Wednesday, October 30, 2013

YANGA YAITIMULIA VUMBI SIMBA



Mabingwa watetezi Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga jana imewafanyia maafande wa Mgambo Shooting baada ya kuwatandika mabao 3-0 katika mechi ya ligi hiyo iliyofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kwa matokeo hayo Yanga, itakuwa imefikisha pointi 22 katika msimamo wa ligi hiyo na kuwaacha nyuma watani wao Simba wenye pointi 20.

Yanga sasa imechumpa hadi nafasi ya tatu na kuiacha Simba nafasi ya nne, Azam ikiongoza ligi hiyo ikiwa na pointi 23 sawa na Mbeya City isipokuwa zimezidiana kwa idadi ya mabao.
Mpira ulianza kwa kasi ambapo timu zote zilikuwa zikishambuliana kwa zamu ambapo dakika ya 11, Omari Yassin aliikosesha Mgambo bao baada ya kupata nafasi nzuri lakini akashindwa kufunga.

Yanga ilipata bao dakika ya 28 kupitia kwa beki, Mbuyu Twite baada ya kuachia mkwaju wa adhabu uliokwenda moja kwa moja wavuni.
Kipindi cha pili Yanga iliingia kwa nguvu na kuliandama lango la Mgambo ambapo dakika ya 50, Hamis Kiiza aliipatia timu hiyo bao la pili kwa mkwaju wa penalti baada ya Dedier Kavumbagu kuangushwa eneo la hatari.

Yanga ilihitimisha bao la tatu dakika ya 66 lililofungwa na Kavumbagu kuachia shuti akiunganisha krosi ya Simon Msuva.
Dakika za nyongeza Mgambo walipata nafasi nzuri ya kupata bao, baada ya Maalim Busungu akiwa katika nafasi nzuri akashindwa kufunga.

Baada ya mechi hiyo Kocha Mkuu wa Yanga, Ernie Brandts alisema amefurahishwa na matokeo hayo na kuwasifu wachezaji wake kwa ushindi huo.
Naye Kocha Mkuu wa Mgambo, Mohamed amekubaliana na matokeo lakini kipigo hicho kimekuja kutokana na kuchezesha wachezaji wengi wa timu B kutokana na anaowategemea kwenda mafunzoni.

Naye Rashid Mkwinda anaripoti kutoka Mbeya kuwa, wageni wa ligi hiyo, Mbeya City, wamezidi kuwa tishio, baada ya kuwafunga ndugu zao Prisons mabao 2-0 katika mechi iliyochezwa Uwanja wa Sokoine na kufikisha pointi 23 sawa na Azam FC inayoongoza ligi hiyo kwa idadi ya mabao

No comments: