Rais
Jakaya Kikwete, amesema ni aibu Serikali kudaiwa na wakulima wa Wilaya ya
Ludewa, mkoani Njombe ambao wameiuzia mahindi yao.
Kutokana
na hali hiyo , aliwahakikishia wakulima hao kulipwa fedha zao haraka
iwezekanavyo.
Rais
Kikwete aliyasema hayo juzi kwa nyakati tofauti wilayani humo ikiwa ni
mwendelezo wa ziara zake za kukagua, kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo
mkoani humo.
“Ni
kweli Serikali inadaiwa sh. bilioni 17 ambazo ni deni la wakulima wa mikoa
mbalimbali nchini ambao walituuzia mahindi yao msimu uliopita kwa Wakala wa
Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA),” alisema.
Akipokea
Ripoti ya Maendeleo wilayani humo, Rais Kikwete alisema wakulima wa Wilaya hiyo
pekee bado wanaidai serikali sh. bilioni 3.115 za mahindi tani 6,231
waliyoyauza NFRA.
Alisema
hadi sasa, wakulima wilayani humo wamelipwa sh. bilioni 2.839 zilizotokana na
tani 5,679 za mahindi ambapo NFRA ililenga kununua tani 13,000 lakini imeweza
kununua tani 11,911 ingawa sehemu kubwa ya kiasi hicho hakijalipiwa na
Serikali.
“Hii
ni aibu, Serikali haiwezi kudaiwa na wakulima hivyo hizi fedha zitalipwa tu,”
alisema Rais Kikwete na kuelezea hatua binafsi alizochukua kuhakikisha deni
hilo linalipwa.
Aliongeza
kuwa, Serikali itaangalia uwezekano wa kununua tani 2,972 za mahindi ya msimu uliopita
zilizobakia mikononi mwa wakulima wa Wilaya hiyo.
“Nimeambiwa
NFRA bado inahitaji tani 40,000, ili kukamilisha shehena ya idadi ya tani
250,000 za mahindi kwa ajili ya Hifadhi ya Taifa mwaka huu...nitawaambia
waangalie kama kuna uwezekano wa kununua tani zilizobaki kwa wakulima wa
Ludewa,” alisema.
Rais
Kikwete pia alizungumzia maombi ya wananchi wa Ludewa kutaka Serikali inunue
meli ili kuchukua nafasi ya Mv. Mbeya iliyozama katika Ziwa Nyasa ili
kurahisisha usafiri ndani ya ziwa hilo ambalo linapakana na Wilaya hiyo.
Alisema
Serikali itanunua meli kwa kwa ajili ya usafiri katika Maziwa Makuu nchini,
kabla ya mwaka 2015 na zinaweza kuwa mbili badala ya moja katika Ziwa Nyasa,
Victoria, Tanganyika.
“Tunajua
kuwa meli ya Mv. Mbeya ilizama katika Ziwa Malawi na nyingine katika maziwa
mengine makubwa ya Tanganyika na Victoria...mimi katika kampeni zangu niliahidi
nitanunua meli moja kwa kila ziwa,” amesema Rais Kikwete na kuongeza;
“Tumeagiza
meli tatu kutoka Korea Kusini kwa sasa zinajengwa, pia tumeagiza meli nyingine
tatu kutoka nchini Denmark nazo zinajengwa hivyo tunaweza kupata meli zaidi ya
moja katika maziwa yote matatu na mbili nitazizindua kabla ya kumaliza kipindi
changu cha uongozi mwaka 2015,” alisema.
Alisema
kero nyingine zilizoibuliwa na wakazi wa Wilaya hiyo pamoja na ujenzi wa daraja
kwenye Mto Ruhuhu, litajengwa.
Wakati
huo huo, Rais Kikwete amewaonya wananchi wa Wilaya hiyo wasiwe hodari wa kuuza
ardhi na mashamba yao ambayo yatakuwa na umuhimu mkubwa miaka michache ijayo
kutokana na matunda makubwa ya uwekezaji.
Alisema
Serikali inatarajia kuwekeza katika miradi ya chuma, makaa ya mawe na madini
mengi yanayopatikana wilayani humo.
Rais
Kikwete aliyasema hayo juzi katika mkutano wa hadhara uliofanyika wilayani humo
na kusisitiza kuwa; Msipochangamka mapema na kuanza kuangalia namna ya
kunufaika na rasilimali za hapa, mtageuka ‘manokoa’ wa watu wengine kwenye
ardhi yenu wenyewe,” alisema Rais Kikwete
Chanzo:
Majira
No comments:
Post a Comment