• Makamu wake asema hajui
kinachoendelea
na Josephat Isango
Hata
hivyo, kamati hiyo imezua mashaka ya vyama hivyo kuhojiwa kwani pamoja na Zitto
kutoa taarifa kuwa atakuwa nje ya nchi kikazi, makamu wake, Deo Filikunjombe,
naye amedai yuko jimboni na hajui kinachoendelea kuhusu vyama hivyo.
Akizungumza
na gazeti hili jana kuhusu madai ya vyama hivyo kutopewa taarifa ya wito kwa
maandishi, Filikunjombe alisema yuko jimboni kwa wapiga kura wake.
“Naomba
usubiri niweze kuwasiliana na wajumbe wengine walioko kwenye vikao Dar es
Salaam ili wao ndio waweze kulisemea jambo hilo ingawa huku niliko mtandao ni
tatizo,” alisema mbunge huyo wa Ludemwa (CCM) ambaye hakupatikana hewani tena.
Wakati
makamu mwenyekiti wa PAC akisema hivyo, makatibu vyama vya CCM, CHADEMA, CUF na
NCCR-Mageuzi walilihakikishia gazeti hili jana kwamba hawakuwa na mwaliko wa
kufika mbele ya kamati hiyo.
Katibu
Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa,
alisema hawajapata barua ya mwaliko kukutana na PAC.
“Mimi
nina mwaliko mwingine wa kuonana na Msajili wa Vyama vya Siasa Oktoba 24 mwaka
huu, lakini ni kwa masuala tofauti kabisa hayana uhusiano na PAC,” alisema.
Naye
Katibu Mkuu wa NCCR- Mageuzi, Samuel Ruhuza, alisema hajapata mwaliko huo wa
PAC lakini akasisitiza kuwa akipata atahudhuria ili kujua nini kinazungumzwa
huko.
Naibu
Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Julius Mtatiro, aliliambia gazeti hili
kuwa hadi jana walikuwa hawajaletewa barua ya mwaliko. Na kwamba hawatahudhuria
hadi wapate barua.
Alipotafutwa
Katibu wa Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, naye
alisema hawakuwa na mwaliko wowote wa barua hadi jana.
Wiki
iliyopita Zitto alisema kuwa vyama vya CHADEMA, CCM, CUF, TLP, UDP, DP, Chausta
na APPT-Maendeleo vinatakiwa kufika mbele ya PAC Oktoba 25 mwaka huu, kwa ajili
ya kujieleza kwa nini hesabu zao za ruzuku hazijakaguliwa na Mkaguzi Mkuu wa
Hesabu za Serikali (CAG) na kuwasilishwa kwa Msajili wa Vyama.
Vyama
vikubwa vinne vya CCM, CHADEMA, CUF na NCCR-Mageuzi vimeingia kwenye msuguano
wa maneno na PAC, vikimtuhumu Zitto kwa kuvijumuisha kwenye kapu moja wakati
vingine hesabu zao zimekaguliwa na kuwasilishwa kwa msajili.
Zitto
alisema tangu mwaka 2009, vyama vyote vya siasa vinavyopata ruzuku ya serikali
havijawahi kupeleka ripoti yoyote ya ukaguzi wa fedha kwa CAG, huku vikiwa
vimepokea ruzuku ya jumla ya sh bilioni 67.7.
Alitaja
mgawanyo huo kuwa ni CCM ambacho kimekwishapokea ruzuku ya sh bilioni 50.9,
CHADEMA sh bilioni 9.2, CUF sh bilioni 6.3, NCCR-Mageuzi sh milioni 677, UDP sh
milioni 333, TLP sh milioni 217, APPT Maendeleo sh milioni 11, DP sh milioni
3.3 na Chausta sh milioni 2.4.
Alisema
sheria inavielekeza vyama vyote vya siasa kupeleka ripoti zao za ukaguzi kwa
CAG, jambo ambalo vimekuwa havifanyi.
Wasomi
wanena
Wachambuzi
wa siasa nchini wamevitaka vyama vya siasa kuacha kulumbana na badala yake
vikubali kuhojiwa na PAC.
Wito
huo ulitolewa jana na wasomi hao, kutokana na vyama kugomea wito wa PAC vikidai
taarifa ya kutokaguliwa si ya kweli.
Mhadhiri
wa Chuo cha Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Bashiru Ally, alieleza kushangazwa na
malumbano hayo kwani suala la ruzuku linatolewa kwa mujibu wa sheria.
Alifafanua
kuwa kujulikana kwa fedha hizo kwa wananchi ni haki yao kwa kuwa inatoka katika
hazina ya serikali ambayo ni kodi za umma, hivyo ni muhimu zijulikane matumizi
yake.
Dk.
Bashiru alisema kukaguliwa matumizi ya ruzuku hiyo ni dhana ya uwajibikaji na
kwamba zipo ofisi zilizopewa dhamana ya kufanya hilo.
Alibainisha
kuwa vyama vya siasa vinaruhusiwa kuwa na mfumo wake wa ndani lakini pia
serikali chini ya ofisi ya Waziri Mkuu ambayo madaraka yake yamekasimiwa ofisi
ya Msajili wa Vyama vya Siasa ndiyo yenye jukumu la kufanya kazi hiyo ya
kuhakiki wa ruzuku.
Alisema
tatizo lililosababisha hali hiyo ni la kimfumo kutoka kwa vyama vya siasa,
Ofisi ya Waziri Mkuu na Kamati ya Bunge; jambo hilo lisizue mjadala usiokuwa na
faida kwa umma.
Naye
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine cha Mwanza (SAUT), Prof. Mwesiga
Baregu, alisema malumbano hayo hayana manufaa katika hatua yaliyofikia kwani
inakuwa ya kujitetea badala ya vyama kukaa na kujindaa kuhojiwa mbele ya PAC.
Alitaka
kusitishwa malumbano hayo kutokana na kutokuwa na faida, bali wanachotakiwa
kufanya ni kukaa mkao wa kwenda kujieleza vizuri katika kamati hiyo waeleweke.
Alibainisha
kuwa iwapo kuna chama kitakuwa kimeshafanya hesabu zake kitaonyesha na kama
bado uamuzi utafanyika kwa kufuata taratibu zilizopo.
Kuhusu
ruzuku ya vyama, alisema ni jambo muhimu si kwa siasa au wanasiasa bali kwa
Watanzania kwani jambo lililoibuliwa ni jema kwa kuwa vyombo hivyo ndivyo vyenye
wajibu wa kuongoza na kuonyesha uadilifu.
Prof.
Baregu alisema upo uwezekano wa CAG na PAC kutounganisha kazi zao hapo nyuma,
hali aliyosema bado hawajachelewa ila wanachotakiwa kufanya ni kulishughulikia
kikamilifu badala ya kulaumiana.
Chanzo: Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment