• CHADEMA yadai kompyuta
yake ina siri zitakazogusa wengi
na Grace Macha, Arusha
MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (CHADEMA) Mkoa wa Arusha ambaye amesimamishwa uongozi kwa tuhuma za
usaliti, Samson Mwigamba, amesema kuwa hakupigana na Mwenyekiti wa Taifa wa
chama hicho, Freeman Mbowe, kama ilivyodaiwa na baadhi ya magazeti.
Mwigamba alitoa kauli hiyo jana
wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa kuelezea kile kilichojiri
mwishoni mwa wiki hadi akapigwa na baadhi ya wajumbe wa kikao, wakimtuhumu
kwamba aliandika taarifa za uongo kwenye mtandao wa kijamii wa Jamii Forums
akizungumzia masuala ya uongozi ndani ya chama.
Mwigamba alisema kuwa hata wakati
akivutana na walinzi wa chama Mbowe hakuwa ndani ya chumba cha mkutano, hivyo
akadai kuwa anashangazwa na wale waliosambaza taarifa hizo kwamba alipigana na
kiongozi huyo ambaye pia ni Mbunge wa Hai na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni.
Aliwataja wale aliodai walimpiga kuwa
ni Katibu wa Bavicha Wilaya ya Arusha, Noel OLovaroya, walinzi wa chama pamoja
na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, kwamba alijaribu bila mafanikio
kumpiga na kitofali ambapo alikikwepa kwa kujiangusha chini na kujigonga
kisogoni.
“Wakati vurugu zikianza Mbowe hakuwa
ukumbini, nilimuona akija Lema na Olevaroya, ambapo Lema alishikwa kabla
hajanifikia huku Olevaroya akiruka juu ya meza na kuja kunipiga ngumi, mimi kwa
kujitetea ilibidi nimpige ngumi kabla hatujaamuliwa,” alisema.
Mwigamba alimtuhumu Lema kuwa amekuwa
akimtishia kumuua kwa kipindi kirefu, ambapo siku ya tukio alirudia kauli hiyo
kabla hajaenda kuchukua kitofali na kujaribu kumpiga nacho ambapo alikikwepa.
Alisema kuwa tayari alishatoa taarifa
polisi na kupewa kumbukumbu: AR/RB/1759/2013 aliyoifungua Februari 12, mwaka
huu, baada ya kuwa anapokea vitisho vya kuuawa kutoka kwa Lema kupitia simu
yake ya kiganjani.
Kuhusu kusimamishwa uongozi, Mwigamba
alisema kuwa ametii licha ya kuwa kikao kilichomsimamisha hakina mamlaka
kisheria, huku akiweka wazi kuwa hayuko tayari kukihama chama hicho, kwani bado
anaamini ndicho chenye uwezo wa kuleta mabadiliko nchini.
Hata hivyo, tuhuma za Mwigamba
zilikanushwa na Katibu wa CHADEMA wa mkoa, Amani Golugwa, akisema ni uongo
dhidi ya Lema, kwani kwenye taarifa yake aliyowasilisha juzi kwenye kikao cha
uongozi wa kanda alimsifu mbunge huyo kwamba ameongoza harakati mbalimbali za
ujenzi wa chama kwa mafanikio makubwa, zikiwamo kampeni za ushindi wa kata nne
zilizofanya uchaguzi mdogo hivi karibuni.
“Kwa kipindi chote ambacho amekuwa
hayuko kazini Lema amekuwa akimsaidia hata kukamilisha ujenzi wa nyumba yake
maeneo ya Sokon 1, hata anavyokwenda kwenye kesi zake Dar es Salaam ni Lema
amekuwa akimsaidia gharama.
“Hicho alichokizungumza kwenye
mkutano wake juu ya malalamiko ndiyo anatudhihirishia kuwa amekuwa nyoka na
mnafiki ndani ya kundi letu,” alifafanua katibu huyo huku akisema hakuna
malalamiko yoyote juu ya suala hilo ndani ya chama.
Golugwa aliongeza kuwa baada ya
kupitia kompyuta ya Mwigamba wamebaini mambo mengi machafu na ya hatari kwa
mustakabali wa chama ambayo yanawagusa watu wengi.
Hata hivyo hakutaka kuingia kwa
undani wala kuyafafanua akisema yatakisaidia chama katika uchunguzi wake zaidi,
na kwamba tayari kikao cha Baraza la mkoa kimeshakaa na kimemwandikia Mwigamba
barua ya ajieleze ni kwa nini asivuliwe uongozi ikiwa ni sehemu ya mchakato wa
kulifikisha suala hilo mbele ya kikao cha Kamati Kuu ya Taifa.
Chanzo:
Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment