na Happiness Katabazi
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar
es Salaam, imewaachia huru Waziri wa zamani, Arcado Ntagazwa na wenzake
waliokuwa na kesi na kujipatia mali kwa njia ya udanganyifu zenye thamani ya sh
milioni 74.9, baada ya kuwaona hawana hatia na hawakutenda kosa hilo.
Sambamba na hilo, mahakama hiyo
imemshauri mlalamikaji katika kesi hiyo ambaye ni Noel Severe kufungua kesi ya
madai kama walivyofanya hivi karibuni, ambapo walifungua kesi ya madai dhidi ya
Ntagazwa.
Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo, Gene
Dudu, alisema kuwa kesi hiyo ya jinai namba 108/2012 aliyoitolea hukumu jana,
haikupaswa kuwa jinai bali ya madai.
Akisoma hukumu hiyo, saa tano
asubuhi, Dudu alisema upande wa Jamhuri uliokuwa ukiwakilishwa na Wakili wa
Serikali, Charles Anindo, katika harakati zake za kutaka kuthibitisha kesi yake
ulileta mashahidi watano wakati upande wa washitakiwa waliokuwa wanatetewa na
wakili wa kujtegemea, Alex Mshumbusi, ulileta mashahidi wanne, ambao ni
washitakiwa wenyewe na shahidi mmoja.
Hakimu Dudu alisema mahakama yake
ilipata fursa ya kuchambua ushahidi wa pande zote mbili na mwisho wa siku
ikabakiwa na swali moja la kujiuliza kuwa, je, ni kweli washitakiwa hao
walitenda kosa kinyume cha kifungu cha 320 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya
mwaka 2002?
Aliongeza kuwa kwa mujibu wa kifungu
hicho ni lazima mtuhumiwa awe ametoa taarifa za uongo kwa mlalamikaji ili
ajipatie kitu fulani kwa njia hiyo ya uongo na awe na nia ovu wakati akitaka
kujipatia mali hizo.
“Lakini kwa mujibu wa ushahidi uliopo
mahakamani, imeonesha wazi kabisa Ntagazwa na mshitakiwa wa pili ambao ni
wajumbe wa bodi wa taasisi ya Ford walitoa oda kwa Kampuni ya Visual Storm
ambayo Mkurugenzi wake ni Severe, ya kuomba watengenezewe fulana 5,000 na
kapelo Korea 5,000, ambapo walifanya hivyo baada ya kikao cha bodi kutenga
bajeti ya kutengenezwa kwa mavazi hayo.
“Mavazi hayo yaligawiwa bure kwa umma
siku ya kumbukumbu ya kifo cha hayati Julius Nyerere, wakiwa na lengo la
kutokomeza ufisadi wakati wa kumuenzi kiongozi huyo, kwa ahadi kuwa wangelipa
ndani ya mwezi mmoja,” alisema Dudu.
Alisema hoja ya kwamba mshitakiwa wa
tatu ambaye ni mtoto wa Ntagazwa, Dk. Webhale Ntagazwa, kuwa ndiye alitoa oda
ya kuchapwa kwa fulana na kofia hizo, hakustahili kushitakiwa kwa kosa hilo kwa
sababu Ford ni taasisi na si mali ya mshitakiwa.
Dudu alisema utetezi wa washitakiwa
unaonesha waliandika barua kwa wafadhili wakiomba fedha za kuweza kufanikisha
mradi wao wa kutaka kumuenzi Nyerere siku ya kumbukumbu ya kifo chake Oktoba
14, na wafadhili hao waliwakubalia waendelee na taratibu za kuchapisha fulana
na kwamba watatoa fedha za kulipia.
Lakini kabla ya tamasha kufanyika,
Ntagazwa na wenzake walishtukia fulana zao hizo zikibadilishwa nembo na
kuonekana ni za Chama Cha Jamii (CCJ), hali iliyosababisha mfadhili
aliyewaahidi fedha kujitoa akidai hawafadhili vyama.
“Mahakama hii imeona habari hiyo
iliyochapishwa kwenye gazeti la Mtanzania, ambapo hata washitakiwa waliandika
barua kwa IGP Said Mwema kulalamika fulana na kofia zao kuhujumiwa, hivyo
kusababisha washitakiwa wajikute wakishindwa kulipia gharama za uchapishaji kwa
kampuni ya Severe baada ya mfadhili wao kujitoa,” alisema.
Baada ya hakimu huyo kusoma hukumu,
Ntagazwa aliangua kilio nje ya mahakama akisema: “Yaani kumuenzi Nyerere ndiko
kulikosababisha nifunguliwe kosa la jinai? Tena polisi walivyo na roho mbaya na
katiri siku wanakuja kunikamata nyumbani walinikamata uchi wa mnyama nikiwa
bafuni naoga kwa sababu nimehamia CHADEMA.”
Mbali na Ntagazwa, washitakiwa
wengine ni mtoto wake, Dk. Webhale Ntagazwa na mshitakiwa wa kwanza ni Senetor
Mirelya (60).
Aprili 23, mwaka 2012, ilidaiwa
mahakamani hapo na wakili wa Serikali, Ladislaus Komanya, kuwa Oktoba 22 mwaka
2009 huko Msasani Mikoroshini, washitakiwa hao kwa nia ovu walijipatia fulana
5,000 na kofia 5,000 zenye thamani ya sh milioni 74.9 kutoka kwa Noel Severe,
kwa makubaliano kuwa wangemlipa katika kipindi cha mwezi mmoja tangu
walipochukua vifaa hivyo lakini walishindwa.
Chanzo:
Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment