Mwasisi
wa Chadema Edwin Mtei (mwenye kofia) akizungumza kwenye mkutano wa siku tatu wa
Baraza la Kanda ya Kaskazini ya chama hicho jijini Arusha juzi. Wapili kushoto
ni Mwenyekiti wa Kanda Mchungaji Israel Natse, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman
Mbowe na Katibu wa Kanda, Amani Golugwa. PICHA | FILBERT RWEYEMAMU
Na Mussa
Juma na Peter Saramba, Mwananchi
Arusha. Mkutano wa Baraza la Uongozi la
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya Kaskazini juzi uligeuka
ukumbi wa ngumi, baada ya Mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Arusha, Samson
Mwigamba kushushiwa kipigo.
Mwigamba alishushiwa kipigo hicho na
baadhi ya viongozi wenzake wa chama kwa madai ya usaliti na tayari
amesimamishwa uongozi kwa muda usiojulikana.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha,
Liberatus Sabas jana alithibitisha kutokea kwa vurugu hizo na viongozi hao wa
Chadema kufikishana polisi.
Alikutwa na zahama hiyo mbele ya
viongozi wakuu wa Chadema Taifa, Mwenyekiti, Freeman Mbowe na mwasisi wa chama
hicho, Edwin Mtei katika Hoteli ya Coridal Spring.
Viongozi hao wamekuwa wakifanya ziara
za aina hiyo nchi nzima, kuimarisha chama na kujipanga kwa ajili ya uchaguzi wa
Serikali za Mitaa mwakani na uchaguzi mkuu ujao wa Rais na wabunge mwaka 2015.
Habari kutoka ndani ya mkutano huo
zinaeleza kuwa hatua hiyo ilifuatia tuhuma kwamba Mwigamba alituma ujumbe
kwenye mtandao wa kijamii wa Jamii Forums, unaodaiwa kukichafua chama hicho.
Tukio hilo la aina yake lilitokea
wakati viongozi wote wa juu wa chama hicho, wakiongozwa na Mbowe walipokuwa
wakijadili mustakabali wa chama hicho, mkutano ambao ulihudhuriwa na wabunge
karibu wote wa Chadema wa kanda hiyo.
Hata hivyo, wakati mijadala
ikiendelea baadhi ya viongozi wa chama hicho, akiwamo Mbunge wa Jimbo la Arusha
Mjini, Godbless Lema walimtuhumu Mwigamba kutuma ujumbe kwenye mtandao huo,
uliokuwa ukizungumzia ufisadi ndani ya chama hicho, wakidai alitaka Mwenyekiti
Mbowe kukubali kuchunguzwa.
Akizungumza na Mwananchi Jumapili
jana, Mwigamba alisema kuwa baada ya Lema kutoa tuhuma hizo aliungwa mkono na
viongozi wengine na vijana waliokuwa wameimarisha ulinzi, kumvamia na kuanza
kumpiga pamoja na kumnyang’anya kwa nguvu kompyuta mpakato (Laptop), aliyokuwa
nayo, kisha kumpeleka Kituo Kikuu cha Polisi, mjini Arusha.
“Wamenipiga sana na kuniweka ndani,
ila nashukuru Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Arusha (OCCID), alikuja na
kunitoa saa 5:00 asubuhi,” alisema Mwigamba.
Alisema kuwa leo katika mkutano wake
na waandishi wa habari ataeleza yote yaliyotokea na hatua atakazochukua,
kwa kuwa yeye ni kiongozi wa juu wa chama.
Hata hivyo, alieleza kwamba bado
anashauriana na wanasheria wake kuona kama anaweza kuwachukulia hatua
waliompinga.
Kauli ya polisi
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha,
Liberatus Sabas alisema polisi wameona hakuna kosa la kisheria lililotokea hasa
kutokana na malalamiko yaliyofikishwa kwao dhidi ya Mwigamba ya kukichafua
chama kwenye mitandao.
“Hili suala la mitandao ni kubwa na
lina taratibu zake sasa kusema tu umechafuliwa na iwe kesi nadhani uchunguzi
unahitajika kwao, sisi tumeona haya ni mambo yao wanaweza kuyamaliza wao ndiyo
sababu tulimwachia, Mwigamba,” alisema Sabas.
Kosa analodaiwa kufanya Mwigamba
Akizungumzia sakata hilo jana, Mbunge
wa Arusha Mjini, Godbless Lema alisema kwamba Mwigamba alibainika kutuma
ujumbe kwenye mtandao wa Jamii Forums uliokichafua chama hicho, akieleza
haikuwa mara yake ya kwanza kwa kiongozi huyo kufanya hivyo na kwamba walikuwa
wakimfuatilia kwa muda mrefu.
“Kilichotokea ni hicho, vijana wa Red
Brigade ndio waliomtoa ukumbini, baada ya kumbaini kukichafua chama, kwani
laptop yake baada ya kuchunguzwa na wataalamu wetu walijiridhisha ni yeye ndiye
aliyetuma ujumbe huo,” alisema Lema.
Katibu wa Chadema Kanda ya Kaskazini,
Amani Golugwa alitaja tuhuma zinazomkabili Mwigamba kuwa ni pamoja na kusema
uongo, kupotosha taarifa za chama na kuchonganisha viongozi kupitia mtandao wa
kijamii ya Jamii Forums.
Katika andiko lake kwenye mtandao,
Mwigamba anadaiwa kuwatuhumu viongozi wa juu wa Chadema akiwamo Mwenyekiti wa
Taifa, Freeman Mbowe na Katibu Mkuu, Dk Wilbrod Slaa kuwa wamechakachua katiba
ya chama hicho kuhusu ukomo wa nafasi za uongozi ili kujinufaisha binafsi.
Golugwa alisema kuwa baada ya kubanwa
kwenye kikao, Mwigamba alikiri kuandika na kurusha taarifa hizo kwenye
mitandao, lakini alipotakiwa kukabidhi kompyuta yake ili ichunguzwe na
wataalamu wa mawasiliano wa chama hicho aligoma, hali iliyozua tafrani kati
yake na walinzi wa chama hicho (Red Brigade), waliolazimika kutumia nguvu
kumdhibiti.
Purukushani zilivyotokea
Habari zaidi zinaeleza kuwa katika
harakati za kutaka kumnyang’anya Mwigamba kompyuta yake, mwenyekiti huyo wa
Chadema mkoani Arusha alianza kushambuliwa na baadhi ya viongozi wa Chadema,
kabla ya kufanikiwa kumdhibiti.
Zinaeleza kuwa katika tukio hilo
kulitokea pia kurushiana maneno na matusi ya nguoni kati yake na viongozi
wengine wa chama hicho akiwamo Lema.
Baadaye Lema aliliambia gazeti hili
kwamba katika purukushani hizo Mwigamba alimrushia ngumi ambayo hata hivyo
aliikwepa.
Alisema kuwa wanakusudia kumfungulia
kesi Mwigamba ya kukichafua chama chao katika mitandao ya kijamii.
Hata hivyo, alisema kikao chao
kiliendelea jana bila ya vurugu zozote na kuweka mikakati ya kushinda majimbo
yote ya Kanda ya Kaskazini mwaka 2015 na kuchukua nchi katika uchaguzi huo
ujao.
Adhabu kwa Mwigamba
Katika hatua nyingine Chadema,
kimemsimamisha uongozi Mwigamba kwa tuhuma za kukisaliti, kukihujumu chama
hicho na viongozi wake.
Akitangaza uamuzi huo mbele ya
waandishi wa habari jijini Arusha jana, Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya
Kaskazini, Israel Natse alibainisha kuwa uamuzi wa kumsimamisha Mwigamba katika
nyadhifa zote za uongozi ndani ya chama ulifikiwa na kikao cha Baraza la
Uongozi wa Kanda ya Kaskazini kilichokutana juzi.
Alisema kuwa Mwigamba amesimamishwa
kwa muda usiojulikana kupisha uchunguzi wa tuhuma dhidi yake na kuonya kuwa
iwapo tuhuma zitathibitishwa, hatua nyingine za kinidhamu zitafuata kulingana
na kanuni na katiba ya Chadema.
“Kwa sasa Mwigamba anatuhumiwa
kuvunja sura ya kumi, kifungu cha 10.1 kifungu kidogo cha 8, 9 na 10 ya katiba
ya Chadema inayozungumzia maadili ya uongozi,” alisema Natse.
Akifafanua zaidi alisema kuwa sura na
vifungu hivyo vinakataza kiongozi wa chama hicho kutoa tuhuma dhidi ya viongozi
wenzake bila kufuata vikao halali vya kikanuni na kikatiba.
Chanzo: mwananchi
No comments:
Post a Comment