Wednesday, October 30, 2013

Mapinduzi mapya yapangwa UVCCM



Mwenyekiti wa UVCCM, Sadifa Hamisi Juma (katikati) Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana (kulia) wakiimba nyimbo ya chama hicho kabla ya kuanza kikao cha Baraza Kuu la jumuiya hiyo kilichofanyika White House, mjini Dodoma jana. Kushoto ni Katibu wa UVCCM, Sixtus Mapunda. Picha na Edwin Mjwahuzi.

Baadhi ya wajumbe wa Baraza Kuu la Jumuiya ya Vijana wa CCM (UVCCM), wameanza kupanga upya mikakati ya kuwang’oa viongozi wa juu wa jumuiya hiyo baada ya kushindwa kwa mpango uliokuwa umepangwa kutekelezwa wakati wa kikao cha baraza hilo kilichofanyika juzi mjini Dodoma.

Wanamapinduzi walikuwa wamepanga kuwatoa madarakani Mwenyekiti wa UVCCM, Sadifa Juma Khamis na makamu wake, Mboni Muhita, lakini jaribio hilo
lilishindwa kutokana na kile kilichoelezwa kuwa ni wahusika kutojipanga vizuri, pia uwapo wa Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana katika mkutano huo.
Kinana anatajwa kukwamisha mapinduzi yaliyokusudiwa kutokana na kauli yake aliyoitoa wakati akifungua mkutano huo kwamba haukuwa kwa ajili ya kuibomoa jumuiya bali kuijenga, hali ambayo iliwafanya wajumbe waliokuwa na ajenda ya kumng’oa mwenyekiti kunywea.

Hata hivyo, jana gazeti hili lilielezwa kuwa baadhi ya wajumbe hawakuridhika na hatua ya kutokujadiliwa kwa hali ilivyo ndani ya UVCCM, hivyo wameamua kujipanga upya ili kutekeleza azma yao ya kuwasulubu viongozi wao katika mkutano ujao.
Mmoja wa wajumbe wa kikao hicho alisema kumekuwa na woga unaowafanya viongozi wa juu wa UVCCM kutoruhusu kuwapo kwa ajenda zaidi ya moja katika vikao vya Baraza Kuu na kwamba huo ni utumiaji mbovu wa rasilimali za jumuiya.

“Kikao kimoja cha baraza kinagharimu zaidi ya Sh60 milioni, lakini mwaka huu pekee tumefanya vikao vitatu kwa hiyo tumetumia zaidi ya Sh180 milioni. Fedha hizi zingeweza kugharimia mambo mengine kama uhaba wa kadi na kanuni za jumuiya kwenye ngazi za chini,” alisema mmoja wa wajumbe kutoka mikoa ya Kanda ya Kati, huku akiomba jina lake lihifadhiwe.

Alisema kwa mujibu wa kanuni za jumuiya hiyo, kikao cha Baraza Kuu kinapaswa kuwa kimoja kwa mwaka, lakini mwaka huu tayari wamefanya vikao vitatu ambavyo kimsingi havina tija kwani hakuna kilichojadiliwa kutokana na woga wa viongozi.
Mjumbe mwingine kutoka mikoa ya Kanda ya Kaskazini alisema jumuiya imeshindwa kuteua makamanda wa wilaya na mikoa kwa muda mrefu, pia kutofanya uteuzi wa wagombea wa nafasi za chipukizi katika ngazi za wilaya na mikoa.

“Mwakani tunakabiliwa na Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, lakini cha ajabu hadi sasa tuna viporo vingi, mikutano kama hii ingetumika kufanya kazi hizo badala ya kujadili ajenda moja tu kama tulivyofanya Zanzibar mwezi uliopita na jana (juzi) hapa Dodoma,” alisema.

Hata hivyo, Katibu Mkuu wa UVCCM, Sixtus Mapunda akijibu hoja hiyo alisema: “Uhai wa jumuiya ni vikao, kwa hiyo siyo kosa kufanya vikao hata kama vitakuwa ni zaidi ya 10 kwa sababu katika vikao ndiko mambo muhimu yanakojadiliwa”.
Kuhusu uteuzi wa makamanda wa vijana wa wilaya na mikoa, Mapunda alisema kazi hiyo ilifanyika na kukamilika juzi katika kikao cha Kamati ya Utekelezaji cha jumuiya hiyo na kwamba suala la wagombea wa chipukizi nalo litakamilishwa.

Sarakasi za Sadifa
Uchambuzi wa kisiasa unaonyesha kuwa Sadifa alifanya mambo mawili makubwa katika kuwakabili wapinzani wake waliokuwa wamenuia kumng’oa katika nafasi yake.
Kwanza alikesha akiomba radhi katika vikao vilivyowahusisha wenyeviti wa UVCCM wa mikoa na baadaye wajumbe wengine wa Baraza Kuu na pili ni hatua yake ya kumteua hasimu wake kisiasa, Paul Makonda kuwa mmoja wa wakuu wa idara za umoja huo.

Wakati huo huo, Baraza la UVCCM, limeitaka Serikali kurejesha bungeni kwa hati ya dharura muswada wa marekebisho ya tozo ya Sh1000 kwa kila kadi ya simu.
Mapunda akizungumza na na waandishi wa habari jana alisema “Lengo ni kufanikisha malengo ya kufikisha mawasiliano ya simu kwa Watanzania wengi kwa haraka”.
Tozo hiyo ya Sh1000 kwa kila kadi ya simu, imetokana na sheria mpya ya fedha ya mwaka huu iliyopitishwa na Bunge . Hatua hiyo ya Serikali inalenga kukusanya Sh 178 bilioni katika Bajeti ya 2013/2014.
Chanzo: Mwananchi

No comments: