Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharrif Hamad.
Na Mwinyi
Sadallah, Mwananchi
Wanasema Serikali inatumia fedha
nyingi kugharimia matibabu ya kiongozi huyo nje ya nchini, kinyume na ahadi
yake ya kutotibiwa nje.
Zanzibar. Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa
Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Sadifa Juma Khamis amesema baadhi ya viongozi ndani
ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa, wameshindwa kutekeleza wajibu wao.
Amesema wajibu huo ni pamoja
na kushindwa kutatua kero za madaktari na kusababisha kuzorota kwa huduma
za afya visiwani humo. Sadifa aliyasema hayo jana alipokuwa akihutubia mkutano
wa hadhara katika Uwanja wa Vuga katika Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja.
“Serikali imekuwa ikitumia gharama
kubwa kumhudumia kwa matibabu, Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharrif
Hamad, itakumbukwa aliwahi kuwaahidi wananchi wa Zanzibar kuwa akiwa kiongozi
atahakikisha anatibiwa hapa hapa badala ya kusafirishwa nje ya nchi,” alisema.
Wabara waishio Zanzibar
Kiongozi huyo wa UVCCM, alisema watu
wa Tanzania Bara wanaoishi Zanzibar, si wakimbizi kwa mujibu wa Katiba ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.
Sadifa alisema wapinzani wanaohoji
uhalali wa watu hao kuishi na kufanya kazi Zanzibar, hawafahamu haki ya
kila mtu kikatiba kwa maana ya kuwa huru kuishi na kufanya kazi katika sehemu
yoyote ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Alisema ibara ya 11 na 26 ya katiba
imeweka wazi kwa kila Mtanzania ana haki ya kuishi sehemu atakayo ndani ya
Jamhuri ya Muungano.
Huku akishangiliwa na wanachama wa
CCM alisema sera za ubaguzi hazitasaidia kujenga amani na umoja wa kitaifa
baada ya kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Novemba mwaka 2010.
Naibu Katibu Mkuu wa UVCCM Zanzibar,
Shaka Hamdu Shaka, alisema umoja huo umeamua kuchunguza kikundi cha watu wenye
asili ya India ambao wamekuwa wakipinga misingi ya Mapinduzi na Muungano
wa Tanganyika na Zanzibar.
Alisema ni jambo la kushangaza kuona
watu hao wakiwa katika mstari wa mbele kuhoji uhalali wa Muungano wa Tanganyika
na Zanzibar, wakati hakuna muafrika anayeweza kwenda kuhoji uhalali wa harakati
za ukombozi wa India au Iran kama hali ilivyojitokeza visiwani Zanzibar.
Alisema kitendo hicho hakikubaliki.
No comments:
Post a Comment