Wednesday, October 23, 2013

TTCL YAJIAPIZA KUPAMBANA NA UHALIFU WA MITANDAO




Kampuni ya Mawasiliano Tanzania (TTCL) imejidhatiti kupambana na udanganyifu unaofanywa na baadhi ya watu kupitia mitandao ili kuwahakikishia wateja wake huduma bora.

Kauli hiyo ilitolewa na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni hiyo Dkt. Kamugisha Kazaura, wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya ufunguzi wa warsha ya wataalamu Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kutoka nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) iliyofanyika jijini Dar es salaam hivi karibuni.
Dkt. Kamuzora alisema kuwa TTCL ina vifaa vya kisasa kwa ajili ya ulinzi na mbinu za kukabiliana na wizi na udanganyifu katika mitandao, hivyo kuwakikishia wateja wake huduma bora.

"Tunalazimika kuwa na mbinu za ziada hata kama wahalifu wanaweza kuwa na utaalamu zaidi yetu," alisema Dkt. Kazura.
Aliongeza kusema kuwa tatizo la wizi na udanganyifu kwa njia ya mtandao ni kubwa na linahitaji kuwepo kwa sera ya udhibiti ya matumizi ya mtandao wa ndani, nje na hata katika ngazi ya kimataifa.

"Uhalifu wa mtandao ikiwemo wizi na udanganyifu ni tatizo ambalo hatupaswi kudhrau, ni kama ugonjwa unaohitaji tiba," alisema Dkt. Kazaura.
Alisema kuwa mkutano huo ulilenga kuja na mapendekezo ya kudhibiti tatizo hilo katika jumuiya.

"Tumekutana kuzungumzia wizi na udanganyifu wa mitandaoni na usalama wa mitandao hii na mapendekezo yatakayotolewa yatafikishwa kwenye mkutano wa Mawaziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC)," alisema.

TTCL ni moja ya taasisi zinazotakiwa kuhakikisha tatizo hilo linapungua na kuisha kabisa kutokana na jukumu lake kubwa la kusimamia Mkongo wa Mawasiliano wa Taifa ambao kupitia kwake huduma za kimtandao zimeshaanza kutolewa ndani na nje ya nchi.
Alisema kuwa nchini Tanzania Mkongo wa Taifa umeboresha huduma za mawasiliano na kusaidia kuboresha huduma za mawasiliano kwa kutumia mitandao mbalimbali ikiwemo ya intaneti.

Kupitia mitandao hiyo watu hutuma na kupokea fedha, pia hupata taarifa mbalimbali, sasa baadhi ya watu hutumia fursa ya kukua kwa tehama kufanya wizi na udanganifu huo mitandaoni.
Chanzo: majira

No comments: