Wananchi wenye hasira wakifunga njia
kwa kutumia vyuma vya kingo vya daraja kuzuia msafara wa Dkt.Emmael Nchimbi
kupita wakati akienda kwenye mkutano wa hadhara ambao baadae ulifanyika kwenye
viwanja vya shule ya sekondari ya kutwa ya matarawe iliyopo katika manispaa ya
Songea (picha na Gideon Mwakanosya)
Diwani wa kata ya Matarawe (CCM) Makene aliyesimama katikati
akijaribu kuwatuliza wananchi wa kata hiyo ambao walifunga barabara itokayo
mjini kwenda matarawe kwa zaidi ya masaa mawili wakimshinikiza mbunge wao Dkt.
Nchimbi awasaidie kulipanua daraja ambalo wamedai kuwa limekuwa likisababisa
ajari nyingi pamoja na vifo aliyesimama nyuma yake ni Dkt Nchimbi (picha na
Gideon Mwakanosya).
HABARI KAMILI
na Stephano Mango, Songea
MSAFARA wa Waziri wa Mambo ya Ndani
ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi, umepigwa mawe na wananchi waliojitokeza kuzungumzia
kero ya daraja la Matarawe, ambalo linadaiwa kusababisha vifo vya watu zaidi ya
watatu mwezi Oktoba mwaka huu.
Tukio hilo limetokea jana saa 10:00
jioni hadi saa 12:00, ambapo wananchi hao wakiwa na hasira walifanya fujo
wakimshinikiza Nchimbi ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini
awasaidie kupanua daraja hilo ambalo kwa muda mrefu limesababisha
kutokea kwa ajali za mara kwa mara katika eneo hilo.
Wananchi hao wa Kata ya
Matarawe, Manispaa ya Songea, wakiwamo waendesha pikikipiki maarufu
kwa jina la ‘yeboyebo’ walifunga barabara kwa zaidi ya saa mbili
huku wakifanya fujo za kung’oa kingo za daraja, kuweka magogo na
mawe katikati ya daraja na kuchoma matairi moto ili kumzuia
kiongozi huyo asiweze kupita na atoe majibu ya kina juu ya daraja hilo.
Hatua hiyo ilililazimu Jeshi la
Polisi kuwatawanya wananchi hao kwa kuwafyatulia mabomu ya machozi ili
kukabiliana na uharibifu pamoja na kuruhusu msafara huo uweze kupita.
Aidha, kufuatia vurugu hizo, Jeshi la
Polisi liliweza kuwashikilia watu wanane.
Hata hivyo Dk. Nchimbi alilazimika
kusimama na kushuka kwenye gari lake akiwa ameongozana na viongozi
mbalimbali wa chama na serikali akiwamo Mkuu wa Wilaya ya Songea, Joseph
Joseph Mkirikiti, ambapo aliwapa pole kwa ajali zinazotokea huku akiwataka
kuwa na subira wakati ombi lao linashughulikiwa.
“Natoa pole sana kwa msiba na ajali
ambazo zimetokea nimewasikia, na ninaahidi nitawajengea daraja
hili, kama nimeweza kujenga barabara hii kwa kiwango cha lami bila maandamano
wala kufungiwa barabara nitashindwa daraja?” alihoji.
Nchimbi alisema kuwa vitu hivyo
vinavyozungumzika hakuna haja ya kufanya maandamano na kuwataka wananchi hao
kuhudhuria mkutano wake kwa kuwa anajua ufinyu wa daraja hilo na ameahidi
kulifanyia maboresho zaidi.
Naye Diwani wa kata hiyo, James
Makene, aliungana na kundi la wananchi hao na kumueleza Nchimbi kuwa hiyo
ni changamoto ambayo wakazi wake wamekuwa wakilia kwa kipindi kirefu.
Aidha, Kamanda wa Polisi wa mkoa huo,
Deusdedit Msimeki, alisema kuwa kufuatia vurugu hizo tayari watu wanane
wanashikiliwa na wanaendelea kuhojiwa zaidi ili kuwabaini vinara wengine
waliosababisha fujo hizo.
Chanzo:
Tanzania Daima/ Mjengwablog
No comments:
Post a Comment