Dar es Salaam. Siku moja baada ya
maudhui ya Ripoti ya Tume iliyoundwa kuchunguza matokeo ya kidato cha nne ya
mwaka jana kuwekwa wazi, wadau wa elimu wamekiri na kusema kuwa mfumo wa elimu
ya Tanzania upo katika hali mbaya.
Akizungumza na gazeti hili jana,
Mbunge wa kuteuliwa na Rais, James Mbatia alisema matokeo ya tume hiyo
yanaonyesha udhaifu wa hali ya juu katika sekta ya elimu jambo ambalo
alishawahi kulisema katika hoja maalumu bungeni.
Mbatia, ambaye pia ni Mwenyekiti wa
NCCR- Mageuzi, alisema alishawahi kuishauri Serikali kuufumua mfumo wa elimu
nchini na kuanza upya ili kunusuru taifa la kesho ambalo ndilo linaloathirika
na rasilimali watu zisizo na ubora.
Matokeo ya kidato cha nne ya mwaka
jana yalionyesha kuwa asilimia 60.6 ya wanafunzi Tanzania walipata alama sifuri
na wanafunzi 23,520 sawa na asilimia tano ndiyo waliofaulu jambo ambalo
lilisababisha Waziri Mkuu Mizengo Pinda kuunda tume ya kuchunguza matokeo hayo.
Baadaye, mitihani hiyo ilisahihishwa
upya na Pinda kukabidhiwa matokeo Juni, mwaka huu.
“Nilishasema katika hoja yangu
bungeni Januari 31 na Februari 1, mwaka huu nikamwomba waziri anionyeshe
mitaala ya elimu ya sasa, lakini hakuitoa,” alisema Mbatia.
Mbatia alisema ili taifa hili
liondokane na janga la elimu lililopo halina budi kukubali kuwa ni kweli
Tanzania ipo katika janga la elimu na kuunda dira ya elimu itakayotuongoza
katika safari ya elimu nchini.
Mbatia aliongeza kuwa elimu ya
Tanzania ipo mahututi na kuwa kila mwaka wanafunzi wanaomaliza katika shule
mbalimbali hawana sifa za kutosha za kuweza kushindana katika masoko ya
kimataifa.
“Tumeshaanza kuona taifa linaangamia
kwa sababu ya ubovu wa elimu, ni lazima tukiri hilo kwa sababu hata Rais
alikiri na kuikubali hoja yangu Aprili 30 mwaka huu alipokuwa mkoani Mbeya”
alisema Mbatia
Mbunge huyu ambaye awali aliteuliwa
kuwa miongoni mwa wajumbe wa tume ya uchunguzi wa matokeo haya na kukataa
kushiriki alisema, ili Serikali iondokane na janga hili haina budi kuunda
Kamati ya Bunge ambayo itaisimamia Serikali na kutoa mawazo mapana kuhusu
elimu.
Mbatia alishauri Bunge lisiegemee
itikadi za vyama au porojo za kutaka sifa za kisiasa na badala yake suala la
elimu lijadiliwe kwa maslahi ya taifa.
Mdau mwingine wa elimu, Dk Method
Samwel, ambaye ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Elimu cha Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam (DUSE), alisema tatizo la elimu hapa nchini lielekezwe zaidi kwenye
mfumo uliopo kuliko laumu taasisi au mtu mmoja mmoja.
Dk Samwel alisema tangu zamani mfumo
wa elimu umekuwa ni wa kudorora na haya ni matokeo ya mfumo huo ambao haukuwa
na misingi imara kwa muda mrefu.
Alitolea mfano wanaokwenda kusomea
ualimu wengi ni wale waliofeli kwa kupata daraja la nne, jambo ambalo
linasababisha wataalamu wa kada hiyo kuwa ni wale waliofeli pekee.
“Yapo mambo mengi yanayotakiwa
kufanyiwa kazi katika sekta ya elimu Tanzania, suala la kudai kuwa Baraza la
Mitihani na Taasisi kuwa ndizo taasisi zenye makosa, hazina ukweli,” alisema.
Hata hivyo, Dk Samwel alisema, tume
hiyo bado ina maswali mengi ya kujibu kulingana na walichokisema katika sehemu
ya ripoti yao.
“Nashindwa kuelewa kwa sababu kila
nikisoma majibu ya tume hiyo napata maswali mengi zaidi. Kwa mfano, walimu
waliofanya mtihani wakafeli walipewa muda wa kujiandaa? “ alihoji na kuongeza:
“Na kuhusu mitihani ya Tanzania
kuonekana kuwa ni migumu zaidi, Je waliwapa mitihani ya Tanzania wanafunzi wa
nchi nyingine au walitumia mbinu gani kupata matokeo hayo?”
Hata hivyo, Mkuu wa Kitivo cha Elimu
wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Kitila Mkumbo, alipinga ripoti ya tume hiyo
na kusema kuwa wamepotosha taarifa kwani tatizo halikuwa katika mtihani bali ni
wanafunzi wenyewe wamefeli.
Dk Mkumbo amesema tatizo si la
walimu, wala baraza, wala mitihani yenyewe bali ukweli utabaki kuwa wanafunzi
walifeli mtihani wa Kidato cha Nne kwa sababu ya mfumo mbovu wa elimu.
Mhadhiri huyo alihoji tena kuwa tume
hiyo ilitumia njia gani kujua kuwa mtihani wa Sayansi ulihitaji saa sita
kuufanya na ni kwa mbinu gani waliupima mtihani wa Tanzania na kujua kuwa ni
mgumu kuliko mitihani mingine.
“Nilipata ripoti fulani iliyoonyesha
kuwa mitihani ya Tanzania ni mizuri na haina matatizo, ripoti ilionyesha kuwa
haina chembe ya mashaka na inatungwa kwa ustadi. Tusitafute sababu, tatizo si
mitihani ni wanafunzi wenyewe wamefeli,” alisema.
Pia, Dk Mkumbo alisema kuwa ni dharau
kubwa kusema kuwa baadhi ya wasahihishaji hawakuwa na sifa kwani hilo ni tusi
kubwa kwa walimu kwani wao ndiyo wamekuwa wakisahihisha kila siku.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki
wa Shule Binafsi nchini,(Tamongsco), Albert Katagira alisema si kweli kuwa
mtihani ulikuwa mgumu bali tatizo lipo katika uandaaji wa wanafunzi.
“Mtihani ulikuwan sahihi kabisa,
mbona wanafunzi wengine walifaulu. Ni wanafunzi wenyewe, ambao nao hatuwezi
kuwalaumu moja kwa moja,” alisema Katagira.
Alisema taifa bado lina tatizo katika
mfumo wa elimu na kuweka mkazo katika masomo ya sayansi na hisabati ambayo
yanaonekana kuwa magumu kwa wanafunzi wengi.
Mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya
Mafinga, Mustapha Mambea alisema, mtihani wa Fizikia na Kemia haikuwa migumu,
lakini kuna mada kadhaa ambazo hawakufundishwa.
Profesa Mchome aongea
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na
Mafunzo ya Ufundi, Profesa Sifuni Mchome alisema kuwa wameshindwa kuiweka
hadharani ripoti hiyo kwa kuwa bado inafanyiwa kazi serikalini.
Profesa Mchome, ambaye ndio aliongoza
tume hiyo, alisema kuwa ripoti hiyo inatakiwa kupelekwa kwenye kikao cha Baraza
la Mawaziri kwa ajili ya kujadiliwa.
Alidokeza, hata hivyo, tayari
walikuwa wameanza kufanyia kazi baadhi ya vitu vinavyotakiwa kufanyiwa kazi
haraka kwenye ripoti hiyo.
Katibu Mkuu wa Necta, Dk Joyce
Ndalichako, ambaye ameomba likizo ya muda mrefu ikitafsiriwa pengine ndio
mwanzo wa utekelezaji wa ripoti hiyo.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment