali na wananchi, huku kikishindwa kuidhibiti rushwa
na kuwawajibisha wahusika wa vitendo hivyo.
“Chama kimebaki kuwa cha walalamikaji, kila mtu amekuwa
mlalamikaji. Hata Waziri Mkuu amegeuka mlalamikaji. Sijaona watu
wanaowajibishwa kwa ufisadi,” alisema Kisumo na kuongeza:
“CCM haiwezi kujivunia ufisadi unaoonekana nchini. Siwezi
kusema imeukumbatia, lakini nasema imekuwa CCM bubu, hata kuukemea ufisadi
haiwezi. Utamaduni huu enzi za Mwalimu Nyerere haukuwapo.”
Alisema kutokana na udhaifu huo wa CCM, kuna uwezekano
mkubwa wa chama cha upinzani, na hasa Chadema kutumia mwanya huo kuwashawishi
wananchi na kushinda uchaguzi.
Kisumo ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa
CCM, alisema ingawa Chadema haijaonyesha wazi mambo kinayoyapigania, kinaweza
kutumia agenda ya ufisadi na matumizi mabaya ya rasilimali za umma kuwavutia
wananchi na kuchaguliwa.
Chanzo:
Mwananchi
No comments:
Post a Comment